Monday, February 18, 2008

Roho ya Mwakyembe

yasakwa kwa bil. 200???


Na Luqman Maloto


wakati wajumbe wa Kamati Teule ya Bunge, iliyochunguza mchakato wa utoaji zabuni kwa Kampuni ya Richmond Development LLC, wakidai kutishiwa maisha, baadhi ya wabunge wamesema, kuuawa kwao ni unyama na aibu kwa taifa.Wabunge hao, walimueleza mwandishi wetu kwa nyakati tofauti, baada ya kuahirishwa kwa kikao cha 10 cha bunge, Ijumaa iliyopita kwamba kusakwa kwa roho za wajumbe wa kamati hiyo ni sawa na kuyafananisha maisha yao na thamani ya mkataba wa Richmond ambao ni zaidi ya shilingi bilioni 200....

Walisema, serikali inapaswa kuingilia kati suala hilo kwakuwa siyo busara roho za wajumbe hao, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, Dk. Harrison Mwakyembe, thamani yake iwe shilingi bilioni 200.

“Wao walitibua ‘dili’ la Richmond ambalo thamani yake ni zaidi ya shilingi bilioni 200, kwa hiyo kitendo cha kumtishia maisha Mwakyembe na wenzake ni sawa na kulinganisha thamani ya roho zao na kiasi hicho cha pesa,” alisema mbunge mmoja wa CCM, mkoani Mwanza ambaye aliomba hifadhi ya jina lake.

Mbunge huyo aliongeza: “Hizo sms za kutishiwa kuawa ni lazima zizingatiwe, maana inawezekana waliohusishwa na ufisadi wa Richmond wakatulia, lakini wapambe wao ndiyo wakalipiza kisasi kwa kuwapiga risasi wajumbe wa kamati
teule.”

Dhana kwamba Mwakyembe na wenzake wanaweza kupigwa risasi, ilichangiwa na mmoja wa mawaziri walioteuliwa katika baraza jipya (jina kapuni).

“Suala la wajumbe wa kamati teule kuuawa kwa kupigwa risasi lipo, ndiyo maana hata Selelii wakati wa kuchangia hoja alisema kwamba waliwahi kushikiwa bastola na baadhi ya maofisa wa serikali ili wasifanikishe uchunguzi wao,”

Ijumaa iliyopita, Mbunge wa Nzega (CCM), Lucas Lumambo Selelii ambaye ni mmoja wa wajumbe wa kamati teule alisema kuwa kipindi wapo kwenye uchunguzi, waliwahi kupokea vitisho, ikiwemo kushikiwa bastola ili wasifanikishe zoezi lao.

Aidha, Selelii aliongeza kuwa yeye na wajumbe wenzake walikuwa wakitishiwa kwamba hawatofika mwisho wa uchunguzi wao.

Sambamba na hao, gazeti hili liliongea na wabunge watano waliopo kwenye kamati teule ambao wote walithibitisha kupokea sms za kutishiwa maisha, hivyo wakawataka Watanzania kuwaombea, pia serikali iwape ulinzi.

Mbunge wa Kyela (CCM), Dk. Mwakyembe alisema kuwa wanazitafakari sms wanazotumiwa na katika siku chache zijazo watawasiliana na vyombo vya dola ili kuwachukulia hatua hao watu wanaowatishia maisha.

“Tunawasiliana na wenzangu, katika siku tatu au nne utaona hatua tutakayoichukua,” alisema Mwakyembe na kuongeza kwamba katika kipindi hiki ambacho wanatafakari cha kufanya, serikali inapaswa kuwalinda.

Wakati Mwakyembe akisema hayo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati Teule, Injinia Stella Manyanya alisema, maisha yake yote amemkabidhi Mungu kwakuwa ndiye mlinzi wake.

“Maisha yangu yapo mikononi mwa Mungu, hata kama kuna vitisho au hakuna vitisho, lakini kila siku ninapoitazama pua yangu na ikinionesha udongo, najua one day (siku moja) nitakufa tu,” alisema Manyanya.

Mjumbe mwingine wa kamati hiyo, Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohammed Mnyaa alisema kwa sasa amebadilisha staili ya maisha yake ili kuweza kujilinda na hatari inayomzingira.

Alisema sasa hivi yupo makini kwa kila kitu anachokula na kunywa kisha akaongeza: “Hata kwenye safari siendi peke yangu, naongozana na wenzangu wanaonifahamu, lakini zaidi namuamini Mola.”

Aidha, Mnyaa alilitajia gazeti hili sms aliyotumiwa na mtu mwenye namba asiyoifahamua, inayosomeka: “Haya sasa umeshatunyang’anya ugali wetu, wewe umefanikiwa sasa shauri yako na wewe utaona.”

Akiongea kwa simu na mwandishi wetu, Jumamosi iliyopita, Selelii aliwataka Watanzania wamuombee pamoja na wajumbe wenzake wa kamati teule iliyochunguza mkataba wa Richmond.

Naye, Mbunge wa Muheza (CCM), Hubert Mtangi alisema: “Namtegemea Mungu na cha msingi ni kupunguza nyendo zako, kama ulikuwa unachelewa kurudi unawahi.”

Mtangi, alipoulizwa na mwandishi wetu kuhusu uwezekano wa yeye na wenzake kupigwa risasi, alijibu: “Hilo tunajua linaweza kutokea, kama ni kuuawa kwa kupigwa risasi nipo tayari, sisi tulishaamua kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya Watanzania.”

Awali, kabla ya Selelii kusema bungeni kwamba wanatishiwa maisha, Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shellukindo alisema Alhamisi iliyopita kuwa yeye na mumewe William Shellukindo wanapewa vitisho tangu ripoti ya Richmond iliposomwa.

William Shellukindo (Mbunge wa Bumbuli CCM) ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Biashara na Uwekezaji, pia ndiye aliyekuwa kinara wa kulishawishi bunge, liunde kamati teule ya kuchunguza mkataba wa Richmond ambao uliigharimu serikali zaidi ya shilingi bilioni 200.

Ripoti ya Richmond, ilisomwa bungeni wiki mbili zilizopita na kuwatia hatiani, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ibrahim Msabaha.

Mawaziri hao, wote walijiuzulu kabla ya Rais Jakaya Kikwete kuvunja baraza zima la mawaziri na kuteua jipya ambalo aliliapisha Jumatano iliyopita kwenye Ukumbi wa Ikulu Ndogo, Chamwino mjini Dodoma.



No comments: