Nani malaya?
Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.
Frank mpenzi,
MBONA kimya kimezidi mpenzi wangu? Yaani nakaa, nakaa, nakaa nikisubiri angalau maneno mawili matatu kutoka kwako lakini kimyaaa! Hata ninapojaribu kukupigia simu hujibu. Napiga weeeee hakuna wa kupokea. Kulikoni mpenzi!!
Yaani sina raha hata kidogo. Kama nimekukosea si uniambie mwenzio, si kuniacha solemba namna hiyo. Nakaa nawaza, nawaza, nimekukosea nini, lakini jibu sipati. Mbona tulipoongea siku ile hakukuwa na dalili yoyote upande wako? Nini kimekubadilisha ghafla?
Hata hivyo, ukitaka kujua hali yangu, mimi hapa ni mzima, ukiacha misononeko inayotokana na ukimya wako. Hadi hata mama bosi alitambua. Lakini kama kawaida ya wakubwa hakutaka kuuliza. Badala yake alirukia uamuzi.
‘Vipi Hidaya? Mbona unashika taya hivyo? Umechoka kazi?’
‘Hapana mama.’
‘Sema kama umechoka kazi nikurudishe nyumbani.’
‘Si hivyo mama. Nilikuwa ninawaza kidogo tu.’
‘Unawaza unawaza. Nakulipa ili uwaze! Basi changamka hapa. Sitaki kukuona umenuna wasikia.’
Basi mpenzi pamoja na misononeko yote ya kukukosa bila kujua sababu, ilibidi niamke na kuchangamka kana kwamba sina shida kabisa. Na kweli, mara nyingine kazi inasaidia maana ninapofua lundo la nguo za bosi (na ni nyingi kwa sababu anang’ang’ania kuvaa suti daima hata ikiwa joto namna gani, eti suti ni dalili ya maendeleo ...) basi nasahau angalau kwa dakika mbili tatu kwamba mpenzi wangu wa moyo hataki kuongea na mimi. Kwa hiyo nihurumie jamani, nihurumie, vinginevyo utashtuka nimefukuzwa kazi hivihivi.
Tuache hayo. Maana najua pia, upande wa shida, kwa kweli siwezi kujilinganisha na wasichana wenzangu wengi. Angalau nina kazi japo mshahara masihara anavyosema fyatu mkuu, angalau bosi hajajaribu kunitongoza hovyohovyo, angalau nina kitanda cha kulalia na chakula kila siku.
Juzi niliangalia wale wasichana walioswagwa na kuburuzwa eti wanajiuza usiku. Kwani wana nafasi ya kuuza bidhaa nyingine? Kwani wamepewa uwezo wa kujenga maisha tofauti?
Nakumbuka huko nyumbani mmoja wa wale wasichana alikuwa anapanga karibu sana na nyumba yetu pamoja na wadogo zake wawili. Kila usiku wanakula pamoja kisha anajipara na kuondokea viwanja. Wazazi walikuwa wananikataza kila siku nisiongee naye, eti mshenzi, eti malaya, eti sijui nini. Lakini kadiri walivyomtukana na mimi nilishikwa na hamu ya kumfahamu zaidi. Kila nikipita nilikuwa namsalimia hadi tukazoeana kidogo. Kisha siku moja akanikaribisha ndani ya chumba chake. Lo! Bonge ya kitanda. Ukiingia tu, yabidi uangukie kitanda hakuna mahali pengine. Nilipoonyesha mshangao akacheka.
‘We Hidaya unashangaashangaa nini? Kashangae watu. Wajifanya watakatifu na kuwalaani wenye dhambi kumbe dhambi zao zimewatifua wengine wafanye kufuru.’
‘Unasemaje dada?’
‘Hebu kaa basi upate soda.’
Nilikuwa na wasiwasi mpenzi, labda alitaka kuniingiza ndani ya biashara hii kijanja lakini sikuona dalili ya mwanamume yeyote. Hata hivyo, nilihakikisha kwamba nakaa karibu kabisa na mlango ili niweze kukimbia mbele ya hatari. Lakini msichana wa watu akaendelea na shughuli zake, kaniletea soda na kalimati mbili tamu sana.’
‘Unazipika mwenyewe dada?’
‘Kabisa.’
‘Sasa, samahani, kama ni hivyo, kwa nini una ... una .. nanihii?’
Wacha yule msichana (anaitwa Neema) acheke.
‘We Hidaya si useme tu. Kwa nini najiuza?’
Niliangalia chini kwa aibu.
‘Ndiyo. Samahani lakini.’
‘Samahani ya nini! Mimi sifurahii kujiuza lakini nitauza nini zaidi. Si umeona wadogo zangu wawili. Watakula nini kama sijishughulishi namna hii. Kalimati hazitoshi kuwalisha hata kidogo, na watu walivyo washenzi wala hawalipi hadi mwisho wa mwezi, tena kwa kukabwa sana. Lakini hii biashara nyingine, lazima walipe kwanza ndipo napata pesa kwa ajili ya wadogo zangu.’
‘Lakini kwa nini ndugu zako hawakusaidii?’
‘Wanisaidie mimi? Usinichekeshe.’
Basi Neema akatoa kicheko cha uchungu sana kisha akanyamaza. Mimi niliamua kushughulikia soda kwanza maana niliona kama machozi yanamlenga.
‘Unajua Hidaya, wazazi wangu walipokufa katika ajali miaka miwili iliyopita, nilikuwa na miaka 14. Ndugu wakaja wakijitia kuangua kilio huku wanachungulia wazazi wangu walikuwa na nini. Wakachukua kila kitu eti ni haki yao kama walezi wetu lakini hakuna aliyekuwa tayari kutuchukua kwa pamoja na kutusomesha. Sasa sisi watoto hatukutaka kutenganishwa hata kidogo, kwa hiyo nilikataa. Nikasema kwamba nitawasomesha wadogo zangu mimi mwenyewe. Wakajifanya wanapinga na kunihurumia tena lakini walikuwa wanatoa tabasamu za kifedhuli kabisa na katika furaha ya kukosa majukumu kwetu walihakikisha kwamba wamechukua hadi sufuria ya mwisho ndani ya chumba.’
‘Lo pole sana dada. Watu wengine washenzi sana.’
‘Si ndiyo. Lakini wanavyojifanya watakatifu mwisho utacheka tu. Yaani wakati wanaondoka wananipa maneno meeeengi ya kuniasa eti niwe na tabia njema, UKIMWI upo, Mungu yupo ... na pia kujidai kunikaribisha kwao nikiwa na shida. Lakini nilijua ni maneno ya fiksi tu. Sasa nimebaki hapa na wadogo zangu. Kutokana na biashara yangu ya mwili nimeweza kuwasomesha wadogo zangu na sasa yule mkubwa anaingia Kidato cha Kwanza. Mungu akinipa miaka minne zaidi ya uhai, bila huo ugonjwa, najua atamaliza Sekondari na hatalazimika kufuata nyayo zangu.’
‘Hee Neema, pole tena’
‘Usinipe pole. Ninafurahi. Sifurahii upumbavu wa wanaume wengi lakini yuko mmojammoja anayenijali na kunifanya nijisikie nathaminiwa angalau kidogo. Lakini kila nikiwaangalia wadogo zangu nafurahi. Na najua, licha ya maneno ya kinafiki ya ndugu zangu na wengine, thawabu yangu iko mbinguni. Watanielewa.’
‘Lakini dada nakupongeza kwa ujasiri wako.’
‘Si mimi tu. Tuko maelfu wenye matatizo kama hayo na hakuna anayejali. Mwanzoni yatima mwenzangu akanishauri kwenda kwenye danguro anakofanya kazi yeye. Alisema kwamba robo tatu wa wasichana pale walikuwa yatima kama mimi na waliobaki wanatoka kwenye familia za kambo. Kwa hiyo tungeelewana. Lakini mimi nilitaka uhuru zaidi ndiyo maana niliona bora nikae mwenyewe barabarani. Kwa nini mwenye danguro achukue pesa zangu wakati naumia mie!!’
Lo mpenzi nilishangaa na nilitaka hata kuwaambia wazazi kwamba wanakosea kumlaani Neema. Lakini nilijua watanihusisha naye nikimtetea kidogo. Si ndiyo akili fupi za watu. Nasikia kulikuwa na bosi mmoja hapa Bongo eti akiamka vibaya anawaswaga wasichana hao ndani. Hakuna cha maswali wala cha kutaka kuelewa matatizo yao. Funga tu. Na watu walipojitokeza kumwambia kwamba hata yeye hana huruma wala haki akawatukana eti ni wateja wao. Sasa juzi bosi mwingine naye ameamua kufanya vilevile. Badala ya kuwakamata waliofanya nchi hii iwe masikini anawakamata wanaouza umasikini wao. Kwa nini wasiwasikilize akina Neema na kujua matatizo yao badala ya kufura kwa kujidai wana maadili wanaochukia maovu? Kama ni watu wa maadili kwa nini hawawafungi wenye madili. Kwa sababu ni Wafarisayo wenzao? Yaani!!!
Labda ni hasira zangu kutokana na wewe kukaa kimya namna hii lakini kwa kweli wiki hii nawachukia watu hao vibaya sana. Namkumbuka Neema kila wakati. Eti yeye anajiuza. Na namwona akijibu.
‘Mnanikamata na nini. Mimi nauza mwili wangu, mali yangu tu. Wenzenu wanauza nchi, wanauza mali isiyo yao. Mimi nauza mwili wangu ili nijilishe mimi na wadogo zangu. Wao wanauza nchi ili waishi maisha ya fahari huku wakivaa masuti yao yanayonuka jasho la ufisadi. Nani malaya?’
Akuchunukuye hata kama wanichunia,
Hidaya.
Kutoka Raia Mwema la wiki hii.
No comments:
Post a Comment