Vigogo wawatisha
mashahidi kashfa BoT
WAKUU wa Serikali na vigogo ndani ya Chama Cha Mapinduzi wanahaha kutokana na kashfa nzito ya wizi wa mabilioni Benki Kuu (BoT), na sasa wanafanya kila liwezekanalo ili kuwakinga baadhi ya watuhumiwa wa moja kwa moja wasianikwe hadharani, Raia Mwema imeambiwa.
Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba kama yote yatakuwa yamesemwa na kuwekwa hadharani, kuhusu nani wamehusika, basi sura za vigogo kadhaa serikalini na ndani ya CCM zitakosa pa kujificha.
“Sasa kuna shinikizo kwamba watakaokwenda kuhojiwa na tume ya Rais wasitaje baadhi ya majina yaliyohusika katika kashfa hii, majina ambayo yanajitokeza mara kwa mara katika kushiriki wizi huu mkubwa ndani ya BoT,” mmoja wa wanachama wakongwe wa CCM ameiambia Raia Mwema.
Lakini kwa mujibu wa ofisa huyo, suala hilo limeleta mgawanyiko mkubwa ndani ya chama chenyewe, huku baadhi wakisema wahusika wawajibike kwa madhambi yao kama yatadhihirika mbele ya vyombo vya sheria ili chama kisije kuathirika.
“ Hilo ni suala ambalo linaendelea ndani ya CCM sasa, tena mpaka hata katika ngazi za juu kabisa za Kamati Kuu, ambako kuna wanaotaka mtu aliyehusika awajibike na wengine ambao wanataka mambo haya yazimwe,” anaongeza ofisa huyo.
Raia Mwema imefahamishwa pia kwamba baadhi ya watu, watuhumiwa na wasio watuhumiwa katika wizi huo, wamekuwa wakitafadhalishwa wasitaje jina la kigogo mmoja ndani ya CCM ambaye kwa kupitia kampuni ya kughushi, alishiriki kikamilifu kuchota mabilioni ya fedha ambazo sasa inaaminika ziliingia katika kampeni za uchaguzi wa mwaka 2005.
“Hata kabla ya baadhi yao kuitwa mbele ya Kamati aliyoiunda Rais Jakaya Kikwete kuchunguza wizi huo wa BoT, wamekuwa wakipelekewa ujumbe mahsusi kwamba watakapokuwa mbele ya Kamati, wasitaje jina la kigogo huyo.
“Wameelezwa wataje majina ya wafanyabiashara wawili wenye asili ya Asia ili ionekane kwamba hawa ndio pekee waliochota fedha hizo. Na wanaambiwa kwamba wafanyabiashara hao kwa sasa wako tayari kuchukua mzigo huo badala ya kigogo huyo.
“Mmoja kati ya wafanyabiashara hao wanaotajwa kuchukua mzigo wa kigogo huyo ni Jeetu Patel, mwenye kumiliki kampuni tisa ambazo zimetajwa wazi katika wizi huo na ambaye tangu suala hili litangazwe na Serikali yuko nje ya nchi,” anasema ofisa huyo akiongeza kwamba mwingine ni mfanyabiashara wa Dar es Salaam ambaye yuko karibu na CCM na ambaye mara kadha amejitosa kutaka kuwa mgombea ubunge.
Vyanzo mbalimbali vya habari vinaeleza kwamba wingu kubwa limetanda kuhusiana na utendaji wa Kamati ya Rais Kikwete inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu Johnson Mwanyika na kufanya baadhi ya watu wajiulize iwapo kweli ukweli wa kashafa hiyo utakuja kufahamika katika mazingira ambayo dola inashiriki kutaka kuficha ukweli kuhusu wahusika wakuu.
Baadhi ya wachunguzi wa masuala nyeti kama haya wameiambia Raia Mwema kwamba hakuna cho chote ambacho Serikali na CCM wanaweza kukiokoa kwa kuweka shinikizo ili baadhi ya wahusika wasitajwe katika uchunguzi.
“Wanachofanya ni kuahirisha tu tatizo. Kesi kubwa katika suala hili si wingi wa fedha hizi na wala si nani alihusika, bali tatizo ni kwamba hawa watu walighushi nyaraka. Kwa vyovyote vile kughushi nyaraka ni kosa zito na upelelezi ukifanyika sawasawa, hatimaye hao ambao wanataka kusafishwa sasa watajikuta wakitajwa na kusutwa na nyaraka.
“Kama kweli kuna utashi serikalini, kama ambavyo Rais Kikwete alijaribu kuonyesha wakati wa kutangazwa kwa hatua dhidi ya wizi ndani ya BoT, basi hakuna namna ila kuliacha suala hili liishe bila Serikali wala CCM kuingilia ili hatimaye wahusika wapatikane,” anasema mtoa habari wetu.
Raia Mwema imeambiwa pia kwamba jitihada hizo zinazoendelea zimeigusa pia familia ya aliyekuwa gavana Dk. Daudi Ballali ambayo imepelekewa ujumbe kuwaomba wamwambie Dk. Ballali anyamaze.
“Wamekwenda mara mbili na mara zote wamefikisha ujumbe kwamba wanataka wawasiliane na ndugu yao (Dk. Ballali) Marekani ili afunge mdomo wake. Nimeambiwa kwamba familia imechanganyikiwa.
“Wao kama wanafamilia hoja sasa ni kaka yao apone, lakini mara wanapelekewa ujumbe kwamba dola haitaki azungumzie kokote suala hilo la BoT. Hawaelewi maana ya yote haya ni nini. Na tukumbuke kwamba hawa ni Watanzania tu wa kawaida, ujumbe kama huo lazima utawachanganya,” anasema mtoa habari huyo.
Bado Dk. Ballali hajaweza kusema lolote, lakini taarifa za waliokuwa karibu naye zinasema kwa jinsi anavyohisi amechafuliwa, wakati ukifika atasema ili asafishe jina lake.
“Huko aliko anasononeka. Haohao ndio waliokuwa wakimshinikiza alipe yale mabilioni. Na hata alipojaribu kubisha ili taratibu za malipo zifuatwe aliambiwa alipe. Sasa wamekwisha kumtumia hata hawazungumzii afya yake ambayo si nzuri. Wanataka ikiwezekana anyamaze moja kwa moja,” anasema mmoja wa watu wa karibu na Dk. Ballali ambaye, kutokana na sababu zinazoeleweka, ameomba asitajwe.
Kwa sasa Dk. Ballali anaelezwa kuwa nchini Marekani na bado ana nia ya kurudi Tanzania pamoja na kuwa siku hasa haijulikani hasa kwa kuwa Serikali ya Marekani imetangaza kumfutia viza yake.
Ubalozi wa Marekani nchini, wiki hii umetoa taarifa ukijivua kuwajibika kumrejesha nchini Dk. Ballali kwa maelezo kwamba jukumu hilo kwa sasa ni la Serikali ya Tanzania.
Lakini baada ya viongozi wote wa juu wa CCM kukanusha hadharani kuhusika kwa chama hicho tawala, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, amesema kwamba CCM haihusiki moja kwa moja katika sakata la BoT pamoja na kwamba upo uwezekano wa watu binafsi ndani ya CCM kuhusika.
Kutoka Dodoma inaelezwa kwamba Wabunge wameitaka serikali kuwasilisha bungeni ripoti kamili ya ukaguzi wa BoT, hiyo ikiwa baada ya Waziri wa Fedha, Zakia Meghji kuwasilisha bungeni taarifa ya kuelezea hatua za serikali kuhusu ukaguzi huo.
Hata hivyo Spika Sitta amewaeleza wabunge kwamba ofisi yake imekua na mawasiliano na serikali kuhusu suala hilo.
Wakati hayo yakiendelea, gazeti la The Citizen la Jumamosi, Januari 26, 2008 liliandika kuhusika kwa watu wazito ndani ya serikali na likieleza majina ya kampuni za Excellent Services Limited na Clyton Marketing Limited bila kutaja majina ya wakurugenzi wake.
Hata hivyo, vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na gazeti la serikali la Kiswahili la Habari Leo lilitaja wakurugenzi wa kampuni hizo na kuainisha jinsi zilivyosajiliwa na kupanda kwa mtaji wake.
Kwa mujibu wa habari hizo ambazo zimethibitishwa na Msajili wa Makampuni (BRELA), wakurugenzi wa Excellent Services yenye makao yake Sokoine Drive, Namba 11649, waliomo ni pamoja na Emmily Samanya, Peter Sabas, Levis Msiko, Elisifa Ngowi na Massimo Faneli, ilipoanzishwa 2004 kwa mtaji wa Sh 500,000/- kabla ya mtaji kuoanda hadi kufikia milioni 50 mwaka 2005.
Kumbukumbu za BRELA na magazeti zimewataja wakurugenzi wa Clyton Marketing Limited, iliyosajiliwa Juni 6, 2005 kuwa ni pamoja na Edwin Mtoi na Elisifa Ngowi. Anuani ya kampuni hiyo ni Plot Namba 707, Mkwepu Dar es Salaam.
“Mmoja kati ya wakurugenzi katika makampuni hayo mawili (anamtaja jina) anatajwa kuwa mkurugenzi mwandamizi na mwenye nguvu katika Idara ya Usalama wa Taifa na amekuwa humo kwa muda mrefu akiwa karibu sana na Mkurugenzi Mkuu aliyestaafu, Cornel Apson,” anaeleza ofisa mwandamizi serikalini na kuendelea:
“...(anamtaja jina) amekua katika kitengo kinachofanya kazi ya kupambana na uhalifu ikiwamo ugaidi, rushwa, biashara ya fedha haramu na uhalifu mwingine wa kimataifa, jukumu linalomsogeza karibu zaidi na kamati iliyoundwa na Rais kuchunguza sakata la BoT.”
Wakati hayo yakiendelea, kamati hiyo imekwisha kuanza kuwahoji kwa kina wamiliki wa makampuni 22 yanayotajwa katika sakata la BoT huku ikielezwa kwamba nyaraka zote za makampuni hayo zimechukuliwa kutoka BRELA.
Kwa mujibu wa habari hizo nyaraka hizo hasa baada ya kupatikana kwa makampuni yaliyodaiwa kutosajiliwa zimechukuliwa na kamati iliyoundwa na Rais na hakuna mwenye nafasi ya kusoma majalada hayo kwa sasa.
Makampuni ambayo nyaraka zake zilikosekana ni pamoja na G&T International Limited, ambayo imefahamika kumilikiwa na Octavio Timoth na Beredy Malegesi, ambaye anaelezwa kuwa shahidi muhimu katika sakata hilo na huenda “akazibwa mdomo,” kwa mujibu wa vyanzo vya habari ndani ya serikali.
Kampuni nyingine ambayo nyaraka zake zimeonekana ni Changanyikeni Residential Complex Limited inayomilikiwa na Jose Vander Merwe, Samson Mapunda na Charles Mabina ikiwa na makao yake, Sinza, Kumekucha, Dar es Salaam.
Sakata la BoT, linaiweka CCM katika mtego mkubwa kutokana na kuhusishwa kwake moja kwa moja na matumizi ya fedha hizo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, lakini viongozi wake wamekanusha madai hayo.
Sasa inafahamika kwamba sehemu kubwa ya fedha ikiwamo zile zilizotokana na kampuni iliyoghushi nyaraka ya Kagoda Agricultural Limited (KAL) iliyochota Sh bilioni 40/- ziliingia katika uchaguzi huo kupitia wana CCM maarufu waliokua katika harakati za kampeni ya Jakaya Kikwete.
Fedha hizo na nyingine ziligawiwa kwa baadhi ya wabunge kwa viwango vilivyotofautiana, na nyingine zilipotea ama kuibwa kutokana na kutokuwapo utaratibu rasmi wa udhibiti na uhakiki wa fedha kitaalamu.
Kwa ujumla sakata zima limemuelemea Dk Ballali ambaye pamoja na kuhusika kwake, ana siri nzito inayoweza kuibua kashfa ya aina yake katika historia ya siasa za Tanzania kama si ya kimataifa.
Pamoja na maelezo kwamba Dk. Ballali alifanya malipo yenye utata kutokana na wakuu wake wa kisiasa kushinikiza, sakata hiyi nzima iliwahusisha watendaji wa BoT na wana CCM maarufu, bado hakuna kati yao anayetajwa wala kuitwa na kamati ya uchunguzi.
Kutoka Raia Mwema wiki hii.