Thursday, November 29, 2007

WASIFU WA WIKI

Nitawaanika makuwadi wa siasa za Tanzania - Zitto

Aristariko Konga

ZITTO Zuberi Kabwe ni jina ambalo limepata umaarufu mkubwa, hasa kutokana na kijana huyo kuwa machachari katika Bunge. Lakini umaarufu wake umekuwa mkubwa zaidi pale aliposimama kidete kuhoji uhalali wa mkata wa uchimbaji madini huko Buzwagi, Kanda ya Ziwa, na kasha kusimamishwa ubunge kutokana na hoja yake hiyo.


Zitto Zuberi Kabwe

Ni mmoja wa viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kupitia chama hicho.

Amekuwa mstari wa mbele katika masuala ya siasa, tangu nilipomfahamu akiwa katibu wa serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa hakika, kama ni kulelewa na kupikika katika siasa, basi Zitto Kabwe amezama katika uwanja huo, tangu akiwa mshiriki wa uaandaaji wa makongamano ya kisiasa katika Chuo hicho.

Pengine katika kauli ambazo siwezi kuzisahau, ni kauli moja ambayo niliikumbuka mara baada ya kusoma makala mmoja iliyokuwa ikimhusu Zitto, kwamba alikuwa ameingia CHADEMA, na alikuwa ni mmoja wa vijana wenye uwezo wa hali ya juu.

Akichangia mada kwenye kongamano katika ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Zitto alisema: "Lazima wanasiasa watufunze na kutupisha, kwa sababu sisi ndio tutakuwa wabunge na mawaziri wa baadaye."

Kwa hiyo niliposikia kwamba Zitto amejiunga na kinyang'anyiro cha ubunge katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, kwa hakika, sikushangazwa. Nilijikumbusha tu, kwamba kauli yake ilikuwa sehemu ya maisha yake ya kisiasa.

Hivi karibuni Zitto aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Kuchunguza Mikataba ya Madini.

Katika mahojiano na RAIA MWEMA mwishoni mwa wiki iliyopita, Zitto alifafanua masuala kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuuhakikishia umma kuwa hawezi kufunga kinywa chake kutokana na uteuzi huo wa mkuu wa nchi.

“Ninaweza kudiriki kusema kwamba nipo comfortable na uteuzi wa Rais. Sidhani kama imekuwa ni njia ya kuninyamazisha. Siamini hivyo.

“Inawezekana kuna wana CCM ambao wanadhani uteuzi wangu ni njia ya kuninyamazisha. Kamwe siwezi kunyamaza. Najua kuna kazi nzito mbele yangu na wenzangu.

“Kama kuna watu wanadhani wanadhani kuwa kamati hiyo ni mtego wa kisiasa, bado wako wrong (wamekosea)…Kama wanadhani kuwa uamuzi wa Rais kuniteua mimi ni njia ya kuninyamazisha, basi wamekosea. Sitanyamaza kamwe.

“Inabidi watu wafahamu kuwa suala la uchunguzi wa mikataba ya madini ni la maslahi ya taifa. Sijui kama ni la kisiasa. Ni suala la ulinzi wa maslkahi ya taifa letu.”

Zitto anasema kwamba suala hilo si la ushindani wa CCM na CHADEMA, ingawa amesikia baadhi ya watu wengine wakisema kwamba baadhi ya wajumbe wa kamati hii ni marafiki wa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, ambaye alishiriki kutia saini Mkataba wa Buzwagi, ambao ndio ulioibua mjadala katika Bunge, na kupelekea Zitto kusimamishwa ubunge.

“Kuna masuala kwamba baadhi ya wajumbge wa kamati ni marafiki wa Karamagi, ni wanasiasa…Lakini mimi ninaamini kuwa CHADEMA ipo juu ya siasa, inaangalia zaidi maslahi ya taifa hili.

“Nikiwa mjumbe wa kamati hii nina uhakika nitakuwa huru kutoa maoni yangu. Nimekuwa uhuru kutoa maoni yangu ndani ya Bunge na ndivyo nitakavyokuwa huru kutoa maoni yangu kwenye kamati hii ya madini.”

Zitto anasema kwamba amekuwa akiungwa mkono na viongozi wa chama chake, akiwamo muasisi wa CHADEMA na mwanasiasa wa siku nyingi, Mzee Edwin Mtei, wananchi na viongozi wa Kigoma, ingawa hana uhakika na msimamo wa mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Bob Makani.

Hata hivyo, anasema kwamba chama chake bado hakijatoa kauli rasmi, kupitia vikao vyake, kuhusu uteuzi wake huo, licha ya kuwapo kwa kauli za kuungwa mkono kutoka kwa viongozi wake. Zitto anasema kwamba kabla ya uteuzi huo wa Rais Kikwete, hakuwa na mawasiliano yoyote naye na wala hakuarifiwa mapema.

“Mimi sijazungumza lolote na Rais Kikwete na sitaki kujiingiza kuwa nilishaurika kuwa mjumbe wa kamati hiyo. Sitaki kulifanya suala hilo kuwa ni la kisiasa.”

Kama ulikuwa hujui maana ya neno “machachari” si ajabu katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita umeijua.

Vyombo vingi vya habari nchini Tanzania vimekuwa vikitumia neno hilo kumuelezea mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kutokana na yaliyojiri bungeni hivi karibuni.

Akiwa na umri wa miaka 29 tu (hivi sasa ana miaka 30) Zitto Zuberi Kabwe, aliingia bungeni na kuwa mbunge mdogo kupita wote wa kuchaguliwa. Aliingia bungeni baada ya kupata dhamana ya asilimia 51 ya wapiga kura wa jimbo lake la Kigoma Kaskazini kwa kupitia CHADEMA.

Hivi karibuni mbunge huyu kijana zaidi alisimamishwa kuhudhuria vikao vya bunge mpaka hapo Januari mwakani. Kufuatia kitendo hicho, jina la Zitto Kabwe pengine ndilo ambalo limekuwa likitajwa miongoni mwa Watanzania wengi kupita jina lingine lolote kwa wakati huu.

Kuhusu kuingia kwake katika siasa, Zitto anasema: “Mimi nilizaliwa mwanasiasa. Siasa ipo kwenye damu yangu. Nimekuwa nikijihusisha na nyadhifa za kisiasa tangu nikiwa shule ya msingi.

“Nilipoamua kujiunga na chama cha siasa cha upinzani, nilishawishiwa zaidi na ukweli kuwa Tanzania inahitaji upinzani imara ili kufuatilia utendaji wa chama tawala. “Nilijiunga na CHADEMA nikiwa na umri wa miaka 16 tu, na nimebakia katika chama hiocho tangu wakati huo.

Kuhusu mwanasiasa ambaye anapenda kuiga mambo yake, Zitto anasema: “Nimekuwa nikimpenda na ninaendelea kumpenda kutokana na mwenendo wake. Nimekuwa nikimwona mtu aliyelelewa vizuri kisiasa. Ingawa ni Rais wa Tanzania, ambaye hakujaliwa kupata wadhifa huo, afanya kazi nzuri kipindi cha mpito kutoka Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) kwenda Muungano wa Afrika (AU).

Kuhusu kama hivi leo asingekuwa mbunge, Zitto anasema: “Kwa vyovyote vile ningekuwa mhadhiri, mtafiti na mwandishi. Nitafanya hayo iwapo nitaondoka kwenye siasa. Ninapenda sana kufundisha.

Kuhusu siasa kuwa ni suala la kifamilia kama ilivyo kwa familia, Zitto anasema: “Jambo hilo lina ukweli. Mama yangu ni mwasiasa katika Manispaa ya Kigoma. Babu yangu alizaliwa katika ukoo wa kichifu. Hata hivyo, kwangu mimi siasa ni matokeo ya kusoma kwingi na kujihusisha na masuala ya kijamii.

Kuhusu uzoefu katika siasa, Mbunge huyo anasema:”Uzoefu ni muhimu ingawa sharti la kutosheleza kuwa kiongozi bora. Kama nilivyosema tangu mwanzo kuwa nilianza kwa kuwa kaka wa shule ya msingi, na hata katika ngazi ya chuo kikuu nilikuwa kiongozi wa wanafunzi.

“Uzoefu ambao niliupata katika uongozi wangu chuo kikuu ulikuwa mkubwa sana. Umenisaidia kuyakabili mambo kwa ubora zaidi. Migomo na migogoro ya wanafunzi iliimarisha uwezo wangu wa kuongoza na kushughulikia migogoro.

Kuhusu malengo yake ya kisiasa, anasema: “Kusema ukweli, kumekuwa na mabadiliko katika msafara wangu wa kisiasa. Nilipokuwa mbunge, malengo yangu yalikuwa kwa ajili ya jimbo langu la Kigoma Kaskazini.

Lakini nilipoingia katika Bunge, nilijikuta nilikilazimika kuzungumzia masuala ya kitaifa kuliko yale ya jimbo langu pekee. Kwa hiyo, nayaona masuala kwa upana zaidi sasa.

Juu ya kuingia kwake katika upinzani anasema: “Nilishawishika zaidi na kiu ya kuona serikali ikiwajibika. Na jambo hilo linawezeka kupitia mfumo wa vyama vingi.

“ Kisheria katika Tanzania tuna mfumo wa vyama vingi, lakini katika hali halisi kuna chama kimoja kinachotawala kila kitu, yaani CCM, ambayo inashika hatamu zote za dola.

“Ni lengo langu kuona kwamba mfumo huo unatoweka hapa nchini. Ninataka kuhamasisha Watanzania wauzike mfumo huu, na baadaye kuhakikisha kodi ina thamani kwa maendeleo ya watu.

“Ninayo njozi kwamba kufikia Novemba 2010, wabunge wa upinzani watafikia asilimia siyo chini ya 40.

Mara baada ya kujiunga na CHADEMA, Zitto alianza na wadhifa wa ofisa wa siasa wa chama. Baadaye akawa Ofisa wa Mambo ya Nje na kisha kuwa Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa. Hivi sasa ni Naibu Katibu Mkuu.

“Ninamwona Freeman Mbowe kuwa mtu muhimu kwangu. Aliniona nikiwa chuo kikuu, akanishawishi niweze kukiunga mkono chama. Anao uwezo, visheni na ujasiri wa kukiongoza chama. Kwa hakika, alinilea kuwa kiongozi.”

Mpaka sasa ni mbunge kivuli wa uchumi Mwanasiasa huyo hupendelea kusikiliza muziki, kufanya matembezi na kusoma.

Zitto anasema kwamba ifikapo Januari mwakani atakuwa ameandika vitabu vitatu, kimoja kikihusu ni kwa nini na jinsi gani alishinda uchaguzi Kigoma Kaskazini, kingine kikihusu maisha ya Marehemu Amina Chifupa na cha tatu ni Siasa ndani ya Bungte la Tanzania. “Vitabu viwili vya mwanzo viko katika hatua ya mwisho, na hiki cha tatu nishakusanya nyaraka zote muhimu.

“Kabla ya 2010 nimepanga kuandika kitabu kuhusu ni nani hasa ana ushawishi katika siasa za Tanzania. Ninataka kuweka wazi ‘Utatu Mtakatifu wa Siasa za Tanzania.’ Nitakiandika kitabu hicho kwa kushirikiana na waandishi wa habari wa hapa nchini.

“Tayari nimewaarifu wenzangu kuanza kufanya utafiti. Mradi wa kitabu hiki, ukifanikiwa, basi utakuwa kivutio kikubwa. Zitto Kabwe anasema hana kiu yoyote ya urais na kwamba hatagombea ubunge mwaka 2010. “Ninataka kuwa sehemu ya timu ya kukampeni ili wapinzani wapate wabunge wengi.

“Katika miaka 10 ijayo nitakuwa nikifundisha katika moja ya vyuo vikuu hapa nchini. Ninashinikizwa sana kugombea ubunge tena mwaka 2010, lakini sidhani kwamba nitabadili mawazo yangu ya kutogombea. Hebu tusubiri na tuone.

Zitto alipata elimu yake katika shule ya msingi Kigoma, na baadaye akapata elimu yake ya sekondari katika shule za sekondari za Kigoma, Kibohehe, Galanos na Tosamaganga, kabla ya kujiunga na elimu ya juu hapa nchini na Ujerumani.

Kutoka Raia Mwema wiki hii.

No comments: