Saturday, October 27, 2007

Watanzania tusiruhusu dini itutengenishe (Maoni)


TANZANIA imebahatika kuwa nchi moja wapo yenye utulivu duniani kufuatia wananchi wake kuishi kwa amani na ushirikiano, bila kujali tofauti za kidini au kikabilia.

Hali hiyo iliifanya jumuia ya kitamataifa imwalike Rais Jakaya KIkwete kuwa mgeni rasmi kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Kiimani ambao uliwajumuisha wakuu wa madehebu ya dini mbalimbali duniani, uliofanyika katika Jiji la Napoli nchini Italia, mwezi huu.

Sababu kuu ya kualikwa Rais Kikwete, ambaye pia alihutubia kwenye mkutano huo, ni kutokana na Tanzania kuwa nchi ya mfano ulimwenguni kwa watu wake kuishi kwa uelewano, ushirikiano na amani bila kujali tofauti zao za kidini.

Ni dhahiri kwamba sifa hii ya kihistoria ya Watanzania kuishi kama ndugu (licha ya kuwepo kwa dini tofauti), imesaidi kudumisha amani na umoja wa kitaifa mpaka sasa.

Itakumbukwa kwamba hata wakati wa harakati za kupigani uhuru, Watanzania (Tanganyika) walikuwa na mshikamano na ushirikiano uliovunja mipaka ya kidini na kuwafanya kuwa kitu kimoja, hivyo kutuwezesha kupata uhuru haraka na bila kumwaga damu.

Wataalam wa masula ya jamii na siasa wanajua jinsi dini inavyoshika nafasi kubwa katika maisha ya watu, kwa vile inahusisha masuala ya imani ambayo yako ndani ya mtu na huchukua sehemu kubwa katika maamuzi juu ya mfumo wake wa maisha.

Watetea amani duniani pia wanafahamu jinsi masuala ya dini yalivyo nyeti na yanavyoweza kusambaratisha amani yakitumiwa vibaya katika jamii na hasa ukitokea mgogoro wa kidini. Ubaya wa migogoro ya kidini, huvunja hata uhusiano wa ndugu kwa sababu mtu anakuwa tayari kutengana au kupigana na ndugu yake ili kutetea imani (dini) yake.

Miongoni mwa migogoro mibaya isiyoweza kupatiwa ufumbuzi haraka, ni ya kidini na kikabila. Migogoro ya kidini ni mibaya zaidi kwa kuwa ikitokea, hata kabila moja na ndugu wa damu wanaweze kutengena, au kupigana na hata kuuana kutokana na kila mmoja kutetea dini yake.

Tunaimba kwamba Tanzania imebarikiwa na Mungu kuwa nchi ya amani, kwa sababu mpaka sasa hakuna migogoro ya kidini iliyowahi kuliingiza taifa hili kwenye vurugu kama inavyotokea katika nchi mbalimbali duniani na hata barani Afrika, ikiwemo Nigeria ambako kila mara watu wanauana kutokana na migogoro ya kidini.

Tunalazimika kuwakumbusha watanzania kuhusu jambo hilo kutokana na hali inayotaka kujitokeza sasa, kufuatia baadhi ya waumini na viongozi wa dini kuanza kulumbana na kutupiana maneno makali yenye vitisho, kwa misingi ya hoja za kidini, ambazo zikiendelea zitaliingiza taifa kwenye wakati mgumu, kwa vile moto mkubwa hutokana na kipande cha mkaa wa moto au kijiti kimoja cha kiberiti.

Ikumbukwe kwamba, mpaka sasa Waislamu na Wakristo ni ndugu na marafiki kwa kuwa hata katika hafla mbalimbali za kidini kuna utaratibu wa kualikana na pia viongozi wake wanashirkiana katika mambo mengi yenye lengo la kudumisha amani na kuletea maendeleo katika jamii nchini.

Mbali na ushirikiano wa viongozi hao, kwenye makazi ya watu wa dini zote mijini na vijini waishi pamoja kama ndugu na wanashirkiana na kusaidiana katika masuala mbalimbali, kama vile misiba, harusi na mengineyo. Huu ndiyo upendo wa watanzania ambao ndiyo kiini cha amani ya nchi yetu.

Tunakumbusha kwamba, amani ni bidhaa adimu na ya thamani kubwa na kila anayeipoteza si rahisi kuirejesha, kwa kuwa gharama yake ni kubwa. Hivyo tunawaomba Watanzania wote kuwa makini na tusikubali wala kuruhusu dini itutengenishe.

Mungu ibariki na ilinde Tanzania.

No comments: