Monday, July 20, 2009

Milioni 70 zaibwa ATM

Jijini Dar es Salaam





Kwa tahadhari bofya na som kiungo hiki





Sikiliza hii

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata raia wawili wa Bulgaria wanaodaiwa kuiba zaidi ya sh milioni 70 katika mashine za kutolea fedha, ATM jijini Dar es Salaam.

Watuhumiwa hao, Nedko Stanchen (34) na Stella Nedekcheva (23) walikamatwa mwishoni mwa wiki jijini humo baada ya polisi kuweka mtego wakishirikiana na benki ya Barclays wilayani Kinondoni.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova amesema leo kuwa, vijana hao wanadaiwa kuhusika katika mtandao wa wizi wa fedha katika mashine za ATM za benki mbalimbali.

Amesema, polisi waliweka mtego baada ya mfanyakazi wa benki ya Barclays kugundua kuwa kuna vifaaa vilikuwa vimewekwa katika mashine za ATM.

Amewaeleza waandishi wa habari kuwa, mfanyakazi huyo alikuwa anafanya usafi, na kwa mujibu wa Kova, vifaa vilivyowekwa kwenye mashine za ATM ni kamera na kifaa cha kunakili taarifa za wateja zilizomo kwenye kadi za ATM.

Kwa mujibu wa Polisi, watuhumiwa hao wameiba fedha katika mashine za ATM za benki tofauti, na wamekutwa na kadi tano za ATM za benki ya Barclays, Stanbic, na vifaa mbalimbali vya mtandao huo wa wizi.

“Hawa watuhumiwa waliweza kuja na mbinu yao ambayo nahisi kuwa ni ya muda mrefu tangu waanze kuitumia tayari fedha nyingi zimeibwa, tumewakamata na vifaa maalumu vyenye uwezo wa kunakili taarifa za wateja toka katika kadi zao za ATM na hivyo kuwarahisishia kuchota fedha toka katika Mashine hizo na baada ya kubaini hilo tuliweka mtego mara moja na kufanikiwa kuwakamata” amesema Kova.

Wakati huo huo polisi katika kanda hiyo wamemkamata mkazi wa Mivinjeni, Dar es Salaam, Athumani Mbani(25), baada ya kukutwa na akiwa na vipande 42 vya meno ya Tembo vyenye uzito wa Kg.66.5, vikiwa na thamani ya zaidi ya Shilingi Milion 4.8.

Kamanda Kova amesema, kuwa vyanzo vya taarifa vimedai kuwa, nyara hizo zimetoka katika maeneo mbali mbali ya Ifakara katika Mkoa wa Morogoro.

Chanzo: Habari Leo


No comments: