Thursday, August 06, 2009

Mtangazaji wa BBC Anyofoa

Sikio la Rafiki Yake Aliyemfumania

na Mpenzi Wake




Laurence Westgaph.


Laurence Westgaph mwenye umri wa miaka 34 mtangazaji wa BBC aliyejipatia umaarufu kwa kuichambua historia ya Uingereza katika karne ya 19 aliingia matatani baada ya kumfumania kitandani rafiki yake kipenzi akifanya mapenzi na mama watoto wake.

Westgaph, ambaye huonekana kwenye vipindi vya televisheni na radio za BBC akichambua biashara ya utumwa, huenda akaenda jela miaka mitano akipatikana na hatia baada ya kukiri kumshushia kipigo cha nguvu rafiki yake.

Mkasa huo ulitokea pale Westgaph alipomtembelea mpenzi wake Natalie Inge, 26, ambaye alikuwa amezaa naye mtoto mmoja.

Westgaph alimfumania rafiki yake kipenzi Ben Blance, akiwa kitandani akifanya mapenzi na mama wa mtoto wake.

Westgaph alimrukia rafiki yake na kuanza kumshushia kipigo cha nguvu na katika harakati za kujinasua Blance aliweka vidole vyake karibu na mdomo wa Westgaph ambaye aliving'ata.

Blance alijeruhiwa jicho lake katika fumanio hilo na kipande cha sikio lake moja kilinyofolewa.

Awali ilisemakana kwamba Westgaph alimng'ata Blance sikio lake na kulinyofoa lakini mahakama iliambiwa kuwa kutokana na jeraha linavyoonekana ni wazi kuwa kipande cha sikio la Blance kilinyofoka baada ya Blance kuangukia sehemu yenye ncha kali.

Wakili wa Westgaph, David William, aliiambia mahakama ya Liverpool kuwa Westgaph alifanya shambulio hilo baada ya kuhuzunishwa sana na kitendo cha rafiki yake wa karibu kutembea na mpenzi wake.

"Blance alikuwa akionekana kama mmoja wa wanafamilia ya Westgaph, alikuwa akialikwa nyumbani kwa mama yake Westgaph wakati wa Krismasi na sherehe mbali mbali" alisema wakili wa Westgaph.

"Walikuwa ni marafiki wa karibu walioaminiana. Alisikitishwa kumuona rafiki yake akifanya mapenzi na Natalie huku mtoto wake akiwa amelala chumba cha jirani".

Mahakama iliambiwa kuwa Blance alikuwa akiamini kuwa Westgaph ameachana na mpenzi wake na hivyo ametaka aadhibiwe kwa kumshambulia.

Uchunguzi wa kesi hiyo unaendelea.

Chanzo: Magazeti ya Uingereza.

No comments: