Sunday, September 16, 2007

Gazeti la Ijumaa lachemsha! ....laomba radhi

Ndugu wasomaji,

Naomba nichukue nafasi hii, kwa niaba ya kampuni, nikiwa Mkurugenzi wa kampuni ya Global Publishers Ltd, wachapishaji wa magazeti pendwa ya Uwazi, Ijumaa, Ijumaa Wikienda, Championi, Risasi, Amani na The Bongo Sun. Pia kwa niaba ya wafanyakazi wa kampuni hii, nachukua fursa kuwaomba radhi ninyi wasomaji kwa kilichotokea katika habari na picha zilizochapishwa kwenye gazeti la Ijumaa la tarehe 14, Septemba, 2007, chini ya kichwa cha habari WABAMBWA!


Asubuhi na mapema siku ya Ijumaa baada ya gazeti hilo kutoka, nilianza kupokea simu kutoka kwa wasomaji wengi wanaotutakia mema wakidai habari hiyo ilikuwa ni ya kweli lakini haikutokea nchini Tanzania kama tulivyoandika, bali nchi jirani na kwamba ziko kwenye mtandao. Simu hizo zilinishtua sana, nikalazimika kulitafuta gazeti hilo ili nisome na kuona kama taarifa nilizopewa zina ukweli wowote.

Baada ya kuziona picha hizo na kuisoma habari husika, nilichofanya ni kumuita mhariri wa gazeti hilo na kutaka atoe maelezo juu ya malalamiko yaliyotolewa na wasomaji wetu. Katika maelezo yake, mhariri alidai habari hiyo ililetwa na chanzo cha habari ambacho siku zote tumekuwa tukifanyanacho kazi na kukiamini. Kwa mujibu wa chanzo hicho, tukio hilo lilitokea maeneo ya Mabibo jijini Dar es Salaam na kikafanikiwa kupiga picha hizo na kuzileta ofisini kwetu na kudai malipo ya shilingi 200,000 (laki mbili) zilizotakiwa kulipwa siku ya Ijumaa baada ya gazeti kutoka.

Kufuatia utata huo, niliagiza chanzo hicho kuhojiwa kwa mara nyingine kama kweli picha hizo zilipigwa Mabibo na yeye ama la, jambo hilo lilifanyika na awali katika maelezo yake, chanzo kilisisitiza kuwa picha hizo alizipiga yeye katika eneo hilo, lakini baadaye alipobanwa kwa maswali mengi ikiwa ni pamoja na kuonyeshwa picha kama hizo zilizotumwa kwetu kwa njia ya mtandao na msomaji aitwaye Anna, alikiri kudanganya kwa lengo la kujipatia fedha!

Kwa kweli, jambo hili, mimi binafsi pamoja na wenzangu katika Global, limetuumiza sana, kwani kwa muda mrefu yamekuwepo madai kwamba habari tunazoandika siyo za kweli, lakini mara nyingi tumefanikiwa kuwathibishia wasomaji wetu kuwa hatuandiki uongo. Ndani ya miaka kumi tunayokaribia kuimaliza, hata siku moja hatujawahi kupata tatizo la aina hii! Hii ni mara ya kwanza, tunakiri kosa hili na tumeshaelewa tatizo letu, tunaahidi kuwa makini zaidi siku nyingine ili tusiudanganye tena umma wa wasomaji wetu wanaotuheshimu na kununua magazeti yetu kila siku.

Zipo hisia kwamba, chanzo hiki kilikuwa kimetumwa na maadui zetu kwa lengo la kutushushia heshima. Jambo hili bado tunalifanyia kazi, lakini tunachokifahamu ni kwamba mwisho wa vita vilivyopo tutashinda tu kama ninyi mtaendelea kusimama na sisi na kutukosoa pale tunapokwenda vibaya. Kumbukeni “to grow economically you need friends, but to develop economically you need enemies, so enemies are important for us to develop.”

Hatua makini zimechukuliwa kwa chanzo hiki, kisingeweza kuachwa kiondoke huru baada ya kuwa kimetuumiza kiasi hiki. Kinachoendelea wakati tunaandika waraka huu, ni kwamba Bw. Anos Magongo Rugahimkamu (pichani chini)yuko Kituo cha Polisi Msimbazi, alikamatwa siku hiyo hiyo ya Ijumaa na kufikishwa kituoni ambako alifunguliwa kesi namba MS/RB/10757/07 ya kujaribu kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu. Anategemea kufikishwa mahakamani Jumatatu.

izi ndizo hatua tulizozichukua, pamoja na yote hayo, hakuna jambo lolote ambalo muungwana anaweza kusema baada ya kukosea zaidi ya kuomba msamaha! Kwa niaba ya wenzangu, tunaomba mtusamehe na tunaahidi kuwa makini sana siku nyingine. Ni matumaini yetu mtakubali kufanya hivyo. Kumbukeni hili ni kosa letu la kwanza na sisi ni ndugu zenu, tumetoka nanyi mbali miaka kumi iliyopita, TUPENI NAFASI NYINGINE.

Mungu awabariki sana.
Ahsanteni
Eric Shigongo James

NB: Hatua makini pia zimechukuliwa dhidi ya Mhariri.

No comments: