Friday, November 09, 2007



Bakita na mkakati wa kueneza Kiswahili kwa njia ya redio, TV.

Magnus Mahenge.

HabariLeo; Friday,November 09, 2007 @01:04
Katibu Mtendaji wa Bakita, Dk Anna Kishe, akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) kuhusu kufanyika kwa kongamano la wazungumzaji Kiswahili duniani. Kulia kwake ni Oni Sigara, mmoja wa maofisa habari wa Bakita.
KONGAMANO la idhaa za redio na televisheni zinazotumia Kiswahili Tanzania na nje ya nchi, litafanyika kwa siku nne katika ukumbi wa Mkukuta, uliomo katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), litafanyika Novemba 12 hadi 15, mwaka huu na ni ufunguo wa kujua namna Kiswahili kinavyokua na watumiaji wanavyoongezeka duniani.

Akizungumza na vyombo vya habari, Katibu Mtendaji wa Bakita, Dk. Anna Kishe, anasema kongamano hilo linafanyika kwa mara ya pili tangu kuanzishwa kwa chombo hicho miaka 40 iliyopita. Kwa mara ya kwanza lilifanyika katika miaka ya 1980.

“Kongamano hili linafanyika ili kuweka mikakati ya pamoja ya kukuza na kueneza Kiswahili duniani kwa njia ya redio na televisheni,” anasema Dk. Kishe.

Nia ni kuweka mbinu za pamoja za kujenga mazingira mapya ya kushughulikia mahitaji, maslahi na matatizo ya wadau wa lugha hiyo duniani na kubainisha njia za kuongeza zaidi watumiaji, aina na ubora wa huduma zinazotolewa kwa lugha hiyo.

Ukuaji wa Kiswahili nchini umechangiwa na Bakita, ambayo ndiyo tochi ya kutoa mwanga kwa watumiaji wa lugha hiyo ndani na nje ya nchi.

Kiswahili kimekuwa kikiongeza watumiaji wake na hadi sasa kuna watumiaji zaidi ya milioni 110 duniani.

Ukuaji huo umekwenda sambamba na ukuaji wa ndani, ambapo hadi hivi karibuni utafiti umebaini kuwa asilimia 97 ya wananchi wa Tanzania, wanazungumza Kiswahili na kukitumia kama lugha yao ya kwanza katika mazungumzo.

Miaka ya hivi karibuni, Kiswahili kimezidi kukwea na kuwa miongoni mwa lugha kubwa zinazotumiwa na mataifa mengi.

Mmoja wa Maofisa Uhusiano wa Bakita, Oni Sigala, anasema Kiswahili kimeshika nafasi ya sita, kikitanguliwa na Kiingereza, Kifaransa, Kihispania, Kiarabu na Kirusi na kukiacha nyuma Kijerumani, Kichina na Kireno.

Kauli mbiu ya kongamano hilo ni ‘Kiswahili kwa Ushirikiano na Mshikamano’. Kongamano hilo litachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha ushirikiano baina ya asasi za utangazaji, zinazotumia lugha hiyo duniani na namna zinavyokuza na kueneza lugha hiyo duniani.

Dk. Kishe anasema kongamano hilo linatarajia kujenga mazingira mapya na bora zaidi ya kiutendaji, yatakayowezesha kushughulikia kwa ufanisi zaidi mahitaji, maslahi na matatizo ya wadau mbalimbali wa Kiswahili, hasa asasi za utangazaji.

Kongamano hilo litazikutanisha redio ya Umoja wa Mataifa, Deutch Welle, BBC, Radio Vatican, Radio China International, Radio ya Ufalme wa Saudi Arabia, National Media Group ya Kenya, Radio Sauti Injili ya Kongo na Voice of Nigeria na nyingine nyingi.

Pamoja na hizo za nje, vituo vya redio vitavyoshiriki ni Radio Upendo, Radio One, Radio Faraja, Radio Tanzania, Radio Free Africa, Sauti ya Tanzania Zanzibar, Radio Imani-Morogoro, Radio Tumaini na Radio Zenj FM.

Vituo vya luninga vilivyoonyesha kupata mwamko wa kushiriki kongamano hilo ni pamoja na Mwakaleli, Sua, ya Taifa, DTV, CTN, Channel Ten, Abood, Sumbawanga na Independent na nyinginezo.

Waalikwa wawili kutoka katika kila idhaa, redio na runinga watakuwa na wakati mwafaka wa kushiriki katika kuchambua kinaga ubaga maendeleo na mchango wa Kiswahili katika kuboresha na kuendeleza maisha ya mwanadamu katika nyanja ya mawasiliano.
Idhaa za Kiswahili za redio na runinga za nje kwa pamoja na za ndani, zitakutana na kuangalia kama uwezekano wa kupanua wigo na kuongeza wingi wa watumiaji wa lugha hiyo. Mkusanyiko huo utaangalia, aina ya lugha inayotumika katika kuwasiliana, ubora wake na huduma nyingine kama ni sanifu na fasaha kote duniani.

Kongamano hilo pia litakuwa sehemu ya maadhimisho ya miaka 40 ya tangu kuzaliwa Bakita Julai 1967.

Katika nafasi hiyo, Bakita itajinadi na kutambulisha shughuli zake za uratibu na usimamizi wa Kiswahili Tanzania na nje ya nchi.

“Bakita inaadhimisha miaka 40 tangu kuanzishwa, hivyo imekomaa … Hivyo ina fursa kubwa ya kutoa mchango madhubuti katika kukuza na kuendeleza matumizi ya Kiswahili ndani na nje ya nchi,” anasema Dk. Kishe.
Katika kuratibu na kusimamia Kiswahili, Bakita imekuwa ikitumia njia za barua, barua-pepe, faksi simu na mitandao kuwasiliana na idhaa, redio na luninga za nje na ndani.

Lakini kwa kuitisha kongamano hilo, Bakita imeamua kupanua wigo wa kuwasiliana na kuhamasisha watumiaji wa idhaa za Kiswahili za nje ili waendelee kutoa kipaumbele matumizi ya lugha hiyo.

Kongamano hilo linalenga kutoa fursa ya kubadilishana mawazo, kuhusu mbinu za kuendeleza lugha hiyo kwa ufasaha na ubora wake kwenye vyombo vya habari vya kielektroniki.

Kongamano hilo ambalo litafunguliwa na Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein na kufungwa na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mohamed Seif Khatib, litakuwa jukwaa zuri la kuchambua makala mbalimbali kuhusu ukuaji wa Kiswahili.

Pia litakuwa jukwaa huru la kuonyesha kazi mbalimbali za Kiswahili, kama istilahi na nyingine zilizotungwa kwa nyakati mbalimbali za kutambulisha Kiswahili na kuonyesha teknolojia ya habari na mawasiliano.

Kwa wale walioibuka washindi katika kutumia lugha hiyo, utakuwa ni wakati mwafaka kupewa tunu ya vyeti na ngao.

Jukwaa hilo litatumika kwa majadiliano na kutangazwa wazi au moja kwa moja na vyombo vya habari kama redio na luninga.

Ni wazi wajumbe mbalimbali watakaoshiriki katika kongamano hilo watapata fursa ya kuonyesha namna wanavyofaidika na Kiswahili.

Licha ya kualika idhaa zinazotumia Kiswahili, Bakita imealika taasisi mbalimbali zinazotangaza vipindi kwenye redio na televisheni nchini.

Taasisi hizo ni zile zinazotumia Kiswahili katika kuelimisha umma, hivyo kuongeza idadi ya watumiaji wa Kiswahili nchini na nje ya nchi.
Mchunguzi wa Lugha wa Bakita, Richark Mtambi, anataja taasisi zilizoalikwa kushiriki katika kongamano hilo ni pamoja na Padep, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Chuo cha Mwalimu Nyerere.

Nyingine ni Kampuni ya Ulinzi ya Zanzibar, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar na Bodi ya Pamba nchini. Milango bado wazi kwa nyingine ambazo hazijathibitisha kushiriki, kwani kongamano hilo ni jukwaa la kutambua mchango wao katika kutumia lugha hiyo nchini na nje ya nchi.

Kangamano hilo linatoa nafasi ya kushiriki kwa vyombo vya habari vya elektroniki nchini.

Hata hivyo, hadi sasa mwitikio wa kujiandikisha kushiriki kwa vituo vya Dar es Salaam vya redio na televisheni ni mdogo, ukilinganisha na mwamko uliopo katika vituo vilivyoko mikoani.

Kongamano hilo litafungua ushirikiano wa karibu wa kikazi ndani ya vyombo mbalimbali vinavyotumia Kiswahili, hivyo kutekeleza kazi mojawapo ya Bakita, ambayo ni kuhakikisha kuwa watumiaji wa Kiswahili wanadumisha na kuendeleza ushirikiano wa kikazi.

Kazi yake nyingine ni kuratibu na kusimamia watumiaji wa Kiswahili, ikiwamo asasi mbalimbali nchini na mawakala wa wote wa lugha ndani na nje ya nchi, ili kukuza Kiswahili nchini na duniani kwa ujumla.

Bakita iliundwa kwa Sheria ya Bunge Namba 27 ya mwaka 1967.

No comments: