Sunday, January 10, 2010

Aftenposten lachapisha vikatuni
vya Mtume Muhammad (S.A.W)


Gazeti la kila siku la Aftenposten limechapisha vikatuni vya Mtume Muhammad (S.A.W) kwenye toleo lake la asubuhi la juzi Ijumaa. Aftenposten wamechapisha vikatuni hivyo vilivyochorwa kwa mara ya kwanza na msanii Mdenish Kurt Westgaard na kuchapishwa kwenye gazeti la Jyllandposten la Denmark miaka minne iliyopita. Mhariri mkuu wa Aftenposten, Bi. Hilde Haugdsgjerd ametetea uamuzi wa gazeti lake kuchapisha vikatuni hivyo kwa kusema; vyombo vya habari vya Kinorwejiani vina uhuru wa kuchapisha lolote, hivyo basi haoni kuwa hivyo vikatuni vinamkashifu Mtume.

Uamuzi wa Aftenposten wa kuchapisha vikatuni hivyo, umeungwa mkono na baadhi wa Waislamu wenye itikadi za kati za kidini walioko Norway na hakukuwa na gumzo kubwa kuhusu hivyo vikatuni.

Hivi majuzi, mchoraji wa vikatuni hiyo, Kurt Westgaard alishambuliwa nyumbani kwake na kijana mmoja wa Mdenish mwenye asili ya Kisomali na nusura auawe. Kijana huyo aliingia ndani kwa kuvunja kioo cha mlango na Westgaard aliposikia mlango unavunjwa akajua nini kitatokea basi akakimbilia chooni kulikotengezwa kama ngome ya kujikinga. Westgaard akabonyeza ishara na polisi wakatokea baada muda mfupi uliofuatia. Kijana huyo aliwatishia polisi wakampiga risasi na kumjeruhi. Kijana huyo tayari ameshafunguliwa mashtaka ya kutaka kuua.

Imethibitishwa na idara ya usalama ya Denmark PET (Politiets  Efterretningstjeneste) kuwa, kijana huyo alikamatwa Agosti mwaka jana mjini Nairobi kwa kuhusishwa na kupanga kumwua waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Bi. Hallary Clinton alipokuwa ziarani nchini humo. Kijana huyo alikamatwa na vyombo vya usalama vya Kenya na aliachiliwa kwa sababu vyombo vya usalama havikuwa na ushahidi wa kutosha, hivyo akarudishwa Denmark.

Vikatuni hivyo viliyochapishwa na gazeti la Jyllanposten miaka minne iliyopita, vilizua mtafuruku mkubwa kwenye nchi za Kiislamu na kwa Waislamu waliona kuwa Mtume na Uislamu umekashifiliwa. Westgaard aliwekewa dau la kichwa chake na Waislamu waliokasirishwa na vikatuni hiyo, na toka wakati huo amekuwa akilindwa.

No comments: