MAJUMA mawili yaliyopita nilikuwa naendeleza mjadala kuhusu chanzo cha matatizo yetu sisi Waafrika. Na ni vyema nikaongeza neno “sisi Waafrika weusi” kwa sababu litakuwa na mantiki katika maswali nitakayojaribu kuyauliza huko mbele.
Nilisema leo hii tunaishi maisha ambayo tukiletewa chochote kigeni tunakipokea na kukitukuza. Tunalamba miguu na nyayo za wageni.
Tunaishi kwa sera zao, tamaduni zao, mila zao, imani zao, lugha zao, majina yao na vitu vitu vyao. Hatujui chetu ni kipi. Tumeacha vya kwetu vya msingi.
Na bado inasumbua kidogo unaposikia watu wakisema kwa ujumla tu kwamba tabia fulani si maadili yetu; jambo fulani ni kinyume na utamaduni wetu. Ukiwauliza utamaduni wetu akina nani ? Wanasema: “sisi Waafrika.” Ukiwauliza: “Utamaduni wa Waafrika kwa maana ya mipaka ya bara; rangi; kabila; dini; mfumo wa maisha au kitu gani?” Hapo mnaanza kutafutana.
Nilisema katika makala za mwanzo kwamba kumbukumbu za historia zinaonyesha kwamba katika karne ya 7 na 8 tayari watu kutoka bara la Asia walikwishafika katika pwani ya Afrika Mashariki.
Watu hawa walikuja na majahazi yao na vitu vidogo vidogo kuona kama wangeweza kufanya biashara. Lakini walipowakuta babu zetu weusi waliwatazama kwa haraka haraka na kuhitimisha kwamba wale hawakuwa binadamu kamili.
Vipo vitu vitatu vilifanyika kuhalalisha hitimisho kwamba watu weusi hawakuwa binadamu kamili. Kwanza ilibidi wafundishwe mila na utamaduni mpya. Ilibidi sasa Waafrika waachishwe tabia zao ambazo zilionekana ni za kishenzi. Tabia hizo ilikuwa ni pamoja na utaratibu wao wa maisha wa kila siku; mahusiano kati ya wanaume na wanawake; majina waliyoita watoto wao na hata jinsi walivyokuwa wakivaa.
Kwa mujibu wa nyaraka za historia, Waarabu wa kwanza kufika pwani ya Afrika hawakuja kuhubiri dini.
Walikuja kufanya biashara. Ndiyo maana walipoanza tu biashara ya kusafirisha watumwa walizua vita na watu weusi.
Inasemekana kwamba watu weusi walizidiwa nguvu kwa sababu ya kuwa na silaha hafifu. Wapo wachambuzi ambao wanaamini sababu hii ni dhaifu.
Wanaamini kwamba hakuna silaha kubwa kama dhamira. Wanasema dhamira ni silaha kubwa kupita vifaru, mizinga bomu la nyuklia. Sababu inayotolewa ya kushindwa kwa watu weusi ni kwamba walikwishachotwa kisaikolojia. Walipoiona mashua kwa mara ya kwanza waliisogelea wakiishangaa.
Walipomuona Mwarabu akishuka mle, walimtizama wakimshangaa. Alipowapatia shanga na kanga walibaki wanashangaa.
Alipogundua tu kwamba ni watu wa kushangaa, akaamini walikuwa duni na kwamba angeweza kuwabadili kuwa kama alivyotaka.
Kitu cha pili, Waafrika walipewa mafundisho ya imani mpya, tofauti kabisa. Wakazikana njia zao zote na ibada za “kishenzi” huku wakimpokea Mungu mpya. Wakajifunza njia mpya za kuwasiliana na Mungu mpya na wakamtukana kabisa yule waliyemjua siku zote za maisha yao.
Katika kufanya hivyo wakaamini kabisa kwamba jinsi walivyojitahidi kutaka kushabihiana na wageni waliowaletea imani mpya basi ndivyo walivyojiweka jirani na Mungu mpya. Hata hivyo bado wakaendelea kuona kwamba muonekano wao (watu weusi) ulikuwa ni mzigo.
Kitu cha tatu, Waafrika walipewa majukumu ya kudumu. Yapo mambo ambayo ilibidi yafanywe na Waafrika weusi tu.
Zipo kazi ambazo zilionekana za ovyo zaidi ilibidi zifanywe na Mwafrika mweusi tu. Nilipata kusoma mahala kwamba wakati wa utumwa watumwa wenye rangi nyeupe zaidi waliweza “kupandishwa cheo” na kufanya kazi za maana kidogo kama kumnawisha mikono bwana mkubwa au kumpikia chai mama.
Ikatokea kwamba watumwa wakawa wanatamani kuwa weupe ilhali wasijue la kufanya. Kwa kweli hakuna sababu ya kuwashangaa watu weusi wanaotumia mkorogo hapa kwetu hii leo. Yawezekana wengi wao hawajui sababu.
Lakini huu ni urithi wa dhamira ile ya wakati wa utumwa; dhamira ya kuikimbia ngozi nyeusi kwa sababu tu mtu mweusi alionekana duni. Weusi ulikuwa nuksi.
Hata walipokuja wavamizi wa Kireno na wengineo kutoka Ulaya hali ilikuwa hivyo hivyo. Hapo awali nilieleza jinsi baadhi ya waliojiita wagunduzi walivyokuwa wakiwaelezea Waafrika weusi. Nikatoa mfano wa mmoja wao aliyeandika hivi: “…Wengine (watu weusi) hawana pua wala matundu ya kupumulia; Wengine hawana midomo ya juu; wengine hawana ulimi wanaongea kwa ishara; na wana kitundu kimoja usoni cha kupumulia na ambacho pia hukitumia kunywea maji; … Wapo pia Waanthropomphagi ambao huishi kwa kula nyama ya binadamu; Wengine wanaitwa Wagamphasante na hutembea uchi kama wanyama.
Wapo pia wacinamolgi ambao vichwa vyao ni kama vya mbwa vile; wapo pia Wablemys ambao wao hawana vichwa kabisa, ila macho na midomo vipo kifuani. Wapo pia waswahili ambao hutembea kwa kutumia mikono na miguu kwa pamoja…”
Kama tulivyoona katika makala zilizopita jinsi watu weusi walivyoonekana machoni pa wageni wa Kiarabu ndivyo pia walivyoonekana mbele ya wageni wa kizungu.
Na bahati mbaya, kama nilivyosema katika makala zilizopita, picha ile waliyoiona wavamizi wale karne kadhaa zilizopita bado ipo na huonekana katika vituo vya televisheni za nchi zilizoendelea.
Lengo la mjadala huu si kuwalaani Waarabu au Wazungu, la hasha. Hawa wana mchango wao mzuri tu katika maeneo mbalimbali ya maendeleo ya dunia.
Lengo ni kuijadili historia ya Mwafrika mweusi na kuona ni jinsi gani unyonge wake mwenyewe na tabia yake ya kujikana na kupenda vijizawadi kutoka ng’ambo (kama vile shanga, kioo cha kujitizama, mvinyo wa kwenye chupa, nguo za kutoka Ulaya na vitu vingine vya urembo) vilivyochangia na vinavyoendelea kuchangia katika madhila anayoyapata hapa duniani.
Wiki ijayo tunaendelea na mjadala wa matatizo ya Waafrika.
ayubrioba@hotmail.comKutoka Raia Mwema wiki hii.
No comments:
Post a Comment