KWA wiki kadhaa sasa tumekuwa tukishuhudia, ama tukitangaziwa, hali mbaya, na mauti hasa, ambayo yememfika mmoja kati ya Watanzania wenzetu wawili, waliolazwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI) na wakafanyiwa upasuaji ambao haukustahili.
Tuwape pole ndugu na jamaa wa marehemu Emmanuel Mgaya na tuendelee kuomba kwamba Emmanuel Didas hali yake inaendelea kuwa njema kusubiri tiba. Tayari tumeambiwa kwamba Didas anatafutiwa namna ya kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu kwa nia nzuri ya kutaka kuokoa maisha yake. Hakika hilo ni jambo zuri. Na tumpongeze yeyote aliyefikiria jambo hilo kwa mara ya kwanza.
Lakini zaidi ya pongezi kuna mambo ya kuzungumza kwa uwazi. La kwanza ni kwamba uamuzi wa kumsafirisha nje kijana huyo umechelewa mno kufanywa. Yawezekana ni kweli kwamba kwa hali yake ya maumivu kweli asingeweza kusafirishwa kama wanavyoeleza wenyewe wenye taaluma yao.
Lakini si kuchukua maamuzi kama hayo ya kumsafirisha ni sehemu ya taaluma yao pia? Kwamba watakuwa katika somo moja ama jingine, wamepitia namna ya kumsafirisha mtu mwenye maumivu ya aina yake?
Ukiacha hilo la uamuzi na taaluma kuna pia ugoigoi wa kusafirisha watu kwenda kutibiwa nje. Kasi iliyopo kwa sisi kina pangu pakavu tia mchuzi na vigogo hakika inapishana sana.
Hakika kama Didas ama hata Mgaya, wangekuwa ni vigogo, wangekwisha kuwa wamesafirishwa kitambo kwenda huko kunakoelezwa kunatolewa tiba nzuri.
Na mifano ya hayo ni mingi. Majuzi kigogo mmoja alipata ajali mikoani, yeye haraka haraka kapelekwa nje kwa matibabu, huku nyuma miongoni mwa walioumia sana hakuna aliyewakumbuka, baadaye ikawa ni hadithi ya mauti!
Ha hapa ndipo kwenye tatizo kubwa. Ghafla miongoni mwetu wamezuka watu zaidi na watu shinda. Kuna wenzetu maisha yao yana thamani kubwa kuliko sisi wengine.
Kwa hiyo jamii yetu ambayo kwa miaka mingi haikuwa na matabaka ya aina hii, sasa inadhihirisha kuwa matabaka ni lazima. Na wenye madaraka hawahitaji waumie sana, mkwaruzo kidogo tu basi safari ya India hiyo!Kutoka Raia Mwema wiki hii.
No comments:
Post a Comment