Thursday, February 28, 2008


Lowassa aonya kuna

‘kidudumtu’ CCM


na deodatus balile, monduli

WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, amekitahadharisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa ndani yake na serikalini kuna wafitini wanaotaka kupotosha ajenda ya maendeleo kwa kupiga kelele za ufisadi.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika eneo la Mto wa Mbu jimboni Monduli, Lowassa alisema CCM ina watu ndani yake ambao hawakitakii mema chama hicho. “Naomba nieleweke katika hili. Sisemi tusipambane na ufisadi, tusishughulikie wanaoiba mali ya umma… tupambane nao, ila wapo wenzetu ndani ya chama na serikali watakaojaribu kututoa kwenye hoja yetu.

“Tusimamie Ilani ya uchaguzi kwa mshikamano. Tukiyumba katika hili na tusipofanya hivyo, mwaka 2010 tutakuwa na maswali mengi sana na wapinzani wetu tutawapa fursa,” alisema.

Alisema wakati wa kampeni mwaka 2005, chama kiliwaahidi watu maisha bora na kuonya kuwa ahadi hiyo isipotekelezwa, hatari kubwa inakinyemelea chama; “Tuwajue wasiotutakia mema mapema tusikitengenezee chama bomu mbele ya safari,” alisema Lowassa.

Lowassa aliyepokewa na waendesha baiskeli eneo la Kigongoni, lililopo wastani wa kilomita tatu kutoka Mto wa Mbu, alihutubia wakazi wa eneo hilo na kupewa magunia mawili ya mchele, ndizi na mkanda wenye sime.

Aliwambia wananchi hao kuwa yeye bado ana nguvu zake, akili na uwezo, na akafafanua kilichotokea kuhusiana na kashfa ya Richmond hadi kujiuzulu katika alichoeleza kuwa ni uwajibikaji wa pamoja.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi, walisema ufafanuzi alioutoa Lowassa ni kiashirio na maelezo tosha kuwa hakushiriki katika kashfa hiyo.

Mwananchi aliyejitambulisha kama Peter Longidai, alisema: “Juzi aliwataja kina (Dk. Ibrahim) Msabaha, (Johnson) Mwanyika na (Grey) Mgonja. Si na wao wanayo midomo? Kama alihusika si waseme? Yeye kasema wao wanajua kila kitu, mbona wako kimya sasa? Ukweli unazidi kufahamika,” alisema.



No comments: