Thursday, November 29, 2007

WARAKA KUTOKA HUSTON

Ili tuendelee tunahitaji watu

Innocent Mwesiga.

MINTARAFU makala ya Jenerali Ulimwengu (Raia Mwema toleo namba 2) nimeona nitoe dukuduku ambalo lengo lake si kukinzana, bali kupanua wigo wa mjadala aliouanzisha.

Kwa kiwango fulani, ukiritimba wa muda mrefu katika safu za uongozi umechangia kibaba cha umasikini unaoisibu nchi yetu. Hivyo basi, kimsingi, mawazo yangu yanashabihiana na hoja ya Ulimwengu katika kona moja tu ya umuhimu wa uongozi bora.

Lakini ukosefu wa uongozi bora, si tatizo kubwa pekee linaloididimiza nchi. Ndiyo maana nachelea kwa jumla kukubali mantiki ya kuwa Ni uongozi, basi; kwa maana kwamba “ili tuweze kuendelea tunahitaji vitu vinne: Mosi, uongozi bora, pili, uongozi bora, tatu, uongozi bora na nne, uongozi bora”.

Sidhani kwamba tukipata uongozi bora pekee, tutakuwa tumepiga hatua muhimu kuelekea katika maendeleo. Natofautiana na mawazo kwamba kuna kundi fulani la watu ndani ya jamii ambalo miongoni mwao, yupo mtu au watu wachache wenye sifa kamilifu za uongozi.

Kana kwamba kazi ya Watanzania bakia, ni kubainisha hilo kundi jalili lenye sifa mithili ya Kakakuona, na kuliibua mbele ya kadamnasi, ili likabidhiwe dhamana ya kuongoza Watanzania kuelekea katika maendeleo.

Kuendelea kuamini dhana ya uongozi bora pekee, ni kupalilia mazishi ya umuhimu wa nafasi ya kila mmojwa wetu katika ushiriki wa kulipia gharama za maendeleo. Kadiri tunavyoendelea kuamini ujio wa uongozi bora, ndivyo njia yetu ya kuelekea kwenye maendeleo inavyokuwa nyembamba na mwishowe itatoweka kabisa.

Ni kujidanganya kudhani kwamba siku moja atatokea kiongozi aliyekabidhiwa ufunguo wa mlango wa maendeleo, na sisi kazi yetu ni kumtafuta mpaka tumpate, ili aweze kutufungulia huo mlango. Katika hali ya kawaida ya maisha ya jamii, kiongozi wa namna hii hawezi kutokea, labda kwa miujiza ya Mwenyezi Mungu. Dhana hii inanikumbusha ushuhuda wa Biblia pale Petro alipopewa ufunguo na kukabidhiwa jukumu la kuongoza Kanisa lililoanzishwa na Yesu Kristo.

Kama kungalikuwapo kiu ya maendeleo miongoni mwa waumini wa Kanisa la Yesu, wangalimuomba kiongozi wao Petro, atumie ufunguo aliopewa na Yesu kuwafungulia mlango wa maendeleo. Lakini, ni vema kung’amua kwamba, hata hao waumini, wasingeweza kumuomba kiongozi wao awafungulie huo mlango bila wao kuimarika katika imani. Petro alipewa ufunguo kwa minajili ya kuwafanya wafuasi wake wawe na imani.

Tofauti na dini, uongozi wa nchi msingi wake si imani, bali ni sayansi ya kufikiri. Imani na sayansi ya kufikiri ni vitu viwili tofauti, kama lilivyo jua na mwezi. Mungu amempatia kila mmoja wetu ufunguo wa karama au vipaji, ambavyo tunatakiwa kuviunganisha kwa pamoja, ili tufungue milango ya maendeleo.

Yatupasa kudamka kutoka katika usingizi huo mzito wa fofofo, uliogubikwa na ukungu wa ndoto za kusubiri ujio wa uongozi bora, kana kwamba tuko katika zama za kusubiri ujio wa Masiya.

Binafsi nafikiri maendeleo yanaletwa na watu. Sioni dosari katika kanuni inayosema ili tuendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi, na uongozi bora. Hata hivyo, msingi wa hii kanuni ni watu. Siasa safi lazima ilenge maendeleo ya watu. Uongozi bora lazima ulenge maendeleo ya watu, ardhi lazima iwepo kwa ajili ya maendeleo ya watu, na watu wawepo kwa maendeleo ya watu, na si vinginevyo. Uvurugaji wa kanuni hii unakwenda sambamba na kufutika kwa ndoto za maendeleo.

Imekuwapo hoja kuwa suala la watu wa kuleta maendeleo si tatizo, kwani idadi ya Watanzania inakaribia milioni 40. Hivyo, kinachokosekana si watu, bali ni kitu kingine.

Sikubaliani na dhana ya kuwahesabu watu kama wahesabiwavyo kondoo malishoni. Au kudhani kwamba watu wanaweza kuongozwa kama waongozwavyo ng’ombe kuelekea mazizini.Watu wa kuleta maendeleo wana sifa ambazo asili yake ni ubinadamu.

Katika suala la maendeleo, haitoshi kutaja idadi ya Watanzania bila kutaja idadi ya Watanzania wenye sifa za kuleta maendeleo.

Watu wa kuleta maendeleo wamejaliwa utashi na ubongo, hivyo, wawe na haki ya kushiriki katika maamuzi yanayohusu maendeleo ya nchi yao. Wana midomo, hivyo, wawe na haki ya kujieleza na kusikilizwa, kuhoji na kujibiwa mambo ya msingi yanayohusu maendeleo ya nchi yao. Wamejaliwa macho, hivyo, wawe na haki ya kuona mambo muhimu yanayohusu maendeleo ya nchi yao. Wana masikio, hivyo, wawe na haki ya kuambiwa bila kificho na wakasikia masuala yote yanayohusu maendeleo yao.

Katiba ya nchi lazima ilinde haki za msingi za binadamu. Hakuna mtu au kikundi cha watu wachache kinachopashwa kupewa mamlaka ya kufuta haki za msingi za wananchi bila ridhaa yao. Lakini kwa bahati mbaya, Katiba yetu imekuwa ikibadilishwa bila kushauriana na wananchi. Matokeo haki za msingi za wananchi zimeporwa au zimewekewa masharti yasiyo ya lazima (rejea ibara ya 67 (1) kifungu kidogo (e) cha Katiba ya Tanzania).

Mara nyingi, zimetungwa sheria zinazompa mtu mmoja mamlaka na nguvu za kufanya maamuzi bila kuhakikiwa na taasisi zinazopaswa kuwawakilisha wananchi (rejea sheria ya madini ya mwaka 1998 ibara ya 10 (1) – (2) (a), (b), (c)). Ndiyo maana nafikiri kwamba, takwimu za idadi ya Watanzania kukaribia milioni 40, hazina maana yoyote, kama Watanzania wenye uwezo Kikatiba wa kufanya maamuzi ya kulikwamua au kulikwamisha taifa ni wawili au watatu. Katika msingi huu, idadi ya Watanzania wenye sifa za kuleta maendeleo haitoshi.

Suala jingine la kuzingatia wakati wa kuhusisha idadi ya watu na maendeleo ni asili ya binadamu. Bila kujali rangi, kabila, Uzungu, Uchina, au Uafrika, watu wote tunaunganishwa na kitu kimoja: ni udhaifu wa kibinadamu. Hakuna aliyemkamilifu au malaika wa kitabia.

Yawezekana kutofautiana maumbo, karama, au vipaji. Pia tunaweza kuwa na mseto wa sifa za kitabia ambazo ni msingi katika mahusiano yetu ndani ya jamii. Baadhi ya hizo sifa ni busara, maono, ujinga, welevu, uaminifu, wema, tamaa, udokozi, wizi, utapeli, na nyinginezo. Lakini sifa ya msingi ambayo iko kwa kila mmoja wetu, ni ile ya udhaifu wa kibinadamu.

Sifa za kitabia zinaweza kuchochea au kudumaza, kuongeza au kupunguza kiwango cha udhaifu wa kibinadamu. Katika hali ya kawaida ya maisha ya ubinadamu wetu, ni nadra kumkuta mtu aliyejaliwa sifa mbaya peke yake, au sifa nzuri peke yake.

Udhaifu wa ubinadamu unatawaliwa na mseto wa sifa mbaya na nzuri kwa wakati mmoja. Ndiyo maana si haba kumkuta mtu aliyejaliwa sifa nzuri ya maono au uwezo wa kuona mbali, lakini pia ana sifa mbaya ya udikiteta.

Mwingine ana sifa nzuri ya werevu, lakini sifa yake mbaya ni udokozi. Mwingine ana busara, lakini si mwaminifu. Kuna anayeipenda sana nchi yake, lakini hashauriki au wakati mwingine ujinga unamzidi kimo.

Bahati mbaya sifa za msingi za kibinadamu zinabadilika kutokana na urithi wa vionjo vya kibaiolojia, malezi, mazingira, umri na sababu nyinginezo. Ndiyo maana baadhi ya watu wasipokuwa na fedha wanakuwa na tabia ya unyenyekevu na heshima kwa wenzao, lakini pindi wapatapo fedha, wanakuwa na kiburi au dharau kwa wenzao.

Wengine katika ujana wao wamejaliwa vipaji vya kufikiri vizuri na kufanya maamuzi ya maana kwa manufaa ya jamii inayowazunguka. Lakini wakiwa na umri wa makamo, yanaweza kutokea mabadiliko ya kibaiolojia ndani ya miili yao, ambayo yako nje ya uwezo wao, na kusababisha wawe na uwezo duni wa kufikiri unaofanya maamuzi yao kuwa ya hovyo. Pia wapo raia wema, wasikivu, wanaopenda kuchanganyikana na kushauriana na wenzao, lakini wanapopata madaraka wanalewa na kuwa malimbukeni.

Katika mseto wa namna hiyo wa kitabia ndani ya udhaifu wa kibinadamu, si jambo jema kuwakabidhi watu wachache mamlaka yote ya kuamua mustakabari wa waliowengi. Hatuwezi kubashiri viwango vya mabadiliko ya tabia za watu kabla na baada ya kukabidhiwa dhamana ya uongozi. Kuna masuala hayahitaji ubashiri na yanajulikana waziwazi. Mosi, binadamu wote wana udhaifu wa kibinadamu, pili, hakuna binadamu aliyejaliwa vipaji vyote kiasi kwamba apewe nafasi ya kuvitumia kwa niaba ya wote, tatu, kila mtu amejaliwa karama au kipaji ambacho ni tofauti na mwingine, na nne, binadamu wote wana mseto wa sifa mbaya na nzuri.

Hivyo basi, hatuna sababu ya kucheza kamari wakati wa kutafuta maendeleo. Msingi wetu wa maendeleo ujengeke katika masuala ambayo tuna uhakika nayo kama niliyo yataja.

Tuchote busara za wahenga waliotuhasa kwamba umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Tupeane miadi ya kukutana kama taifa kwa lengo la kuunganisha karama au vipaji vya kila mmoja wetu.

Tuweke mfumo ambao utatoa nafasi kwa kila mmoja wetu kupata haki na mamlaka ya kikatiba ya kudhibitiana. Jukumu hili liwe ni la wote na si kumkabidhi mtu mmoja au kikundi cha watu wachache. Hatua ya kuwahusisha watu wote katika masuala ya msingi ya maendeleo itakuwa ni muhimu kuelekea kwenye maendeleo na kujenga jamii shadidi, hata kama tutakosa uongozi bora.

Ni kweli, ukiondoa mitume, wamekuwapo binadamu wa kawaida ambao wanasifika kwa kutumia vipaji vyao kwa muda wote wa uhai wao, ili kutoa mchango mkubwa wa kuendeleza jamii walimoishi. Wengine wanasifika kwa kutokubadili tabia na sifa zao nzuri, hata kama mazingira walimoishi yalibadilika kwa kiasi kikubwa.


NELSON Mandela

Mfano, Kabla hajahukumiwa, Nelson Mandela alisema kuwa alichokuwa anapigania katika maisha yake yote ni jamii huru ambamo watu wote wataishi kwa mapendo, uelewano, furaha, amani, na haki sawa kwa wote. Alipotoka jela baada ya miaka 27 alirudia maneno yaleyale. Alipopewa nafasi ya kuongoza nchi, badala ya kulipiza kisasi kwa waliomuweka jela, aliyaweka maneno yake kwenye matendo kwa muda wa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake. Mpaka sasa hivi anatamka maneno yaleyale bila kuwa na soni.

Mwaka 1967 Mwalimu Nyerere alitangaza Azimio la Arusha, ambalo ndani yake kulikuwa na kipengele cha maadili ya viongozi. Kimaadili, hata wake wa viongozi hawakutakiwa kuendesha miradi ya kawaida ya kuendeleza familia zao. Mwaka 1985 wakati anang’atuka madarakani, Mwalimu Nyerere na Mama Maria walikuwa wanafanana na Azimio la Arusha. Mwaka 1995, Mwalimu alisisitiza msimamo wake na kusema kwamba alikuwa haoni dosari yoyote katika Azimio la Arusha. Aliliishi Azimio la Arusha mpaka siku yake ya mwisho.

Lakini lazima tukubali ukweli kuwa watu mithili ya Mandela, Gandhi, Martin Luther King Jr, Nyerere na wengineo, ambao wanasifika kujaliwa sifa nzuri za maadili, maono, na busara kwa muda mrefu, ingawa pia walikuwa na udhaifu mwingine, hawazaliwi mara kwa mara. Hatuwezi kuweka nchi zetu rehani kwa miongo kadhaa tukisubiri mtu kama Nyerere azaliwe tena. Hata huo uongozi wa kusadikika ukijitokeza na kutukuta tumelala usingizi wa namna hii, maendeleo ya kweli na ya muda mrefu, hayawezi kupatikana.

Vilevile uongozi unakuwa bora kama unapata nguvu na akili kutoka kwa wananchi. Ni muungano wa nguvu na akili za Watanzania ambao uliwatisha wakoloni mpaka wakabwaga manyanga na kutimua mbio.

Nyerere peke yake asingefua dafu. Muungano wa nguvu na akili za Weusi wa Afrika Kusini, waliopoteza maisha yao, na wale waliokuwa tayari kujitoa muhanga, wakisaidiwa na muungano wa nguvu na akili za wapenda haki popote duniani, ndio uliowafanya Makaburu wasalimu amri. Mandela peke yake asingefika mbali, kwani alikuwa jela. Vivyo vivyo, kwa Martin Luther King Jr, na Indira Gandhi.

Hata hivyo, yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Yatupasa kufanyia kazi kile tulichonacho mkononi. Watu waliosheheni jamii zetu ni wale wanaozaliwa kila siku ambao wana udhaifu wa kawaida wa kibinadamu. Mfano, Benjamin Mkapa. Aliingia madarakani mwaka 1995 akisema kwamba alichukia rushwa kwa moyo wake wote, na asingekuwa na suluhu kwa wala rushwa.

Kumekuwapo na wito kutoka kwa wananchi wa kumtaka atie neno, na ikiwezekana ayarudie maneno aliyoyasema mwaka 1995, lakini wapi, anapata kigugumizi.

Itaendelea

inno@comcast.net

Kutoka Raia Mwema.

No comments: