Thursday, November 01, 2007

Kutoka gazeti jipya la Raia Mwema

CCM yahitaji Sokoine mwingine -Mangula


Philip Mangula, katibu mkuu mstahafu wa CCM.

KATIBU Mkuu mstaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula, amesema kutokana na kukithiri kwa rushwa, Tanzania inahitaji kiongozi kama alivyokuwa Waziri Mkuu wa zamani Edward Moringe Sokoine, kukabiliana na hali hiyo.

Katika mahojiano maalumu na Raia Mwema nyumbani kwake, kijijini Kinenulo, Tarafa ya Imalinyi, wilayani Njombe, Mkoa wa Iringa, Mangula alisema kuna wakati viongozi wa kitaifa wanakuwa wanafiki katika kupambana na rushwa kwa kutoa kauli katika majukwaa, zinazopingana na matendo yao.

“Wakati mwingine viongozi wa kitaifa wanakuwa wanafiki. Wanapotafuta kura wanatenda tofauti na wanapohubiri rushwa majukwaani. “Matendo yao majukwaani yanakuwa kinyume kabisa na pale wanapokuwa kwenye uchaguzi ndani ya chama.

Matokeo yake, wanapoingia madarakani kwa njia za rushwa, wanashindwa kuikemea wakipata nyadhifa zao. “Hii ni hatari, na sijui tufanye nini, na hasa pale wapiga kura wanapotaka rushwa kwa nguvu.

Labda tutahitaji Sokoine (Edward) mwingine ili watu waziogope pesa hizo haramu,” alisema Mangula akirejea kukithiri kwa vitendo vya rushwa katika uchaguzi ndani ya CCM unaohitimishwa wiki hii.

Alisema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa mkali katika vita dhidi ya rushwa na hasa katika uchaguzi wa ndani ya CCM na hata serikalini. “Mwalimu alikuwa serious kuhusu watu wanaotaka uongozi kwa rushwa.

Wakati mmoja mgombea mmoja aliandaa chakula kwa ajili ya wajumbe, siku moja kabla ya uchaguzi. Kabla ya uchaguzi kuanza kufanyika, Mwalimu aliwaambia wajumbe kwamba kuna mtu ametumia rushwa kutaka uongozi. Akawaomba wajumbe wasimpigie kura na akatangaza kuondoa jina lake mapema kabisa. Huko ndiko kupiga vita rushwa,” alisema.

kwa sasa viongozi wa sasa wanajua sana kwamba kabla ya uchaguzi kunakuwa na mialiko mingi ya chakula lakini hawataki kuchukua hatua zozote kukabiliana na hali hiyo. Mangula alishindwa katika kuwania uenyekiti wa CCM mkoani Iringa, nafasi ambayo baadhi ya wachambuzi waliiona ni ndogo kwake kuiomba baada ya kushika wadhifa wa juu ndani ya chama hicho.

Anasema aligombea nafasi hiyo baada ya kushawishiwa sana na viongozi wakongwe wa CCM wa wilaya na hata mkoani baada ya kuwa ameamua kustaafu siasa na kufanya kazi za kilimo.

Anasema walimwambia nafasi hiyo haitambana sana. “Siku mmoja nilikuwa napita pale Makambako, nikakutana na rafiki yangu mmoja. Baada ya kusaliamiana akanishauri nikasalimiane na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa, ambao walikuwa wakielekea Iringa kwenye uchaguzi.

“Rafiki yangu huyo akanisihi kuwa ilikuwa muhimu kwangu kukutana nao kwa sababu wao ndio walikuwa wapiga kura wangu. Akaniambia kuwa ilikuwa muhimu kwangu kwenda kuwasalimia kwa kuwapa angalau soda... Nikamjibu kuwa kama ni salamu za kujuliana hali tu, nilikuwa tayari, lakini siyo salamu za kupeana soda.

“Nikamwonyesha kipeperushi chenye maelezo yangu binafsi. Akanikejeli kuwa wajumbe hawataki hayo siku hizi. Akasema mtindo huo umepitwa na wakati, hivyo nijirekebishe. Nikakataa, na mambo yakabaki hivyo. “Wao hivi sasa wanasema wanataka vipepe-rushwa, siyo vipeperushi... Hii ndiyo hulka ya wapigakura wetu wa sasa... CCM ya sasa sicho chama kile ambacho kiliongozwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere).

“Nilikataa kwa sababu kwangu ninaamini kuwa ni mwiko kuhonga. Kufanya hivyo ni mwiko. Nikifanya hivyo nitakuwa ninalikosea kanisa langu ambalo naliamini. Ni mwiko pia kwenye chama changu. “Kwa miaka yote 10 niliyokuwa Katibu Mkuu wa CCM nilikataa takrima, nilihubiri kuwa ni lazima kuzingatia kanuni za chama.

Kutoa takrima wakati wa uchaguzi ni kosa la kikanuni. Huwezi kutoa chakula, vinywaji au usafiri kwa watu wanaokwenda kukupigia kura. Kanuni za CCM zinakataa hilo,” anasema.

Mangula anasema pia kwamba hakutaka kutoa ‘soda’ kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM Iringa, kwa kuwa kichwani mwake ilikuwa imejaa picha ya ushiriki wake katika vikao vya kuwaengua watu walioshinda kura za maoni uchaguzi mkuu wa 2000 na hasa ule wa 2005.

“Mwaka 2000 wagombea 32 waliongoza katika kura za maoni za CCM, lakini ilibainika kuwa walikuwa wametumia pesa. Tulikuwa na njia kadhaa za kuthibitisha rushwa hiyo… Tulikuwa tukituma timu mbili au zaidi za kufanya uchunguzi, kila mmoja ikitoa ripoti ya siri inayojitegemea.

“Tulipobaini kuwa ripoti za timu zote zilikuwa zinafanana, ndipo tulipoamua kuwaengua wahusika. Wakati fulani tulilazimika kuchukua mtu wa nne katika kura za maoni, tukawaacha watatu. Wakati mwingine tuliamua kufuta matokeo na kura kurudiwa.”

Anasema kwamba wakati mmoja mgombea mmoja wa Mkoa wa Dar es Salaam alibainika kuwa alitumia pesa ili kujipatia kura, lakini walipobaini kulikuwa na kasoro, ilibidi watume timu za kuchunguza. Waliridhika na ripoti za timu hizo, na ndipo wakaamua kumwengua.

“Lakini cha ajabu viongozi wakubwa kabisa katika chama, tukiwa kwenye kikao cha chama , wakasimama kidete kumtetea mtu aliyetoa rushwa. Ilikuwa bahati sana, kwamba tulimjulisha mapema mwenyekiti wetu Rais Benjamin Mkapa) kuhusu ripoti hizo. Pamoja na kutetewa kwa nguvu zote, Mwenyekiti akaamua mhusika aenguliwe.

“Pamoja na mwiko wangu wa kutokuhonga, kushiriki kwangu kuwaengua watu waliotoa rushwa kulichangia zaidi kuwa na msimamo imara wa kukataa kutoa ‘soda’. Wagombea wengine walikuwa wakizunguka kwenye kata. Kila kata ina wajumbe sita wa mkutano mkuu wa mkoa. “Mimi sikuzunguka kwenye kata. Ukienda kwenye kata kila mjumbe kati ya hao sita atahitaji umpe kitu kidogo. Mimi siwezi na sitaweza kufanya hivyo.

Hivyo ndivyo nilivyo na nitaendelea kuwa hivyo.” Mangula anasema kwamba tatizo kubwa linalojitokeza kila uchaguzi unapofanyika siku hizi, ni kwamba wapiga kura ndio wanakuwa wa kwanza kuwashawishi wagombea wawape chochote.

Utawakuta wanadai vitu kama chumvi, soda, sabuni au hata pesa taslimu. “Hivi sasa wapiga kura wana-induce (wanachochea) wapewe chochote… Wapiga kura hivi sasa wana-demand vitu kutoka kwa wagombea. Hili ndilo lililonitokea mimi katika uchaguzi wa Iringa. Hii ni hatari kubwa. “Mimi nilishindwa Iringa kwa sababu sikutoa ‘soda’.

Ndiyo maana baada ya matokeo, nilitia saini ya kukubaliana nayo. Lakini katika hati ile niliweka angalizo, kwamba mwenendo wa pesa katika uchaguzi unahitaji nafasi zinazogombewa zitangazwe kwa njia ya tenda. “Nilitoa angalizo hilo kwa sababu kwa mwenendo uliopo mwenye pesa ndiye anapata uongozi.

Angalizo hilo liliwaudhi sana watu, lakini hali ndiyo hiyo katika uchaguzi hivi sasa. “Kulikuwa na sababu kadhaa ambazo zilisababisha mimi nishindwe uchaguzi ule. Sababu mojawapo ni kuwa mimi sikutoa pesa kwa wapiga kura. Ya pili, ni kwamba watu walikuwa wakijiuliza kuwa iweje mimi nitoke nafasi ya ngazi ya taifa hadi mwenyekiti wa CCM wa mkoa.

“Wengine walikuwa wakisema kwamba mimi nilikuwa nikigombea wadhifa huo ili nianzishe mtandao mpya wa kupambana na kundi la wana-mtandao kwa kuwa sitakiwi na kundi hilo.” Kundi la wana-mtandao ni lile lililotumiwa na Jakaya Kikwete katika mchakato wa kumtafuta mgombea urais wa CCM.

“Lakini pia sababu nyingine iliyochangia kushindwa kwangu ni pale mtu alipotuma watu, waliojifanya kuwa wanatoka anti-corruption (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa- TAKUKURU). Hawa waliwatisha wajumbe waliokuwa wakija kwenye uchaguzi. “Waliwahoji ni nani aliwalipia usafiri wa mabasi waliyokuwamo… Kuhoji huko, tena kwa ukali wa hali ya juu, kuliwakera wajumbe kwa sababu walichelewa kufika kwenye eneo la mkutano.

Baadaye wakawaruhusu, huku wakiwanong’oneza kuwa mimi ndiye niliyekuwa nimewatuma, kumbe sivyo. “Najua sana mambo yalivyokwenda kombo, lakini sikuona sababu ya kulalamika. Nimekuwa bize (busy) nikilima. Mimi ninafahamu kutoa ‘soda’ ni mwiko kwenye uchaguzi, kwa mujibu wa kanuni za CCM.
“Tatizo linalokipata chama chetu, ni kwamba wajumbe hawa wa mikoa, wanaoomba ‘soda’ kutoka kwa wagombea, ndio hao hao wanakwenda kushiriki katika chaguzi za ngazi ya taifa. “Huko pia hujifunza kutokana na rafu wanazozifanya viongozi wanaowania uongozi wa kitaifa. Wanarudi na dhambi ya kutaka ‘soda’ kwenye maeneo yao. Huu ni ugonjwa.” anasema.


Kutoka: Raia Mwema


1 comment:

Anonymous said...

mwaweza soma hili gazeti kwenye mtandao kupitia http://www.raiamwema.co.tz/index.php#