Mtambo wa DNA
waumbua wanawake
* Wengi wagundulika kuzaa watoto nje ya ndoa
* Mmoja alilea mtoto asiye wake kwa miaka 15
na dennis luambano
* Mmoja alilea mtoto asiye wake kwa miaka 15
na dennis luambano
ASILIMIA 47 ya wazazi wa kiume waliowasilisha sampuli za vinasaba (DNA), kwa ajili ya kufanyiwa utafiti katika Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), wamethibitika kubambikiwa watoto.
Kati ya mwaka 2006 na 2007, GCLA ilichunguza sampuli 209 za vinasaba na kubaini kuwa, asilimia 47 ya vinasaba hivyo havina uhusiano wowote kati ya wazazi (baba) na watoto.
Kwa upande mwingine, asilimia 53 ya sampuli hizo 209, zilithibitisha kuwa wazazi wenye sampuli hizo ni halali baada ya uchunguzi huo kufanyika kwenye mtambo wa DNA.Takwimu hizo zilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Ernest Mashimba, wakati akizungumza na MTANZANIA ofisi kwake.
“DNA ni chembechembe asili za urithi ambazo zinabeba taarifa zote kama za maumbile na tabia ambazo zipo katika kila kiumbe…kila kiumbe kikiwa na DNA zisizofanana.
“Matumizi ya uchunguzi wa DNA yapo mengi mojawapo yakiwa ni ya utambuzi wa mtoto na mzazi (parentage) ambapo katika hili tulipokea sampuli 209 mwaka juzi na mwaka jana kwa ajili ya kuchunguza uhalali wa uzazi,” alisema Dk. Mashimba.
Alisema sampuli walizozipokea kwa ajili ya uchunguzi huo zilikuwa ni damu, majimaji ya uume na uke, ngozi, nywele, mate, kamasi, jasho, kucha, mkojo na kinyesi.
Kwa mujibu wa Mashimba, kati ya mwaka 2005 hadi 2006 kesi 250 za utambuzi wa uhalali wa mzazi kwa mtoto zilipokewa GCLA.
Alisema baada ya uchunguzi kufanyika, asilimia 40 ya kesi hizo zilithibitisha kuwa wenye sampuli hizo ni baba halali huku asilimia 60 zikithibitisha kuwa si baba halali.
Aidha, alisema mwaka 2004 jijini Dar es Salaam, uchunguzi wa DNA uliweza kuthibitisha kwamba baba alilea mtoto kwa miaka 15 akidhania ni wake kumbe alikuwa si wake.
“Mtu huyo alilea mtoto kwa muda wa miaka 15 akidhani ni wake mpaka kesi hiyo ilipokuja kwetu ndipo vipimo vya DNA vilipobainisha kwamba hakuwa wake,” alisema Dk. Mashimba.
Alisema mwaka 2006 vipimo vya DNA vilitatua kesi mbili za kubadilishwa watoto (swapping) katika hospitali ya Bugando iliyopo Mkoa wa Mwanza na hospitali ya Muhimbili iliyopo jijini Dar es Salaam.
Alisema gharama za vipimo vya DNA kwa mtu mmoja ni Sh 100,000 na vinafanyika jijini Dar es Salaam tu.“Gharama za vipimo vya DNA ni Sh 100,000 ambayo ni nafuu sana ukilinganisha na nchi nyingine za Ulaya kwa sababu kule hawatozi kwa mtu bali hutoza kwa kesi nzima,” alisema Dk. Mashimba.
Alisema kesi zinazowafikia ni za watu wa ngazi tofauti ambao ni wenye kipato cha chini, matajiri na wengine ni wasomi.
Aidha, alisema maabara iliyopo Mkoa wa Mwanza na Arusha hazina mitambo hiyo ila zinafanya kazi nyingine za kuchunguza chakula, maji, dawa na vipodozi.
Alisema wanatarajia kufungua maabara nyingine katika Mkoa wa Mbeya ili kufanya huduma za kimaabara ziwe zinapatikana kwa urahisi.
No comments:
Post a Comment