Saturday, March 24, 2007

Kikwete awacharukia Wasomali majambazi



*Asema operesheni maalumu imeandaliwa kuwang'oa
*Aonya wananchi wanaoshiriki nao kufanya uhalifu

Na Said Njuki, Arusha

RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali itatumia nguvu zote kulinda usalama wa wananchi na mali zao unaotishiwa na ujambazi unaoonekana kuwa na viota katika baadhi ya maeneo nchini.

Amesema jambo hilo linachukuliwa kwa uzito unaostahili na kwamba Serikali itatumia nguvu zote kuwatoa, kwani imeandaa operesheni kubwa ingawa kunaweza kuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu, lakini hakuna mtu atakayeonewa.

Rais alisema hayo jana wakati akijumuisha ziara yake mkoani hapa wakati akizungumzia usalama wa raia na mali zao, kuhusiana na matukio kadhaa ya ujambazi unaodaiwa kufanywa na wanaodaiwa kuwa raia wa kisomali na taarifa alizopata kutoka Arumeru, Ngorongoro na Longido, kuhusu wageni hao.

“Lipo tatizo kubwa la usalama, si kwamba watu hawalali…tatizo la Wasomali ni sura moja ya tatizo hilo, ni wahamiaji haramu wameingia nchini kinyume na taratibu, tena wanafanya vitendo vya uhalifu…tutaongeza nguvu ya operesheni ili Watanzania katika nchi yao waishi kwa usalama na mali zao,” alisema.

Hata hivyo alisema Watanzania wana mchango wao katika tatizo la Wasomali, kwani wanashirikiana nao kuwahifadhi na kufanya vitendo vya uhalifu.

Aliwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya Dola kwa kufichua wahalifu hao ili kuwatoa na kuwasukumiza magerezani kutumikia adhabu zao kwa mujibu wa sheria.

Hivi karibuni kulitokea matukio ya ujambazi yaliyodaiwa kufanywa na wavamizi wa kisomali kutoka nje ya nchi, ambapo watu kadhaa walipoteza maisha na mali za thamani ya mamilioni ya fedha kuporwa.

Source: http://www.majira.co.tz/kurasa.php?soma=tanzania&habariNamba=2674


No comments: