Sunday, December 23, 2007

Athuman Machupa, aitwa majaribio Norway

Na Clara Alphonce

KLABU ya Simba ipo katika mazingira ya kumkosa mshambuliaji wake Athuman Machupa aliyesajiliwa hivi karibuni kwa ajili ya kuichezea timu hiyo kwenye nichuano ya Ligi Kuu ya Vodacom na mashindano ya Klabu Bingwa Afrika, baada ya kupata nafasi ya kufanya majaribio katika klabu ya Molde FC ya Norway.

Wakala wa FIFA, Mehd Rhemtullah alisema jana kuwa Machupa ni miongoni mwa wachezaji watano waliopata nafasi hiyo ya kujaribu bahati yao ya kucheza soka la kulipwa nchini Norway.

Rhemtullah aliwataja wachezaji wengine kuwa ni; Suleiman Ndikumana wa Inter FC ya Burundi na mchezaji mmoja wa Uganda ambaye hakutamtaja jina lake.

Alisema kuwa, wachezaji hao waliweza kugundulika uwezo wao kutokana na ushiriki wao katika mashindano ya Chalenji, wakati Machupa na Majaliwa wao walionekana kufaa majaribio baada ya kutazamwa kupitia mikanda ya video.

Wachezaji wengine ni; Yonathan Ngwitou wa Red Sea ya Eritrea na Haruni Nzoyimana wa APR ya Rwanda, ambao wanatakwenda kufanya majaribio katika klabu ya Vålerenga ya Norway.

Alisema kuwa klabu hizo zote zinashiriki ligi kuu ya Norway na Vålerenga ni moja ya timu zilizoshiriki mashindano ya UEFA.

Kwa mujibu wa Rhemtullah, uteuzi wa wachezaji hao umefanywa kwa kushirikiana na Azzedine Saoud ambaye ni meneja wa masoko wa kampuni ya uwakala ya Gran Canaria Football Center inayotambuliwa na Shirikisho la soka la Dunia, FIFA.

Alisema kuwa, Saoud anatambulika na FIFA kutokana na kuandaa programu mbalimbali za mazoezi wakati wa majira ya joto na baridi katika kisiwa cha Grand Canary huko Ulaya.

Klabu kutoka nchi za Ujerumani, Finland, Norway, Denmark, Sweden na Uholanzi zimekwishafanya programu na Saoud na ndiye atakuwa mfuatiliaji wa karibu maendeleo ya wachezaji hao wakiwa nje ya nchi.

Wachezaji hao kwa mujibu wa taarifa za wakala huyo wataondoka nchini Januari 20, 2008 na kuanza majaribio hayo mara moja na kisha kurejea mwezi Februari mwakani.

"Pia kuna nafasi kwa Eric Majaliwa na Henry Joseph wa Simba, hata hivyo, wachezaji hao bado sijafanya mazungumzo na viongozi wao ili kuona wanakwenda kufanya mazoezi timu gani," alisema Rhemtullah.


"Links" na http://watanzaniaoslo.blogspot.com

No comments: