Monday, January 07, 2008


Hata kukonyeza ni kosa la ubakaji

Na Mohamed Majaliwa

KATIKA mfumo wa kisheria wa nchi yetu, kosa la ubakaji na makosa mengine yenye kufanana nalo, yalikuwa yakisimamiwa na kushughulikiwa chini ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 1984. Kwa mujibu wa sheria hii, kosa la ubakaji lilichukulia na kushughulikiwa kama makosa mengine ya jinai.

Pia kwa mujibu wa sheria hii, kosa hili lilimaanisha kitendo cha mtu mwenye jinsia ya kiume kumlazimisha mtu wa jinsia ya kike kushiriki naye katika tendo la ndoa.

Kwa mujibu wa sheria hii, aina ya makosa ya ubakaji yalielezewa kwamba yanaweza kutokea katika mazingira ya aina mbili tofauti, mojawapo ikiwa ni kosa lenyewe linavyojieleza kimantiki. Mtu wa jinsia ya kiume atakapomlazimisha wa jinsia nyingine kushiriki naye tendo la ndoa bila ya hiari yake.

Lakini kwa upande mwingine, kosa la ubakaji kwa mujibu wa sheria hiyo niliyoitaja awali, ni pale kosa linapotambulika mbele ya sheria licha ya kuwa mtendewa wa kitendo husika ametoa hiari na ridhaa yake bila ya kulazimishwa.

Kosa hili hutokea pale mkosaji atakaposhiriki tendo husika na mtu wa jinsia ya pili ambaye bila ya shaka yoyote miaka yake haijakidhi haja ya umri wa utu uzima. Kitendo hiki kikitokea, basi hiari ya mtu mwenye jinsia ya kike haitakuwa na nafasi ya kumtetea mkosefu katika kosa kama hili.

Lakini pamoja na uwepo wa sheria hii ambayo pia iliainisha aina ya adhabu anayostahili mbakaji au mkosaji, bado makosa ya ubakaji yamekuwa yakiripotiwa kushamiri kila kukicha kwa kile kilichosemekana kuwa ni udhaifu wa sheria husika na udogo wa adhabu kwa mujibu wa sheria hiyo.

Kutokana na kushamiri kwa makosa haya, ndipo mnamo mwaka 1998 ilipitishwa sheria maalum ya kusimamia na kushughurikia makosa yote yanayotokana na vitendo vinavyolenga kudhalilisha jinsia ya mtu. Hii ilijulikana kama Sheria ya Makosa ya Jinsia ya mwaka 1998.

Sasa basi mbali na kosa lenyewe la ubakaji kama lilivyoelezewa katika sheria ya makosa ya jinai, sheria hii mpya kwa makusudi imeongezea makali ili kupanua wigo wake katika kushughurikia vitendo vyote vyenye mwelekeo wa kudhalilisha jinsia ya kike.

Katika kuridhia lengo hili lenye la kudhoofisha vitendo vinavyoonekena kwa namna moja au nyingine kuchangia matendo ya ubakaji, hasa kwa wanawake na watoto, ndipo sheria ikadhihirisha wazi vitendo ambavyo endapo vitafanywa na mtu yeyote dhidi ya mwanamke au mtoto, basi vitamaanisha kosa kinyume na sheria hii ya makosa ya jinsia ya mwaka 1998.

Kwamba mtu yeyote ambaye atafanya kitendo chochote kinachoweza kusababisha kero ya kijinsia kwa mwanamke atakuwa anatenda kosa hilo.

Zaidi imeelezwa na sheria husika kuwa, kero hii ya kijinsia inaweza kufanywa kwa kutumia ishara na namna nyingine za lugha zinazofanana na hizo ikiwa ni pamoja na kukonyeza. Kwa mujibu wa sheria hii, kosa hili linajulikana kisheria kama shambulio la kijinsia ambalo adhabu yake ni kifungo kisichozidi miaka mitano jela.

Vitendo hivi vya kutumia lugha za matusi na ishara nyingine zenye ueleo wa kusababisha kero ya kijinsia kwa mwanamke vimekuwa vya kawaida.

Pengine kwa sababu watendaji au hata watendewaji hawajui au wamegubikwa na ujinga kuhusu haki na wajibu wao katika hili. Mara kadhaa imetokea katika maisha yetu ya kila siku, na hata kusababisha ugomvi kati ya watu wanaodaiwa kufanyiana vitendo hivyo vyenye asili ya shambulio la kijinsia.

Kitendo cha kukonyeza ni cha kawaida sana katika jamii yetu, hasa endapo itatokea kufanyika kati ya watu ambao wenyewe wanaelewana kwa lugha hiyo iwe kwa utani au kwa mahusiano yao kwa nia ya kupata mawasiliano ya faragha kati yao.

Lakini lugha hii ikitumiaka kwa mtu ambaye hana maelewano wala mazoea na mtendaji, inawezekana kusababisha matatizo kwa upande wa mtendaji kwa kufunguliwa mashtaka ya shambulio la kijinsia kinyume na sheria ya makosa ya kijinsia niliyokwaishaitaja hapo awali.

Ikumbukwe kuwa kosa la vitendo hivi linakwenda sawa sawa na vitendo vingine vyenye mwelekeo wa kero ya kijinsia kama vile ishara za matusi kwa kutumia vidole vya mikono na nyinginezo.

Simu ya mkononi: 0786 809798
Baruapepe: almajah2000@yahoo.com

No comments: