Thursday, November 29, 2007

MRABA WA MAGGID

"Heri kuongoza walioelewa, kuliko walioachwa gizani"

Maggid Mjengwa

JUMAPILI ya kesho kutwa, tutasherehekea miaka 46 ya Uhuru tangu Desemba 9, 1961 Tanganyika ilipopata uhuru.

Huu ni wakati wa kutafakari. Ni wakati wa kufikiri kwa bidii. Na ili tuelewe tunakokwenda ni busara kuangalia tulikotoka na tulipo sasa. Natafakari nchi ndogo ya Sweden. Tanzania ni mara mbili ya nchi hii kwa ukubwa. Sweden ni taifa kubwa sana kiuchumi na kisiasa.

Septemba mwaka jana Sweden walifanya uchaguzi mkuu. Raia walimchagua Waziri Mkuu ambaye umri wake hauzidi umri wa Tanzania kama nchi. Anaitwa Freidrik Rehnfeldt. Hajatimiza hata miaka 46.

Nakumbuka, mara tu alipounda baraza la mawaziri, hazikupita siku nane kabla ya mawaziri wake wawili kulazimishwa kujiuzulu. Walijiuzulu kutokana na kashfa ya kujipendelea kwa kutolipa ushuru wa televisheni na kukwepa kodi. Kazi ya kufichua dhambi za mawaziri hao ilifanywa na vyombo vya habari vikishirikiana na wananchi, walipa kodi.

Pamoja na ujana wake, Waziri Mkuu huyo wa Sweden alionyesha kukomaa kisiasa. Kwenye baraza lake hakuwa tayari kuwa na mawaziri ambao wangekuwa ni "mzigo wa ksiasa" kwake.

Aliwatua mapema na kuendelea na changamoto nyingine za kuongoza nchi yake. Miaka 46 ya uhuru wetu si sawa na miaka 10 ya uhuru. Dunia imebadilika. Zamani tulikuwa na "Wajomba" wa kutubeba hata pale tulipovuruga vuruga mambo ndani ya nchi zetu. Hali imebadilika.

Kwa viongozi wa nchi zetu, kwenda na wakati ni pamoja na kuwa na uwezo wa kusoma alama za nyakati. Wakati umebadilika. Miaka 46 ya Uhuru bado tunachangiwa asilimia 46 ya bajeti yetu. Hii ina maana katika shilingi mia ya matumizi yetu, shilingi 46 zinatoka kwenye mifuko ya wahisani. Wakati wazee wetu walipokuwa wakidai uhuru walitamka; "Ni fedheha kutawaliwa". Leo baada ya miaka 46 ya Uhuru umefika wakati wa kizazi chetu kutamka; " Ni fedheha kufadhiliwa".

Kama nchi tumeweka bakuli ambamo wahisani hutumbukiza pesa zao za misaada. Wenyewe wanaita " Basket Fund". Kizazi hiki kifike mahali kijisikie aibu kuendelea kutegemea fedha za wafadhili kuendeshea mambo yetu. Watanzania lazima tuelewe, kuwa wahisani hawa wanaochangia asilimia 46 ya bajeti yetu nao wanabanwa sana na wapiga kura wao.

Katika chaguzi zao, vyama vya nchi za wenzetu vimetoa ahadi kadhaa kwa wapiga kura wao. Mojawapo ni hii; kuwa wakipewa fursa ya kuunda serikali, basi watahakikisha wanadhibiti mapato na matumizi ya fedha za wananchi, wapiga kura wao.

Ikumbukwe, kuwa moja ya shutuma zinazotolewa na wapiga kura wa nchi hizo ni namna serikali zao zinavyokumbatia tawala za nchi zinazoendelea zenye kuendekeza ufisadi ikiwa ni pamoja na ufujaji wa mali za umma na ubadhirifu wa fedha za misaada. Misaada inayotokana na jasho la walipa kodi wa Ulaya na Marekani.

Ni katika mantiki hii inapaswa kuwaelewa wakubwa hawa wanapofuatilia na kutoa maoni yao juu ya taarifa za ufisadi wa mabilioni ya shilingi katika serikali zetu. Kimsingi wanafuatilia fedha za walipa kodi wao waliowaahidi kufanya hivyo katika chaguzi zao.

Mwishoni mwa mwaka jana tuliambiwa, kuwa taasisi ya kuzuia Rushwa, TAKUKURU, ingepewa meno ifikapo Februari mwaka huu. Kuna wananchi wanaonong'ona mitaani juu ya aina ya meno waliyopewa TAKUKURU, kwani meno yako ya aina nyingi.

Hakika wananchi bado wanasubiri utekelezaji, maana njia ya kupambana na vigogo wa ufisadi ina tope zito. Ni rahisi kwa TAKUKURU kuwavua dagaa, sambamba na hilo, wanachotaka wananchi ni kuona Taasisi hiyo ikianza kuwavua kambale wakubwa wa ufisadi.

Itakumbukwa, kuwa kabla ya kuachia madaraka, rais mstafu Benjamin Mkapa alitamka; kuwa anaiacha nchi yenye uchumi ulio tayari kupaa. Lakini tufikiri, katika hali ya mvua ya manyunyu,rubani anaweza kuitayarisha ndege, akawasha injini, ndege ikawa tayari kuruka.Hata hivyo, ndege hiyo inaweza kubaki hapo uwanjani ikiunguruma bila kupaa. Hilo laweza kutokea kama mvua itaongezeka ghafla na barabara za udongo za uwanja huo kujaa matope.

Kujenga uchumi wa kisasa ni sawa na kutengeneza mazingira mazuri ya ndege, si tu kuweza kupaa, bali kuvutia marubani wengine kutua na ndege zao kwa salama na amani. Katika nchi yoyote yenye dhamira ya kweli ya kwenda mbele kimaendeleo, usalama na amani ni vitu viwili muhimu kuwapo. Bila usalama na amani hakuna maendeleo. Na katika mazingira yenye kuruhusu kushamiri kwa rushwa, kubwa na ndogo, basi, haki na usawa katika nchi hiyo hukosekana. Na pasipo na haki na usawa, hakuna amani na usalama.

Unaweza kuwa na amani katika nchi lakini ukakosa usalama kwa maana ya kuwa, ingawa nchi haimo katika vita, lakini wananchi kwa kiwango kikubwa hawana hakika ya usalama wa maisha na mali zao.

Hawana hakika ya maisha yao ya kila siku, chakula chao, afya yao, elimu yao na ya watoto wao. Nchi inaweza kuwa na amani lakini haina usalama kwa maana ya pili niliyoielezea. Na hilo la kukosekana kwa usalama huhatarisha kuvunjika kwa amani.

Kuwapo wa amani na usalama katika nchi hujengeka katika misingi ya haki na usawa, misingi ya kuaminiana. Misingi ya kuheshimu haki na uhuru wa raia kutoa mawazo yao. Ni lazima kuwapo misingi imara ya demokrasia. Wananchi ni vema wakawaamini viongozi wao, na viongozi pia ni vizuri wakawaamini wananchi wao. Na ili viongozi waaminike ni lazima wawe wakweli na wawazi. Wawe waadilifu.


RAIS Mstaafu Benjamin Mkapa

Yaweza kusemwa mengi juu ya mstaafu Mkapa. Lakini, katika awamu yake nimejaribu kufuatilia kwa karibu kauli zake ambazo hakika leo twaweza kufanya kazi ya kumhukumu kutokana na kauli zake hizo na matendo yake. Ni busara kuifanya kazi hiyo kwa haki.

Nakumbuka mstaafu Mkapa aliwahi kutamka; " Ni afadhali nichukiwe kwa kuwa mkweli, kuliko kupendwa kwa kuwa mwongo na mlaghai" Kisha akaongeza; " Kiongozi aliyejiridhisha kuwa jambo fulani ni la manufaa kwa wananchi wake hana sababu za kuogopa kuwa mkweli, na kuelezea kwa nguvu ya hoja, kwa nini sera, mikakati na mambo fulani ni ya lazima. Ni vema, na haki, kuongoza walioelewa, kuliko kuongoza walioachwa gizani". Alisema Mkapa.

Wanadamu hatuna budi kufahamu, kuwa uaminifu ni biashara nzuri, ni biashara yenye tija.

Tusipoaminiana na kibaya zaidi, tusipoaminiwa kama watu binafsi, tusipoaminiwa na wengine ndani na nje ya mipaka yetu. Hilo ni jambo la hasara kwa mtu mmoja mmoja na kwa taifa.

Haya ni mambo ya msingi kabisa kuyatafakari. Hii ni nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Ni lazima tuaminiane. Tulio wengi tuna mapenzi ya dhati na nchi yetu. Kama taifa, miaka 46 ya Uhuru inatutaka tutafakari kwa kina juu ya mustakabali wa taifa letu.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.

Kiselule: 0754 678 252,
Baruapepe: mjengwamaggid@gmail.com,
Blogu: http://mjengwa.blogspot.com

Kutoka Raia Mwema wiki hii.



No comments: