Saturday, August 08, 2009

Je, Tunaweza Tukawa Na

Mrembo Wa Tanzania?”


Profesa Joseph L. Mbele

KWA wiki kadhaa nimewazia kuandika makala kuhusu mashindano ya urembo. Katika Tanzania ya leo, mashindano hayo yameshamiri katika miji mikubwa na yanazidi kuenea.

Kwa upande moja nimekuwa sipendezwi na mashindano hayo. Nimekuwa nikijiuliza kama yana maana gani katika jamii yetu, kwani ni wazi kuwa mwenendo wake ni wa kuigwa kutoka nchi za magharibi. Ninayachukulia kama ishara nyingine ya ukoloni mambo leo.

Kwa upande mwingine, nimelazimika kukubali kuwa yamesaidia kwa namna mmoja au nyingine kuitangaza nchi yetu, wakati washiriki wanapoenda nje wakiwa na bendera ya nchi yetu. Vile vile, washindi wa mashindano hayo wameweza kufanya mambo ya maana katika jamii yetu. Wamekuwa watu maarufu nchini, wenye mvuto na uwezo wa kuhamasisha shughuli mbali mbali za manufaa kwa jamii. Wengine wameweza kujijengea msingi wa kujiendeleza kimaisha, kama vile kuwa wanamitindo katika nyanja za kimataifa. Hayo nimeyawazia na kuyazingatia. Ni mifano ya manufaa yatokanayo na mashindano hayo.

Lakini duku duku haziishi. Masuali hayaishi. Bado ukweli uko pale pale kuwa mashindano hayo yanayoshamiri siku hizi ni mambo ya kuiga. Si yetu. Vigezo vinavyotumiwa ni vya kuigwa; si vyetu. Tunashinikizwa tufuate vigezo vya Ulaya. Kwa mfano, wanawake wanaoshiriki mashindano hayo ni lazima wawe wembamba, au wembamba sana. Wanene hawakubaliki.

Hii ni ajabu katika nchi yetu na bara letu kwa ujumla, ambamo vigezo vya uzuri wa mwanamke ni tofauti. Katika mila na desturi za makabila yetu, kuna vigezo vya urembo, tofauti na hivi vya Ulaya. Kwa ujumla, unene ni uzuri, jambo la kujivunia. Katika makabila mengi, kulikuwa na mila ya kuwanenepesha wasichana kabla ya kuolewa.

Pamoja kushamiri kwa mashindano ya urembo, siamini kuwa katika mioyo ya waTanzania, dhana ya kuuenzi unene wa mwanamke imetoweka. Bado unene wa mwanamke ni jambo linalomfanya avutie. Kwa nini basi, tunajitumbukiza katika mashindano ya urembo ambayo vigezo vyake ni tofauti na hisia zetu? Naamini kuna baadhi ya waTanzania, kama vile vijana waliokulia Ulaya au Marekani, ambao wanalelewa katika mtazamo wa huko walikokulia hata kwenye suala la vigezo vya urembo. Lakini je, hisia za Mtanzania wa kawaida ni zipi?

Mashindano ya urembo ni jambo la kawaida katika jamii za binadamu. Hapa Afrika hali ni hiyo hiyo, tangu enzi za mababu na mabibi. Kwenye ngoma ilikuwa ni sehemu maalum ya mashindano hayo. Katika utungo wake maarufu uitwao “Wimbo wa Lawino,” mwandishi Okot p’Bitek wa Uganda alielezea vizuri jadi hii ya wasichana na wavulana kushindana kwenye ngoma katika kabila la Acholi.

Ili tuwe na upeo mpana wa kujitambua, tujiulize, je, kwa mila na desturi zetu, vigezo vya urembo wa mwanamke ni vipi? Vigezo vya Mmasai ni vipi? Vigezo vya Mnyakyusa, Mmakonde, au Mhaya ni vipi? Je, tunaweza tukawa na mrembo wa Tanzania? Naamini kuwa, ili tuwe na mrembo wa Tanzania, ingebidi sisi wenyewe tukae tukubaliane vigezo badala ya kuiga vigezo vya Ulaya.

Leo hii, mashindano haya ya urembo ambayo yanatumia vigezo vya Ulaya yanazidi kushamiri nchini mwetu. Mwishowe yatafika hata vijijini. Hata katika vyuo vikuu vya Tanzania, mashindano hayo yanayotumia vigezo vya Ulaya yanapamba moto. Nilitegemea kuwa vyuo vikuu ni sehemu ya kutafakari masuala na mambo ya jamii, mahala pa kufanya uchambuzi na kujua baya na jema. Haipendezi kuona kuwa chuo kikuu, badala ya kuwa mahali penye watu wa kuongoza njia, panakuwa ni mahali pa watu waliopotea njia.

Huko Ulaya na Marekani baadhi ya watu wameanza kutambua madhara yanayoendana na mashindano ya urembo. Watu wameanza kutambua kuwa shinikizo wanalowekewa wanawake kuwa wembamba linawafanya wajitese kwa mazoezi, wajinyime chakula au wale vyakula vya aina fulani tu na kwa mpangilio fulani maalum. Matokeo yake, angalau kwa baadhi ya wahusika, ni kujikosesha lishe bora, kudhuru afya, na kuugua maradhi mbali mbali. Kuna pia matatizo ya kisaikolojia miongoni mwa wasichana. Hawajisikii vizuri au wanajichukia kwa kuambiwa kuwa hawapendezi kutokana na umbo lao. Wasichana na wanawake wanene wengi wanaishi na masononeko na hata kujichukia kutokana na suala la unene.

Nafahamu kuwa unene wa aina fulani ni dalili ya afya mbaya, au ni hatari kwa afya. Hakuna ubishi kuwa unene wa aina hiyo ni jambo lisilohitajika. Tatizo la mashindano ya urembo ni kuwa hata unene wa kawaida tu hauruhusiwi. Hapo ndipo penye tatizo.

Tufikirie masuala haya ili tuweze kuinusuru jamii yetu. Huko Ulaya, baadhi ya wanawake wanene wamechoshwa na hali ilivyo, na wanarudisha hadhi ya unene katika urembo. Wanaendesha mashindano ya uzuri wa wanawake wanene, kupinga haya mashindano yanayotamba, ambayo yanasifu wembamba tu.

Labda tunahitaji kujielimisha upya, ili tuweze kuliona suala la urembo kwa upeo mpana zaidi. Mwandishi wetu maarufu, Shaaban Robert, aliwahi kutunga shairi ambamo tunawasikia wanawake wakisifia uzuri wao. Mwanamke mnene anasifia unene wake, na mwembamba anasifia wembamba wake. Na wote wanafanya hivyo kwa ufasaha na mantiki nzuri. Naamini kuwa Shaaban Robert alituelekeza katika njia nzuri.

Joseph L. Mbele
1520 St. Olaf Avenue
Northfield MN 55057

Phone: 507 403 9756

http://www.josephmbele.blogspot.com
http://www.hapakwetu.blogspot.com

No comments: