Kuelekea uchaguzi mkuu
Norway 14.09.2009
Ikiwa imebaki wiki moja kabla ya uchaguzi mkuu hapa Norway (Jumatatu 14. Septemba 2009), hakuna mwelekeo wowote kuwa chama gani kitashinda na kuchukua usukani wa kuiongoza Norway kwa kipindi kijacho cha miaka minne.
Serikali ya sasa ya mseto ya vyama vya Labour Party (Arbeiderpartiet), Socialist Left (SV) na Agrarian Party (Senterpartiet) inayoongozwa na Waziri Mkuu Jens Stoltenberg (Arbeiderpartiet) inaweza kuendelea kuongoza tu endapo, vyama vyenye mwelekeo wa uhafidhina (conservatives) vitashindwa kuafikiana kuunda serikali ya mseto.
Mpaka sasa kwenye kura ya maoni, ngoma ni droo kati ya vyama vya mwelekeo wa kushoto na vile vyenye mwelekeo wa kulia. Kura za maoni zinayumba kila kukicha. Bado kuna asilimia kubwa ya wapiga kura ambao hawajaamua nani na chama gani cha kukipigia kura.
Vyama vyenye mwelekeo wa siasa za kihafidhina, The Conservative (Høyre/H), Liberal (Venstre/V) na Christian Peoples Party (Kristelig Folkeparti/KrF) vinaweza tu kuunda serikali ya mseto na kuendelea kuongoza kwa muda mrefu, kwa kutegemea kuungwa mkono na chama cha wahafidhina wenye siasa kali (Fremskrittspartiet/FrP).
H, V na KrF tayari wanamgombea wao wa nafasi ya Waziri mkuu, ambaye ni Bi. Erna Solberg wa H.
Jana Bungeni, kulitokea mtafaruku kidogo kati ya kiongozi na mgombea wa uwaziri mkuu H, Bi. Erna Solberg na kiongozi na mgombea wa uwaziri mkuu Bi. Siv Jensen wa FrP, pale Siv alipomwambia Erna mbele ya kamera za vyombo vya habari kuwa asahau ushirikiano na FrP na kuwa kuwa waziri mkuu, kama hawatawashirikisha FrP na kuwapa nafasi ya uwaziri mkuu.
FrP wameshasema kinagaubaga kuwa hawataunga mkono mseto huo, kama walivyofanya kuunga mkono serikali ya mseto ya Bw. Kjell Magne Bondevik (1997 - 2000/ 2001 - 2005), bila ya wao kushirishwa kikamilifu. Frp peke yao wanaweza kuwa na wingi wa kura kuliko vyama vyote hivyo vitatu (matagemeo yao kufuatilia uchaguzi wa 2005 na kura za maoni za hivi karibuni). Na FrP wanamgombea wao wa nafasi ya uwaziri mkuu, Bi. Siv Jensen.
Tayari hapa kumeshakuwa na mgongano!
Hata kama H, V na KrF wataunda mseto wenye pungufu wa wabunge, serikali yao haitadumu muda mrefu. Uwezekano wa kuangushwa na FrP ni mkubwa zaidi, kuliko hata wa kuangushwa na vyama vyenye siasa za mkondo wa kushoto.
Kwa upande wa vyama vyenye siasa zenye mwelekeo wa upande wa kushoto, Arbeiderpartiet (AP), Socialist Party (SV) na Senterpartiet (SP), bado wana nafasi ya kushinda na kuendelea kuongoza. Nafasi hiyo inatokana na hali shaghalabaghala ya vyama vya mkondo wa kulia ilivyo (angalia hapo juu)
AP, SV na SP wamekuwa wakitapatapa siku hizi za karibuni kwa kutoa mapendekezo ya kanuni na sheria ili kuwakuna mioyo wapiga kura. Nyingi za sheria walizopendekeza hivi karibuni, zilishapendekezwa kitambo na FrP.
Inapohusu sheria za wageni, mapato na kodi na misaada ya kwa nchi zinazoendelea, FrP wamekuwa wakichuma kwa wapiga kura. Wapiga kura wengi wamechoshwa na sheria zilizodi kikomo hapa Norway (Kwa wale wasiojua; hapa Norway kuna sheria karibu kila kona ya nyanja za maisha).
Wapiga kura wanataka nyufa kwenye sheria za wageni zizibwe, wanataka wageni walazimishwe kujua mila na desturi za Wanorweji, atakayeshindwa arudi alikotoka. Wanataka wanaokuja kuomba ukimbizi, washughulikiwe haraka sana na watakaokataliwa waondoshwe bila huruma. Wanataka kodi zisizo za lazima ziondolewe kupunguza makali ya maisha kwa walalahoi.
Mfano huu mdogo ndio unaowafanya wapiga kura waliochoshwa na ahadi za kila siku za wanasiasa wa kawaida, kuwapigia kura FrP.
AP ambacho bado ni chama kikubwa hapa Norway, kinagwaya kuhofia kupoteza kura na madaraka. Lakini hata kama vyama vyenye mwelekeo za siasa za upande wa kushoto vitashindwa kunyakua wingi wa kura, kinaweza kuitwa na Mfalme kuunda serikali pungufu.
Serikali hiyo pungufu itakuwa inategemea sana kuendesha shughuli zake za kila siku kwa kuungwa mkono toka pande zote ili iweze kuongoza kwa muda mrefu. Kitu ambacho kinawezekana, lakini maisha ya serikali hii yatakuwa mafupi. Serikali ya kwanza ya Jens Stoltenberg (AP) ilikuwa pungufu na aliweza kuongoza kwa mwaka mmoja (2000 – 2001).
FrP wanaweza kuitwa na Mfalme kuunda serikali yao pungufu, ikiwa AP, SV na SP watashindwa kupata wingi wa kura kuendelea kuongoza kimseto, Jens Stoltenberg anaweza kukataa kuunda serikali pungufu ya mseto ya AP, SV na SP na pia kukataa kuunda serikali pungufu ya AP pekee yake.na H, V na KrF kushindwa kuuafikiana na FrP kuunda mseto.
Imeandikwa na mhariri wa blogu
2 comments:
EEEH BWANA EEEH MCHANGANUO WAKKOWA WA HALI YA KISIASA KABLA YA UCHAGUZI POA!!!
Usikose kutuandikia tathmini baada ya uchaguzi.
Post a Comment