Sunday, February 25, 2007

Tumekuwa watumwa wa lugha na tamaduni za kigeni

Mwandishi Wetu

UTAMADUNI ndicho chombo muhimu cha utambulisho wa jamii yoyote ile. Utamaduni huundwa na vipengele mbalimbali kama vile mila, desturi, sanaa na lugha. Mfano, Afrika, tuna tamaduni zetu, Ulaya wana tamaduni zao na vile vile Uarabuni wana tamaduni zao. Hii aishii hapa, bali tukienda kwa ndani zaidi tutaona Afrika Mashariki tuna utamaduni wetu, Kenya wana tamaduni zao, Uganda wana tamaduni zao na Tanzania tuna tamaduni zetu.

Hata hivyo, si kusema kwamba hizi tamaduni haziwezi kufanana, kwani utamaduni ni kitu chote kinachofanyika na binadamu katika maisha ya kila siku. Kwa maana hiyo, utamaduni si tenge, bali uweza kubadilika kutokana na mazingira au kuiga kutoka sehemu nyingine.

Baadhi ya vitu vikuu ambavyo utamaduni uweza kutooa ni kama mila, desturi, sanaa na wakati mwingine lugha na hii ndiyo maana tunaona mabadiliko makubwa katika maisha yetu ya kila siku na wakati mwingine mabadiliko haya, yanatokana na kuongezeka kwa sayansi na teknolojia na mabadiliko katika maisha kadiri tunavyohama toka kizazi kimoja hadi kingine.

Msukumo wa kuandika makala haya si kwa sababu napingana na mabadiliko katika nyanja mbaliambali za utamaduni. Nasema hivyo kwa sababu nimekerwa sana na tabia za sasa hivi, ambazo zimechukua ukurasa mpya wakati tunapoona watu wanajaribu kuiga mila na desturi za kigeni ambazo najaribu kutafuta umuhimu wake katika jamii zetu, lakini siuoni tofauti na kuzidi kudidimiza Utanzania wetu na uasili wa ubora tulionao.

Ijulikene kuwa lugha katika desturi, ndiyo kitambulisho kikuu cha jamii yoyote ile. Mfano mtu yeyote ataitwa Mtanzania katika sehemu yoyote ile atakapoenda. Pale, ataonekana akizungumza Kiswahili fasaha, na vivyo hivyo utamtambua mtu fulani kuwa ametoka Uganda pale tu atakapoonekana akizungumza lugha ya Kiganda na utaweza kumtambua Mchina kama anazungumza Kichina.

Hii simaanishi kuwa ni lazima Mganda asizungumze Kiswahihi au Mtanzania asizungumze Kireno, bali namaanisha ni nani anayeweza kutambulika kama mwanajamii fulani na ni nani hawezi kutambulika kutokana na kutumia kigezo cha lugha. Nimekuwa nikitafakari matumizi ya lugha ya Kiswahili kama lugha ya taifa katika sehemu mbalimbali zikiwemo za makongamano makubwa, matamasha, mashuleni, na katika baadhi ya vipindi vya redio na luninga na sehemu nyingine ambazo nilitegemea lugha hii kupewa mkazo kama lugha ya taifa.

Nimegundua kuwa, kuna udhaifu mkubwa wa Watanzania kuamini lugha ya Kingereza na kuipa heshima kubwa. Japokuwa ni lugha ya kimataifa, sina maana kuwa tusiitumie kwani ndiyo lugha kuu ya kutuunganisha duniani, lakini tuthamini lugha yetu. Matumizi ya lugha hii yanaonekana kuabudiwa sana na kusahau utambulisho wetu, mifano hii nitakayoieleza hapa chini, itakuwa ya kuthibitisha ukweli wa mambo ninayotaka kuyajadili.

Mfano wa kwanza ni yaliyotokea mwaka jana wakati wa kutafuta mlimbwende wa Tanzania (Miss Tanzania 2006). Ijulikane kwamba alikuwa anatafutwa mrembo wa Tanzania. Tuliamini maonyesho yalionyeshwa kwenye luninga zetu kwa madhumuni makubwa, hasa ya kuwafahamisha na kuwaonyesha Watanzania nini kilichokuwa kinaendelea.
Na kwa watu hawa, asilimia kubwa Kiswahili ndiyo mkombozi na ndiyo lugha ya taifa. Tulitegemea lugha ya Kiswahili ingetumika, lakini jambo la kushangaza, warembo walishindana kwa kutumia lugha ya Kingereza na mrembo aliyeweza kuzungumza Kingereza vizuri, ndiye aliyeonekana anafaa.

Lugha ya Kiingereza ilionekana kigezo cha mrembo kuchaguliwa na wengine waliokuwepo kuonekana hawafai zaidi kwani hawakuweza kuzungumza Kiingereza vizuri. Hata tukiangalia wasimamizi au majaji wa mashindano hayo, walikuwa wakitumia sana lugha ya wenzetu na hii si kwamba watu hawa hawakuweza kutumia lugha ya Kiswahili, bali ni ile dhana iliyojengeka ya kusali ibada za wenzetu.

Mfano mwingine tuangalie kuwepo kwa muziki wa Kizungu ambao Watanzania walio wengi, hawajui hata maana yake, lakini la kushangaza vijana wengi wamekuwa watumwa kuamini muziki wa Kizungu ni mzuri zaidi kuliko wa nchini (Bongo flever), sababu hawatumii lugha za kigeni.

Nimeshuhudia watu wengine wakijaribu kuigiza hata sauti za wanamuziki wa Kizungu. Wanakariri sauti baadala ya maneno hata kama hawajui maana yake kwa sababu ni lugha ya Kingereza inatumika. Wakati nikiangalia kipindi katika luninga (EAST AFRICAN TV) cha “BONGO STAR SEARCH” kuchagua mwimbaji bora Tanzania, waimbaji wangeweza kushindana kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

Watanzania leo imefika mahala, wanaamini kuwa kipimo cha ustarabu ni kuzungumza Kingereza. Wapo wanaoamini kuwa lugha hii inawafanya kuwa tabaka la juu. Ndio maana watu wengi wakilewa huweza kutamba kwa kutumia lugha ya Kiingereza. Nasisitiza kuwa si nia yangu kwamba lugha hii isitumike, lakini isiwe kipimo cha maendeleo ya mtu.

Hivi karibuni, tumefanya sherehe za maadhimisho ya miaka 45 ya uhuru. Hii inamaanisha kuwa tangu tuanze kujikomboa kutoka kwenye meno ya wakoloni katika nyanja zote za kisiasa kiuchumi na kiutamaduni, tunapaswa kujibunia utamaduni wetu. Kamwe tusikubali kutawaliwa kimawazo wakati tuko huru. Vinginevyo sherehe hizi tunazofanya kila mwaka hazina maana kama tunazidi kutukuza zaidi mila na desturi za kigeni. Tubadili mwelekeo wetu. Thamani ya kiswahili ianze kuonekana toka shule za msingi. Leo hii wazazi wanapeleka watoto wao Kenya na Uganda kwa ajili ya kujifunza Kiingereza.

Utumwa si lazima kulazimishwa kwa nguvu au kufungwa na kupigwa mijeledi kama walivyokuwa wakifanyiwa babu zetu bali mtu unaweza kutawaliwa kwa njia nyingine kama ya kupenda lugha na tamaduni za Kizungu na kudharau mila na tamaduni zetu.

Mwandishi wa makala hii, ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaa (UDSM), anayepatikana kwa simu: 0713 894129.

Source: http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/2/24/makala4.php

No comments: