MABADILIKO makubwa yamefanywa na Serikali katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu. Kwa mujibu wa mabadiliko hayo yatakayoanza kutekelezwa muhula ujao wa masomo, wanafunzi katika vyuo hivyo watakuwa wanapata mikopo kwa kuzingatia kipato cha wazazi na walezi wao.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolla, alipotembelea Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu Dar es Salaam (DUCE) jana.
Kutokana na mfumo huo mpya, wapo wanafunzi watakaopewa mkopo kwa asilimia 100 wakati wengine wataondolewa katika kundi la kupewa mkopo. Awali, wanafunzi walikuwa wanapewa mkopo wa asilimia 60 na kuchangia asilimia 40 bila kuangalia uwezo wa wazazi au walezi.
Profesa Msolla alisema kabla wanafunzi hawajaenda likizo kubwa Juni mwaka huu, watapewa fomu za kwenda kujaza ambazo zitasaidia kujua uwezo wa kila mzazi au mlezi na kumpangia kiwango cha kuchangia katika ada.
“Hili suala la wanafunzi kuchangia asilimia 40 linakwisha muhula huu na badala yake kila mwanafunzi atatakiwa kujaziwa fomu na kiongozi wake wa kijiji pamoja na viongozi wa dini yake, tuweze kujua kila hali ya maisha ya mwanafunzi.
“Tutaanza kupanga asilimia kwa kuzingatia hali ya maisha ya mwanafunzi husika ambayo yatakuwa yamebainishwa na viongozi wa dini tukiwa na imani kuwa viongozi hawa hawatadanganya. Hapo tutaangalia wa kuwalipia asilimia 100, wengine 20, wengine 60 na wengine hatutawalipia kufuatana na kipato cha wazazi.
“Mzazi ana ng’ombe zaidi ya 20, ng’ombe mmoja akiuzwa ni zaidi ya Sh 300,000 wakati ada ni Sh 600,000 halafu mzazi huyu huyu anasema hana uwezo ni mambo ya ajabu. Safari hii tutakuwa makini katika hilo, ili watu wote wapate elimu,” alisisitiza.
Waziri pia aliwataka wahadhiri wa DUCE kuwahamasisha wanafunzi kuchukua masomo ya hesabu na sayansi ili kuendana na mabadiliko ya dunia.
“Mkumbuke kuwa hii ni dunia ya sayansi na teknolojia na wakati huo huo, hivi sasa tumejiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, sasa tusipokuwa makini wageni watakuja kufanya kazi hizo hapa kwetu na sisi tutakuwa watumwa wao,” alisema.
Profesa Msolla alisema kuwa wataweza kufanikiwa kupata wanafunzi wengi iwapo wataajiri walimu wazuri na waliobobea katika masomo kwani watakuwa na njia mbadala za kufanya wanafunzi wapende masomo hayo kama walivyoyapenda wao.
Alisema wakati wa kusaili wanafunzi wazingatie wanafunzi waliofaulu vizuri katika masomo hayo na wawachague kuliko kuchagua ili mradi tu katuma maombi hata kama hana sifa.
Profesa Msolla vilevile alizungumzia suala la mrundikano wa wanafunzi katika madarasa na kuwataka waandae ratiba maalumu ya kuwafundisha kwa makundi ya wanafunzi wachache kusaidia kutoa wanafunzi bora.
Naye Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Henry Mosha aliomba ada za wanafunzi ziwe zinaingizwa katika akaunti ya chuo kabla ya wanafunzi kuripoti chuoni kuepusha migogoro wakati wa kulipa.
Source: HabariLeo; Saturday, March 24, 2007 @00:07
No comments:
Post a Comment