Mambo ya ushirikina?
Mwanafunzi albino
atekwa Mbeya
Merali Chawe, Mbeya
Daily News; Thursday,February 28, 2008 @00:04
MWANAFUNZI wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Ukukwe wilayani Rungwe ambaye ni albino, amepotea akidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana.
Henry Mwakajila (18), alikumbwa na masahibu hayo Februari 5, mwaka huu wakati akirejea nyumbani kwao kutoka kwenye masomo ya jioni na wanafunzi wenzake.
Babu wa kijana huyo, Mzee Mbweleweta alisema siku hiyo ya tukio, alipelekewa taarifa na mjomba wa kijana huyo aliyekuwa akiishi naye ambaye alikuwa akitaka kujua kama Henry alilala kwa babu huyo kutokana na kutorejea nyumbani.
Alisema baadaye walipofuatilia kwa ndugu, jamaa na marafiki mbalimbali bila kumpata, ndipo walipotoa taarifa kwa uongozi wa Serikali ya Kijiji ambao uliitisha mkutano na kufuatilia, ambako waliokota kofia na kalamu ya Henry ambavyo vilikutwa vikiwa vimeanguka umbali tofauti njiani kwenye shamba la mahindi.
Katibu wa Kitongoji cha Masebe, Lucy Kipesile, alisema katika kufuatilia tukio hilo la kupotea kwa mwanafunzi huyo, walibaini kuwapo kwa mibururo ardhini kwenye majani pamoja na mahindi kulala chini hali iliyoonyesha kwamba kijana huyo alikuwa akivutwa kwa nguvu na watu waliomteka.
Alisema kuanzia hapo wanakijiji walifuatilia mibururo ambayo iliishia katika mto Kipoke. Pia walifuatilia kilomita kadhaa kandokando ya mto huo na mito mingine midogo, vichaka, misitu bila ya mafanikio ya kuona dalili za kuwapo kwa mwili wa kijana huyo kutokana na hisia kuwa huenda alikuwa ameuawa.
Baadhi ya wakazi wa Kitongoji cha Masebe, wanalihusisha tukio hilo na imani za kishirikina, wakiamini kuwa kijana huyo alichukuliwa kwenda kunyofolewa viungo vya mwili kwa ajili ya kutengenezea dawa za kupata utajiri wa haraka kama inavyotokea katika Mkoa wa Mwanza.
Kwa upande wake, Chifu wa eneo hilo, Ruben Mwakang’ata alisema yeye na Chifu mwenzake Mwankenja katika mambo yao ya kimila wamegundua kuwa kijana huyo ametekwa kufanyiwa mambo ya ushirikina na kwamba hata hivyo wanadai kuwa kijana huyo bado hajauawa.
Alisema wao wanaendelea kufanya mambo ya kimila kuweza kuwatambua watu waliomteka kijana huyo na mahali alipofichwa waweze kumuokoa akiwa hai. Hata hivyo wameelezea kusikitishwa kwao na kutothaminiwa na kutambuliwa mchango wao na Serikali hasa kwenye matukio makubwa kama hilo.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Mariam Lugaila alisema watu wenye ulemavu wa ngozi, (Albino) ni sawa na watu wengine hivyo wana haki ya kuishi na kulindwa kama ilivyo kwa wananchi wengine na kwamba imani kuwa viungo vyao vinafaa kutengenezea dawa ili kupata utajiri ni imani potofu na zinapaswa kupigwa vita kwa nguvu zote.
Akijibu malalamiko ya Machifu kudai kutothaminiwa na Serikali, Lugaila alisema Serikali inathamini na kutambua mchango wa Wazee wa Mila, lakini haiamini ushirikina hivyo ametoa wito kwa kila mtu kwa imani yake ashiriki katika kumtafuta kijana huyo akiwa hai au amekufa.
Naye Kiongozi wa Maalbino wa Mkoa wa Mbeya, Gwantwa Mwalyaje alisema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kupotea kwa kijana huyo na wanaamini ametekwa na watu wenye lengo la kupata utajiri, hivyo ameiomba Serikali kufuatilia kwa kina tukio hilo na kuwalinda albino.
No comments:
Post a Comment