Saturday, February 16, 2008

Kwa nini miswada

inaandaliwa kwa

Kiingereza?



Hellen Ngoromera

KISWAHILI ni lugha ya Kibantu yenye asili ya mwambao wa pwani ya Afrika Mashariki, yenye lahaja mbalimbali ambayo inatumiwa na watu wengi hasa wa Afrika Mashariki na Kati.

Kwa hapa Tanzania lugha hiyo hutumika kwa asilimia kubwa katika shule za msingi, majumbani, maofisini na sehemu nyingine.

Katika mfumo rasmi wa elimu hapa nchini Kiswahili kinatumika kama lugha ya kufundishia katika elimu ya awali, shule ya msingi, mafunzo ya cheti cha elimu ya ualimu na elimu ya watu wazima na katika ngazi ya elimu ya sekondari hadi elimu ya juu. Kiingereza ndiyo lugha ya kufundishia.

Mwanaharakati wa Kiswahili nchini, Malachi Majwala, anasema pamoja na lugha hiyo kuwa ya taifa hadi sasa imeendelea kudharauliwa kutokana na kutotumiwa sana, na badala yake kuitumia lugha ya Kiingereza kama lugha ya kufundishia katika elimu ya sekondari.

“Kama tutaendelea kufundishia kwa lugha ya Kiingereza, sayansi na teknolojia ambayo tunahitaji sana kwa maendeleo ya taifa letu katika karne ya 21 na itaendelea kuwa haki ya watu wachache wanaofahamu Kiingereza,” anasema mwanaharakati huyo.

Anasema ili Tanzania iweze kupata maendeleo katika maeneo ya elimu sayansi na teknolojia sera kama vile mpango maalumu wa kuwezesha elimu na mafunzo katika ngazi zote kutolewa katika lugha ya Kiswahili utaandaliwa.

Anasema Tanzania iliamua pia kufanya mageuzi makubwa katika kupindua utaratibu wa elimu ya shule za msingi ukabadilishwa watoto kusoma Darasa la Saba badala ya la Nane.

Anasema pia pamoja na hilo masomo yote yalianza kufundishwa kwa lugha ya Kiswahili hadi leo. Tangu kipindi hicho hadi sasa ni miaka 41, lengo lilikuwa ni kuhakikisha elimu yote hadi chuo kikuu kufundishwa kwa lugha ya wazalendo.

Anasema kwa makusudi na njama za hali ya juu watawala wachache waliihujumu nchi wakaacha kuweka wazi lugha ipi itakuwa ya taifa kati ya Kiingereza na Kiswahili.

“…Jambo hili lilitamkwa tu kuwa lugha ya taifa ni Kiswahili hivyo inaniwia vigumu kujua kwa nini katiba haikufafanua kuwa lugha ya taifa kama itakuwa Kiswahili?

“Watanzania hii ni njama za wachache kututawala na kuna mengi ambayo yamefichika, ukweli ni kwamba ‘gawa utawale’. Hizo zote na mengineyo yasiyojulikana kwa wengi bali na wachache ni njama za Wazungu kwa kutumia wachache kututawala Waafrika hadi mwisho wa dunia atakapokuja Bwana Yesu.

Ooo! Kiswahili lugha yangu ninakatazwa nisikutumie, katika bara la Afrika ambalo lina nchi 53, ni nchi saba tu ndizo zilizo na lugha zinazoweza kutumiwa kufundishia. Nchi hizo ni Tanzania, Somalia, Botswana, Lesotho, Swaziland, Rwanda, Burundi”, anasema Mwanaharakati huyo.

Anasema katika nchi hizo saba Tanzania tu ndiyo inayoongoza kwa lugha ya Kiswahili, yenye uwezo na uliosambaa na kupanuka duniani kote. Anawashauri Watanzania kuwaacha dhana iliyojengeka na kupandikizwa rohoni na akilini kwamba ili uweze kuwa na elimu ya kimataifa ni lazima ufahamu wa Kiingereza, anasema si kweli kwani wapo watu wengi wanafahamu Kiingereza lakini hajui hata kutengeneza baiskeli.

“Watoto wetu wanapokwenda kusoma Urusi wanaofika huko huchukua mwaka mmoja au miwili wakijifunza Kirusi, ndipo huanza masomo yao vyuoni. Kwa nini Warusi wao wasitumie Kiingereza kama lugha ya kimataifa ya kujifunzia?

Utaratibu ambao tunapigania ni ule ule wa shule za msingi kuwa Kiingereza kitaendelea kufundishwa katika hatua zote kuanzia Darasa la Kwanza hadi vyuo vikuu kwa ufasaha na walimu waliobobea kwa lugha lakini masomo yote na mazoezi pamoja na utafiti zifanyike kwa lugha ya Kiswahili,” anasema Mwanaharakati huyo.

Anasema vitabu vipo na vitaendelea kuwapo na kufanyiwa tafsiri. Mambo mengine yataendelea kubadilishwa hatua kwa hatua hadi kufikia umakilifu wa mwisho.

“Haya yakiendelea kufanywa wito wangu ni kuwa patolewe amri, tamko, sera na utekelezaji kuanzia mwaka 2011 kwa walimu waanze kufundisha kwa kutumia Kishwahili kwa masomo yote hata kama watakuwa wanachanganya lugha yaani ‘kiswanglish’, pia mitihani itungwe kwa Kiswahili kwa masomo yote na ikiwa kutakuwa na sehemu itakayoshindikana watumie kiingereza” anasema.

Mwanaharakati huyo anashauri pia wanafunzi kuwa huru wakati wa kufanya mitihani ya masomo mbalimbali wawe huru kujibu mitihani kwa Kiswahili.

Majwala anashauri Watanzania kuhamasishwa kujitolea kufanya jitihada za dhati kufanya mageuzi makubwa ya kutafsiri vitabu mbalimbali, ili viweze kutumika katika shule mbalimbali.

Anawashauri wataalamu wa chuo kikuu, Baraza la Kiswasili la Taifa (Bakita) na wengine wa ndani na nje ya nchi kusaidia kufanya kazi hiyo ya kutafsiri. Anamtaja Profesa Issa Shivji, Profesa Salai, Bakita na watu wengine.

Kwa mujibu wa Majwala, wataalamu hao ambao pia ni wadau wa jambo hilo wametoa ushauri juu ya jambo hilo na kukubaliana na kazi hiyo pia Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) kimepiga hatua kwa kuweka Kiswahili katika kompyuta. Kwa mantiki hiyo mwanaharakati huyo anaomba wapewe haki hiyo.

“…Serikali zetu hizi hutumia udikteta, ukandamizaji hata katika mambo ambayo ni haki ya wananchi, Watanzania wengi hawajui ni athari gani watoto wao wanapata leo na baadaye kwa kutoruhusiwa kutumia lugha ya kufundishia hadi chuo kikuu.

Hebu angalia muswada wowote ambao unawasaidia Watanzania ambao chimbuko lao ni Kiswahili unaandaliwa kwa Kiingereza, halafu bila aibu wabunge wetu tuliowachagua, hawaupingi bali huujadili kwa Kiswahili, wana maana gani muswada huu ni wa Watanzania - Waswahili au Waingereza? Huu ni ukiukaji wa haki za raia,” anasema Majwala.

Anarudi nyuma na kusema mwaka 1969 Mzee Rashidi Kawawa alitoa nyaraka kwa ofisi zote za serikali kuanza kutumia lugha ya Kiswahili na mabadiliko yalifanywa.

Anasema sambamba na hilo iliamriwa masomo yote kuanzia darasa la kwanza hadi la saba kufundishwa kwa Kiswahili na Kiingereza kilibaki kufundishwa kama lugha katika madarasa hayo.

“Utaratibu huo tunataka utumike hadi vyuo vikuu sambamba na katika mitihani, mwaka huo huo wizara ya elimu ilitoa nyaraka kwa wakuu wote wa shule za sekondari kufundisha masomo ya siasa, na sayansi ya jamii kwa Kiswahili. Mwaka 1970 iliamriwa history, jiografia, baiolojia, na hisabati kufundishwa kwa lugha ya Kiswahili pia kuanzia mwaka 1971 maagizo ambayo hadi leo hayajatekelezwa.

Suala hilo limepigiwa kelele bila mafanikio, hadi leo sisi bado ni watumwa wa Wazungu kwa kuenzi lugha yao na kuidharau lugha yetu, viongozi wengi wamepiga kelele,” anasema.

Anashauri Kiswahili kitumike kufundishia kuanzia vyuo vikuu vyote nchini hadi chekechea na kuwa hiyo ndio itakayokuwa suluhisho la matatizo mbalimbali likiwamo la kushuka kwa kwango cha elimu nchini.

Watoto wengi wanashindwa kufanya vizuri darasani kutokana na kutumia lugha ya Kiingereza ambacho hawakijui vizuri. Aliongeza kuwa lugha hiyo pia inawapa shida hata walimu.

Anasema hata Jaji Mkuu, Agostino Ramadhani aliwataka watendaji wa mahakama wakiwamo mawakili kutumia lugha ya Kiswahili wanapoendesha kesi zao.

Anazungumzia kuhusu katiba ya nchi na kusema kwa makusudi watawala wachache wa nchi wameacha kuweka wazi lugha ya taifa itakayotumika. “…Imetamkwa tu lugha ya taifa ni Kiswahili hivyo inawawia vigumu kujua kwa nini katiba haikufafanua lugha ya taifa itakuwa ipi kati ya Kiswahili na Kiingereza,” anasema Majwala.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0754 886 749 au
barua pepe: helenpendo@yahoo.com



No comments: