Thursday, February 22, 2007

Wanafunzi wa Tanzania Ukraine kujisalimisha Uingereza



Na Mwandishi Wetu

WANAFUNZI 29 wa Kitanzania wanaosoma katika vyuo vikuu nchini Ukraine, wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha na sasa wanapanga kwenda katika ubalozi wa Uingereza nchini
humo kuomba misaada ya kibinadamu, ikiwemo chakula na mahali pa kujihifadhi.

Wanafunzi hao wamekumbwa na hali hiyo ngumu ya maisha baada ya kufukuzwa katika vyuo walivyokuwa wakisoma baada ya kushindwa kulipa ada kwa muda mrefu, huku pia wakikosa fedha za kujikimu kwa ajili ya chakula na mahitaji mengine muhimu.
Wakizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu kutoka Ukraine, jana, wanafunzi hao walisema wamefikia hatua hiyo baada ya kuona serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi, haijawatumia fedha za ada na za kujikimu tangu Septemba, mwaka jana.
Walilalamika kuwa serikali imewatelekeza kiasi cha kuwafanya waishi kama wakimbizi katika nchi hiyo ya ughaibuni, huku wengine bila ya kupenda wakijiingiza katika vitendo vichafu ili waweze kukabiliana na hali ngumu ya maisha inayowakabili.

“Tunaishi maisha magumu sana, hatujui tutakula wapi wala kulala wapi, tumefukuzwa vyuoni na kwenye hosteli sasa tunaishi maisha ya kutangatanga na wengine wamejiingiza katika vitendo vichafu bila ya kupenda ili waweze kuishi,” alisema mmoja wa wanafunzi hao ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini na kuongeza;

“Hali sasa imekuwa mbaya sana tumekata tamaa kwa hiyo ili kuokoa maisha yetu tumeamua tukajisalimishe katika ubalozi wa Uingereza ili tuombe kupatiwa misaada ya kibinadamu kama vile chakula, malazi na mahitaji mengine muhimu ya kibinadamu.”
Wanafunzi hao walilalamika kuwa wamekuwa wakifanya juhudi kubwa na za mara kwa mara kuwasiliana na Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Bodi ya Mikopo kueleza tatizo lao, lakini vyombo hivyo vya serikali vimekuwa vikiwajibu kuwa haviwatambui.

Wanafunzi walieleza kuwa walienda nchini Ukraine Septemba mwaka jana kwa ajili ya masomo baada ya kukubaliwa kupewa mikopo na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kuanzia muhula wa masomo wa 2005/06.

Hata hivyo walisema kutoka na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wao, walishindwa kwenda Ukraine kwa ajili kuanza masomo katika muhula huo na badala yake waliondoka mwaka jana kwa ajili ya kuanza masomo muhula wa 2006/07.
Walisema baada ya kushindwa kuanza masomo muhula huo, walikubaliana na Bodi ya Mikopo pamoja na Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kuwa mikopo yao ihifadhiwe kwa ajili ya muhula wa 2006/07.

Walidai kuwa waliondoka nchini kwenda Ukraine baada ya kuhakikishiwa na Wizara ya Elimu ya Juu, Syansi na Teknolojia kuwa mikopo yao itahifadhiwa hadi muhula wa 2006/07, lakini sasa wanashangaa kuona pamoja na makubaliano hayo, wizara hiyo pamoja na bodi ya mikopo inawaruka kuwa haiwatambui.

“Tunaomba serikali itusaidie, tunaishi katika mateso makubwa huku ugenini, hatujui tutakula wala kulala wapi, hatuna msaada, hapa hakuna ubalozi wa Tanzania tunategemea ubalozi uliopo Urusi ambako ni mbali,” alisema mmoja wa wanafunzi hao.
Mwananchi ilipowasiliana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Dk Naomi Katunzi, ili kujua undani wa malalamiko ya wanafunzi hao, alisisitiza kuwa wizara yake haiwatambua wanafunzi hao.

Alifafanua kuwa wanafunzi hao walipatiwa mikopo kwa ajili ya muhula wa masomo wa 2005/06 lakini walishindwa kuondoka nchini katika kipindi hicho na badala yake waliondoka muhula wa 2006/2007 wakati masharti ya uombaji mikopo yakiwa yamebadilika.
Alisema kabla ya kuondoka nchini wanafunzi hao walielezwa masharti ya mkopo yamebadika hivyo hawataweza kupata mikopo hiyo kwa muhula wa 2006/07.

“Walikuwa kama wanfunzi 40 hivi, tuliwaambia masharti ya mikopo yanabadilika kila mwaka kwa hivyo wasiondoke kwenda Ukraine na badala yake tukawashauri waombe mikopo ili wasome hapa nchini, baadhi walitusikiliza lakini sasa nashangaa kusikia hao 29 wapo Ukraine na wanadai mikopo,” alisema Dk Katunzi.

Alisema kwa mujibu wa masharti mapya ya mikopo kwa wanafunzi yaliyoanza kutekelezwa mwaka jana kabla ya wanafunzi hao kuondoka, wanafunzi wanaostahili kupewa mikopo kwa wale wanaotaka kwenda kusoma nje ya nchi ni wale tu wanaokwenda katika nchi zenye makubaliano maalumu na serikali ya Tanzania na kwamba Ukraine si moja ya nchi hizo.
Alipoulizwa na Mwananchi hivi karibuni kuhusiana na suala la wanafunzi hao, Mkurugenzi Msaidizi wa Mawasiliano katika Bodi ya Mikopo, Cosma Mwaisombwa, alikiri kuwa wanafunzi hao 29 walikubaliwa kupatiwa mikopo kwa ajili ya muhula wa masomo wa 2005/06 na si muhula wa 2006/07.

Alisema kabla ya kuondoka nchini, wanafunzi hao walielezwa kuwa kwakuwa wameshindwa kuanza masomo muhula huo wa 2005/06, bodi haitakuwa tayari kutoa mikopo hiyo kwa muhula wa 2006/07 kutokana na kubadilika kwa vigezo vya uombaji wa mikopo kwa wanafunzi wanaotaka kwenda kusoma nje.

Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/mwananchisite/Mwananchi/Habari/Habari2.asp 22.02.2007

No comments: