Imetolewa mara ya mwisho: 03.09.2007 1023 EAT
Na Mwandishi Wetu
USHINDI wa mnyange mwenye asili ya Kihindi, Richa Adhia aliyetwaa taji la Miss Tanzania 2007 na kurithi mikoba ya Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu, umepingwa na wadau mbalimbali wa fani ya ulimbwende nchini.
Richa anayeshikilia taji la Miss Kinondoni 2007, aliibuka kidedea katika shindano lililofanyika Dar es Salaam juzi usiku, akiwapiga kumbo wanyange wenzake 25 waliopanda jukwaani kuwania taji hilo.
Hata hivyo, baada ya Richa kutangazwa mshindi, mashabiki wengi waliinuka vitini kwa hasira wakiguna kupinga ushindi wake huku Miss Tanzania 1999, Hoyce Temu akiporomosha kilio kutokana na kuwa na uchungu zaidi akipinga ushindi wa mrembo huyo.
Hoyce Temu akiporomosha kilio kutokana na kuwa na uchungu zaidi akipinga ushindi wa mrembo huyo. Picha kutoka gazeti "Ijumaa"
____________________________
Wadau wengi wa fani ya urembo walisikika wakipiga kelele na kulalamika kwamba 'Mhindi' huyo hastahili kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss World 2007 yanayotarajiwa kufanyika Sanya, China Desemba Mosi mwaka huu.____________________________
Mkurugenzi wa Kamati ya Miss Tanzania, Hashimu Lundenga alipoulizwa kuhusu ushindi wa mrembo huyo kupingwa na wadau wengi wa fani ya ulimbwende, alisema ni uamuzi wa majaji na anaona wako sahihi. Jaji Mkuu alikuwa Miss World 2001, Agbani Darego kutoka Nigeria aliyemtangaza mshindi.
Katika kinyang'anyiro hicho, Lilian Abel pia kutoka Kinondoni akishika nafasi ya pili na kuambulia sh. milioni 5.5 na Queen David ambaye ni Miss Temeke 2007 aliambulia nafasi ya tatu na kuzawadiwa sh. milioni 3.5.
Wengine walioingia tano bora ni Hadija Sula kutoka Kanda ya Ziwa na Victoria Martin kutoka Kanda ya Kaskazini aliyetwaa taji la Balozi wa Redd's lililokuwa likishikiliwa na Jokate Mwegelo. Kila mmoja alipata sh. milioni 2.5.
Wanyange wengine waliotinga kumi bora ni Gladness Katega, Marietha Richard, Cecilia Charles, Latifa Warioba na Neema Khatibu ambao kila mmoja alipata sh. milioni 1.2. Ambao hawakufika hatua hiyo kila mmoja alipata kufuta jasho cha sh. 600,000.
Kwa kutwaa taji hilo, Richa alizawadiwa kitita cha sh. milioni 8 na gari aina ya Toyota RAV 4. Pia mnyange, Helga Tarimo kutoka Kanda ya Ziwa alitwaa taji la Miss Popularity.
Mashindano hayo yalianza kwa burudani iliyopambwa na wanenguaji wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta Original' kucheza sebene, ikafuata 'shoo' ya warembo kisha kupita jukwaani kwa mavazi ya ufukweni na ubunifu.
Burudani pia ilipambwa na kundi la Tanzania House of Talent (THT) na mwanamuziki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Wazekwa aliyeshindwa kukonga nyoyo za mashabiki.
Wanyange wengine waliowahi kutwaa taji la Miss Tanzania tangu mwaka 1994 ni Aina Maeda (1994), Emily Adolf (1995), Shose Sinare (1996), Said Kessy (1997), Basila Mwanukuzi (1998), Hoyce Temu (1999), Jacqueline Ntuyabaliwe (2000), Happiness Magese (2001), Angela Damas (2002), Sylvia Bahame (2003), Faraja Kotta (2004), Nancy Sumary (2005) na Wema Sepetu (2006).
Wadau mnasemaje?
1 comment:
watanzania mbona mna ubaguzi wa rangii hivi mnalia kwa kuwa ana asili ya kihindi au hakuwa na sifa za kufikia kuwa miss?
kama mnajali uhindi basi wote ni washamba huyo dada kazaliwa tz kwa maana ni mtz nyie kinachowauma kitu gani?ushamba tu kisa ana asili ya uhindi ndo asiwe miss huyo hoyce temu kutwa kujitongozesha kwa wahindi !!!!!!!!!!1
Post a Comment