Tuesday, August 04, 2009

Polisi Tanga kusaka

mashoga, makahaba



Mnara wa mji wa Tanga.


Na Sophia Wakati, Tanga

JESHI la Polisi mkoa wa Tanga linaendesha msako mkali dhidi ya mashoga wa kiume na wanawake wanaoendesha biashara haramu ya kuuza miili yao katika maeneo mbalimbali ya starehe ya jijini hapa.

Msako huo unaenda sambamba na kuwakamata wamiliki wa maeneo hayo ya starehe ikiwemo baa ambao wameamua kugeuza matumizi kulingana na leseni wanazomiliki. Vijana hao wanadaiwa kuweka maskani zao katika maeneo yenye baa kubwa ambazo baadhi ya wamiliki wameamua kuzifanya kama ‘Night Clubs’ badala ya baa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Simon Sirro, alibainisha hayo alipozungumza na gazeti hili na kukiri kuwepo kwa wimbi kubwa la watu hao. Alisema tayari askari wameanza msako tangu Agosti Mosi mwaka huu na kwamba wahusika watakaokamatwa watafikishwa mahakamani. Sirro alisema ongezeko la vijana hao wa kike na kiume wanaojiuza hapa Tanga limetokana na uamuzi wa wamiliki wengi wa maeneo ya starehe kubadili matumizi ya leseni zao za biashara na kuyafanya maeneo hayo kuwa klabu za usiku.

“Unajua wafanyabiashara wa baa na maeneo ya starehe wa hapa Tanga wameenda kuchukua leseni ya kumiliki baa, lakini baadaye wanaamua kugeuza matumizi na kudai biashara zao ni za klabu za usiku ili kuwadanganya watu kuhusiana na matendo machafu yanayoendelea kwenye eneo husika,” alisema kamanda huyo.

Alisema tayari polisi wamebaini kwamba jiji hilo halina mfanyabiashara aliyesajiliwa na Ofisa Biashara wa Halmashauri ya jiji la Tanga ili kuendesha Night Club. Kutokana na hali hiyo, amewataka wafanyabiashara wote ambao wanamiliki maeneo hayo kufuata na kuzingatia masharti ya leseni za biashara zao ikiwemo kufunga ifikapo saa 5.00 usiku kwa siku za kazi na saa 6.00 usiku kwa siku za mwisho wa wiki.

Kutoka gazeti la Uhuru

No comments: