Sunday, June 20, 2010

Tanzania - Kikwete atangaza mikoa, wilaya mpya



RAIS Jakaya Kikwete ametangaza mikoa mitatu , wilaya, tarafa na halmashauri za wilaya mpya ili kuimarisha utawala bora.

Kwa sasa Tanzania bara ina mikoa 26 hivyo kwa tangazo hilo la kusudio la kuanzisha mikoa mipya mitatu itafikia 29.

Hata hivyo, Pinda alidokeza kuwa mazungumzo bado yanaendelea kuhusu uanzishwaji wa mkoa wa Mpanda na mkoa wa Arusha kupewa hadhi ya kuwa Jiji.

Wakati hayo yakiwa yanaelezwa taarifa zinaonyesha kuwa gharama ya kuanzisha mkoa mpya ni kati ya Sh4 mpaka 6 bilioni na kwa wilaya mpya ni Sh1 bilioni.

Gharama hizo zinajumuisha ujenzi wa makao makuu, kulipia gharama za uendeshaji, kuweka miundombinu muhimu pamoja na kuajiri watumishi.

Kusudio la kuanzishwa kwa mgao huo mpya ulitangazwa bungeni mjini Dodoma jana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokuwa akihitimisha hotuba ya Makadirio ya Bajeti kwa Ofisi yake ambayo ni Sh2.6trilioni. Bajeti hiyo ilipitishwa jana jioni.

Kwa mujibu wa Pinda mikoa mipya itakuwa ni mkoa wa Njoluma, Simiu na Geita ambapo mkoa wa Njoluma utajumuisha maeneo ya Njombe, Ludewa na Makete.

Mkoa wa Simiu unagawanywa kutoka mkoa wa Shinyanga na Geita.

Kwa mujibu wa Pinda baadhi ya wilaya zinazokusudiwa kuanzishwa ni Butiama mkoani Mara, Mbogwe mkoani Rukwa, Nyang'wale, Ilemela na Ushetu mkoani Mwanza.

Nyingine ni Kwela na Bulele mkoani Rukwa, Kaliua, Ikungi mkoani Singida, Kalambo, Ushelu, Gairo mkoani Morogoro, Mkalama, Nyasa mkoani Ruvuma na Uvinza mkoani Kigoma.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, serikali pia inakusudia kuanzisha halmashauri za wilaya mpya ambazo ni Kaliua, Uvinza, Kakong'o, Kalambo na Mkalama.

Nyingine ni Nyasa, Nyang'wale, Kahama, Masasi na Lindi.

Hata hivyo, akitoa maelezo wakati wa kujadili vifungu vya bajeti ya Waziri Mkuu kabla ya kupitishwa, Waziri wa Nchi (Tamisemi)

Celina Kombani alisema mikoa na wilaya hizo hazikutengewa bajeti kwa mwaka 2010/2011 kwa kuwa mchakato wa kugawa mipaka yake bado unaendelea.

Alisema hatua ya kuanza kazi kwa mikoa na wilaya hizo zitapelekwa kwa rais ambapo pia wananchi watashirikishwa kabla ya kutolewa kwa notisi kwenye gazeti la serikali.

1 comment:

Anonymous said...

Kama Mikoa iliyopo haijaweza kufanya kazi na kuimarisha maisha ya Watanzania, hiyo mikoa mipya ita fanya maajabu gani kuhusu hilo? Naamini nia hasa ni kuwapa watu wa serikalin na wana CCM Kazi!! hilo tu na sio jingine...