Evarist Chahali, Uskochi.
HISTORIA huwa haibagui kati ya matukio mazuri na mabaya au binadamu waliofanya mambo mazuri na wale waliofanya mabaya. Matukio mazuri ya kihistoria kama vile nchi yetu kupata uhuru mwaka 1961 na kukomeshwa kwa siasa za ubaguzi huko Afrika Kusini yaliingia kwenye vitabu vya historia.
Vivyo hivyo kwa matukio mabaya kama ya unyama wa manazi na mafashisti wakati wa vita kuu za dunia na ukatili wa Osama bin Laden na washirika wake katika mlolongo wa mashambulizi ya kigaidi hususan lile la Septemba 11 mwaka 2001.
Historia pia haijafanya ubaguzi kwa waliobadili historia ulimwenguni kama vile Yesu Kristo na Mtume Muhammad (SWA) au hata Mwalimu Nyerere, lakini pia “imewapa shavu” viumbe waovu kama vile Osama, Hitler na Musollini kwa kuwajumuisha katika kumbukumbu za kihistoria.
Pamoja na ukweli kwamba mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001 huko Marekani sio ya kwanza katika historia ya matukio ya aina hiyo duniani, matokeo yake yaliibadili dunia kwa kiwango kikubwa sana.Wamarekani wanakiri kwamba Osama na kundi lake wamefanikiwa kuibadili nchi yao kwani tangu wakati huo kumekuwa na mlolongo wa hatua za kuhakikisha kuwa balaa hilo halitokei tena.
Eneo moja ambalo limeathiriwa zaidi ni uhuru wa raia ambapo licha ya malalamiko ya asasi zinazotetea uhuru wa raia, mamlaka za usalama zimekuwa zikisisisitiza kwamba sheria zinazoimarisha amani na usalama zinapaswa kupewa kipaumbele zaidi, hata kama kwa kufanya hivyo itamaanisha kuminya uhuru wa raia.
Usumbufu kwenye viwanja vya ndege unaosababishwa na upekuzi wa kina, kunaswa maongezi ya simu za binafsi na hatua nyingine za kibabe kama hizo zinazoingilia uhuru wa mtu binafsi, yamekuwa ni mambo ya kawaida katika maisha ya kila siku ya Wamarekani.
Wanaounga mkono hatua hizo wanadai kwamba zimesaidia kutotokea kwa mashambulizi mengine kama yale ya mwaka 2001, lakini wapinzani wanadai kwamba kwa kuchukua hatua kama zile zinazominya uhuru wa raia ni sawa na kuwapatia ushindi magaidi kwani miongoni mwa malengo ya mashambulizi ya kigaidi ni kubadili utaratibu wa maisha ya kila siku ya raia katika nchi wanayoilenga (magaidi hao).
Kama ilivyotokea sehemu nyingine duniani, Uingereza nayo ilijikuta ikilazimika kuimarisha hatua za kiusalama baada ya mashambulizi hayo ya kigaidi huko Marekani.
Lakini mabadiliko makubwa zaidi yalikuja baada ya matukio ya kigaidi kwenye mfumo wa usafiri wa chini ya ardhi jijini London Julai 7 mwaka juzi. Tofauti na ilivyokuwa Marekani,Waingereza wengi wameonekana kutoafikiana na dhamira ya serikali kuminya haki na uhuru wa raia kwa kisingizio cha kudhibiti ugaidi.
Pengine tofauti hii inachangiwa zaidi na ukweli kwamba wakati Marekani inaelekea kuwa nchi ya kihafidhina zaidi hasa baada ya kukua kwa matishio ya ugaidi, Uingereza imeendelea kubaki kuwa nchi ya kiliberali zaidi ambapo asasi za kutetea haki na uhuru wa kiraia bado zina nafasi kubwa katika maisha ya kila siku nchini hapa.
Hata hivyo, hatua kadhaa zimeendelea kuchukuliwa na kupendekezwa katika jitihada za kuwadhibiti magaidi. Kabla ya kuandaa makala hii,Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, Jacqui Smith alionekana kwenye luninga akitoa tahadhari kwamba kuna uwezekano wa mashambulizi ya kigaidi katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu ya Krismasi.
Pia hivi karibuni kulikuwa na taarifa kwamba wasafiri wa treni hapa Uingereza watarajie taratibu za kiusalama kama zile wanazokumbana nazo wasafiri wa ndege. Kwa mujibu wa habari hizo, wasafiri wa treni watalazimika kujibu maswali takriban 50 ya kiusalama na kupekuliwa kwa kama kwenye viwanja vya ndege. Serikali inajitetea kwamba japo inatambua kwamba hatua kama hizo zitasababisha usumbufu kwa wasafiri, lakini inachukua hatua hizo kwa ajili ya kuwalinda raia wake.
Uzuri mmoja wa mikakati wanayojipangia hawa wenzetu ni kwamba inafuatiliwa. Hii sio mikakati inayoishia kwenye semina elekezi, makongamano au warsha, bali ni mikakati ya muda mrefu ambayo pindi mtendaji akizembea katika utekelezaji, basi, anamwaga unga na pengine kuishia gerezani.
Nimesoma habari fulani kwenye gazeti moja la huko nyumbani kwamba TAKUKURU inakuja na teknolojia ya vyombo maalumu vya kuwanasa wale wanaodai rushwa ya ngono kwa akinamama. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk. Edward Hosea, vyombo hivyo vina uwezo wa kunasa sauti na kuchukua picha ya wakware wanaoomba rushwa ya ngono,na aliwataka akinamama kutoa ushirikiano kwa kuwasiliana na TAKUKURU ili wakabidhiwe vidude hivyo pindi wanapooona dalili za kubughudhiwa na wakware hao.
Kama mkereketwa wa teknolojia mpya, napenda kuipongeza taasisi hiyo kwa kuja na mkakati huo. Pengine hizi ni dalili za mwanzo za matunda ya udaktari wa falsafa katika rushwa aliohitimu Dk. Hosea.
Niliposikia kiongozi huyo amehitimu kwa ngazi ya juu kabisa katika taaluma inayohusiana moja kwa moja na eneo lake la kazi, nilijikuta nikimlinganisha na kamanda wa majeshi ya Marekani huko Irak, Jenerali David Petraeus, ambaye pamoja na sifa nyingine za kijeshi alizonazo, mada ya utafiti wa PhD yake -“Jeshi la Marekani na Mafunzo yaliyotokana na vita ya Vietnam”, iliwaaminisha wengi kuwa ndiye mtu sahihi wa kuleta mafanikio katika vita inayoendelea huko Iraki.
Yangu macho, lakini pengine shahada ya uzamivu ya Dk. Hosea inaweza kubadili mwelekeo katika mapambano dhidi ya rushwa huko nyumbani.
Hata hivyo, historia inaweza kutoa hukumu ya mapema kwenye mkakati huo wa “vinasa sauti na picha za wanaodai rushwa ya ngono”. Teknolojia ya vidhibiti mwendo, maarufu kama spidi gavana, ilitarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani lakini lililo dhahiri ni kwamba mkakati huo ulioleta matumaini uliishia kuwa ndoto ya alinacha.
Mitaani wanaita “kumwagiana mchanga wa macho”, yaani kuja na mawazo mazuri yanayotarajiwa kuleta ufumbuzi wa tatizo fulani, lakini mwishowe inaishia kuwa ni hadithi tu (na pengine inamaanisha fulani keshaongeza kipato kwenye akaunti yake).
Kweli tunahitaji teknolojia katika kupambana na rushwa lakini ni vigumu kufanikiwa pasipo uzalendo na uchungu wa dhati kwa nchi yetu. Kama waliochangia kuharibu spidi gavana ni watu walewale waliotarajiwa kusimamia ufanisi wake, sintoshangaa vidude hivyo vya TAKUKURU vya kuwanasa wakware vikaishia kufanyiwa “usanii” na hao wenye majukumu ya kuhakikisha vinadhibiti kweli rushwa ya ngono.
Nadhani tatizo letu kubwa haliko kwenye mikakati bali utekelezaji wa mikakati hiyo. Nilizaliwa Desemba 9 miaka 30 na kitu iliyopita, na kila tunapoadhimisha siku ya Uhuru na Jamhuri huwa ninajaribu kutathimini maendeleo yangu binafsi na ya Taifa langu kwa ujumla.
Basi wakati tunaelekea kwenye maadhimisho ya siku hiyo, yatupasa kukumbushana kwamba njia nafuu na nyepesi ya kutatua matatizo mbalimbali yanayolikabili nchi yetu, ikiwa ni pamoja na rushwa, ni kuweka mbele maslahi ya Taifa letu badala ya maslahi binafsi.
Taifa letu “changa” linapotimiza miaka 46 lina kila sababu ya kutuuliza kwa nini tuko hapa tulipo na sio mbele zaidi ilhali tuna kila nyenzo muhimu ya kujiletea maendeleo yetu (sio ya takwimu) wenyewe.
Hepi bethdei Tanzania!
Barua-pepe: epgc2@yahoo.co.ukKutoka Raia Mwema wiki hii.
No comments:
Post a Comment