Thursday, July 01, 2010

Uzee



Uzee kitu adhimu, huo ninauingia
Ujana sasa adimu, Shabani aliusia
Maungoni mwangu humu, uzee unanijia,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Mbali ninamuachia, rafiki yangu ujana,
Miaka inakimbia, ya leo siyo ya jana,
Nabaki nakumbukia, nilipokuwa kijana
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Shabani aliandika, kaulilia ujana,
Ni vipi unamtoka, kashindwa kuung’ang’ana,
Meno yalimdondoka, na nguvu tena hamna,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Taratibu waingia, uzee wabisha hodi,
Siwezi kuukimbia, hata niwe mkaidi
Hata nikitukania, ndivyo napigwa baridi,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee

Mvi sasa zanijia, nimejaribu kung’oa
Kidevu zasalimia, na miye nazichomoa,
Nikitoa zazidia, nami nazidi kutoa!
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Mapensi nayaachia, na macheni ya shingoni,
Hereni nilivalia, kwenye sikio jamani,
Mwendo nilibadilia, nilivyonesa njiani,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Niliwapata mademu, tena wengine kwa zamu,
Nikaitwa mtaalamu, wa mambo yale matamu
Sasa yanitoka hamu, nanyimwa hata salamu!
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Nilenda nilipotaka, wasiponitaka nilenda,
Sikuwa na hata shaka, ati mtu kunidunda,
Leo naogopa paka, ninavutwa kama punda,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Mwendo wa kudemadema, nikishika natetema,
Uso umenikunjama, natembea nikihema,
Magoti nayo yauma, uzee si lele mama!
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Kumbe maisha ni hivi, uzee haukwepeki,
Ninazikubali mvi, hata kama sizitaki,
Uzee siyo ugomvi, ujana haushikiki,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Kweli nilifurahia, enzi zile za ujana,
Kamwe sintoyarudia, yalopita naagana,
Uzee nakumbatia, kwani lingine hakuna,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Nasubiri wajukuu, nione na vitukuu,
Nakunja miguu juu, na mshukuru Mkuu
Kuona umri huu, enzi hizi ni nafuu,
Na miye nakusalimu, mgeni wangu uzee!

Na. M. M. Mwanakijiji
(Sauti ya Kijiji a.k.a Vuvuzela Matata)

No comments: