Saturday, March 29, 2008


Hata kaburini, Mwalimu bado

anatusikitikia Watanzania


“KAMA mtaamua fedha kuwa ndio chanzo cha kuwapatia viongozi, basi mjue nchi inakwisha na CCM inakwisha. Oh! Nawasikitikia Watanzania wenzangu waliokuwa na uwezo wa kuongoza lakini hawana fedha, wataukosa uongozi.”

Hayo yalipata kutamkwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere katika moja ya hotuba zake wakati wa uhai wake.

Naam sherehe za Maulid na Pasaka za mwaka huu ziliambatana na kauli nzito za viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu kukemea ufisadi ulioshamiri nchini na hususan unaofanywa na viongozi.

Kimsingi, mashehe, mapadri na maaskofu ni viongozi wa kiroho. Viongozi wa kidini wana nafasi kubwa katika jamii yenye waumini wengi wa dini hizi kubwa mbili; Uislamu na Ukristo.

Tafsiri ya kemeo la viongozi wa kidini juu ya ufisadi ni kuitahadharisha Serikali juu ya kinachoendelea katika jamii na athari zake mbaya. Ukiona katika jamii viongozi wa kidini wamekaa kimya muda mrefu bila kutoa kauli za kuitahadharisha serikali, basi, ujue mambo yanakwenda vema.

Maana, si kazi ya mashehe na maaskofu kusimama na kuitetea au kuipongeza serikali. Hiyo ni kazi ya wanasiasa na wadau wengine wa masuala ya kiutawala.

Lakini mambo yanapokwenda kombo, ni kazi na wajibu wa mashehe, mapadri, maaskofu na hata viongozi wa imani za kijadi kusimama na kusema, kwa ukweli kabisa na bila ya chembe ya fitina au unafiki, kuwa mambo yanakwenda kombo. Na ndiyo maana ya kauli za viongozi wa kidini kuwa kuna ufisadi unaotokana na ubinafsi wa viongozi zinachukuliwa kwa uzito mkubwa na waumini wa dini zote na hata wasio waumini.

Huko nyuma tumeona matumizi makubwa ya fedha katika kutafuta uongozi. Hata sehemu ya fedha zilizopotea katika akaunti ya EPA inadaiwa zimetumika katika masuala ya uchaguzi kwa maana kutumika katika kuwapata viongozi. Ndipo hapa tunapaswa kurejea kauli ya busara ya Mwalimu hapo juu. Ni kweli, baadhi wameamua kutumia fedha kama chanzo cha kupata uongozi, na ni kweli sasa CCM inayumba na nchi inakwenda kombo.

Rais na Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete ana wajibu wa kwanza wa kuhakikisha imani ya wananchi kwake na Serikali yake inarudi haraka na kubaki. Hivyo basi, ana wajibu wa kwanza wa kuongoza harakati za kukisafisha chama chake ili kiondokane na kundi dogo la viongozi walioonyesha wazi wazi hulka za kifisadi. Jambo hili lina lazima ya kufanyika.

Naam. Viongozi wetu wa sasa wanahitaji kuambiwa mipaka yao kwa maana ya kuwa na miiko ya uongozi itakayowekwa wazi na ikajulikana na umma. Na adhabu ziainishwe kwa watakaokiuka miiko hiyo. Miiko ya uongozi yaweza kuwa tiba ya kuondokana na viongozi mafisadi wenye kutanguliza ubinafsi. Na hilo la ubinafsi ndilo lenye kuchangia sana vitendo vya kifisadi.

Kuna wanaoutafuta uongozi kwa maslahi yao binafsi. Inahusu haki pia. Na hii ni hoja ya msingi. Tumeona hata mifano ya baadhi ya viongozi waliotumia hila kukwapua nyumba za Serikali ili baadaye waje wazitumie kwa maslahi yao binafsi.

Ni hao, ambao bila haya, wanafanya dhuluma kubwa kwa wananchi wanaodai wanawaongoza. Baadhi yao kimsingi ni wahalifu kwa maana vitendo vyao vya kuhujumu mali za umma ni vya kihalifu. Hawa hawawatendei haki wananchi wanaodai wanawaongoza.

Siku zote, kujipendelea ndilo shina la maovu. Mathalan, tunaamini lililosababisha uamuzi wa kuuza nyumba za Serikali ni ubinafsi na hulka ya baadhi ya viongozi kutaka kujipendelea. Ni ajabu sana kwa viongozi hawa kutafuta hila za kukwapua nyumba za Serikali kwa kisingizio cha shida ya makazi wakati wa kustaafu wakati asilimia kubwa ya viongozi wetu waandamizi tayari wanazo nyumba walizojenga na nyingine kupangisha!

Naam. Siku zote, hamu inakuwa ni jambo jema, endapo binadamu ataweza kuitawala hamu yake.Tusipoitawala hamu yetu, tukaanza kujipendelea, kuwasahau wengine, basi, hilo huwa ndio chimbuko la maovu, huleta kutoelewana baina ya wanandugu na hata kwa maswahiba walioshibana. Huzua vurugu na machafuko katika jamii. Tunazungumzia uwepo wa upendo, haki na usawa.

Dini nyingi zinazungumzia umuhimu wa upendo, haki na usawa katika jamii. Iwe ni Uislamu na Ukristo vivyo hivyo. ” Naapa kwa zama . Hakika binadamu wote wamo katika hasara isipokuwa wale walioamini na wakafanya vitendo vizuri. Wakahusiana na haki na wakahusiana na subira” (Koran tukufu, Surat ASWR)

Na Biblia inasema kuwa Kaini alikuwa mtu wa kujipendelea mno, akamwua nduguye. Mfalme Saulo alijipendelea mno, akamdhulumu Daudi. Yuda alijipendelea mno, akaiba fedha za wenzake, hatimaye akamsaliti Yesu.

Ikumbukwe, mwaka 1966 kabla ya Azimio la Arusha, Mwalimu Nyerere na TANU waliliona tatizo la baadhi ya viongozi kuwa na tamaa ya kuishi kifahari na kujipendelea. Baadhi ya viongozi na hususan jijini Dar Es Salaam walianza ujenzi wa majumba ambayo baadaye yalipangishwa hata kwa ofisi za kibalozi au mashirika ya kimataifa. Jambo hilo linaandikwa na mwandishi Cranford Pratt katika kitabu chake; ” The Critical Phase In Tanzania 1945-1968).

Haikuwa haramu kwa viongozi kujijengea majumba ya kupangisha, kwani viongozi wa wakati huo walijenga nyumba hizo kwa kutumia mikopo ya watumishi. Hata hivyo, kulingana na sera za TANU za Ujamaa na Kujitegemea, Mwalimu Nyerere na TANU waliona haja ya kubadilisha taratibu hizo za mikopo ili kupunguza wimbi la viongozi kujijengea majumba ya kupangisha na kuongezeka kwa pengo la kipato kati ya viongozi na wanaowaongoza, yaani wananchi. Nyerere na Rashidi Kawawa waliamua kulishughulikia jambo hili kwa kupitishwa azimio la NEC ya TANU . Ndipo hapa tunaona chimbuko la miiko ya uongozi katika Azimio la Arusha.

Miaka ile ya 1960 TANU ililiona hilo la kiongozi kukopa na kujenga kuwa ni dhambi kwa vile iliona hatari ya kuwapo kwa pengo kubwa kati ya waongozao na waongozwao. Masikini, viongozi wale katika uadilifu wao, hawakujiwa hata na wazo la kuzigeuza nyumba za Serikali kuwa mali yao. Walichotaka ilikuwa ni mikopo tu, wajenge nyumba wapangishe, na bado haikuwa sahihi kwa mazingira ya wakati ule.

Mwalimu Nyerere aliziona nyumba za serikali, alikuwa na uwezo wa kutumia mamlaka yake na kukwapua yeyote aliyoitaka na kuifanya kuwa mali yake, akawapa hata wanae, nduguze na marafiki. Lakini akaamua kuchukua mkopo na kujijengea nyumba yake pale Msasani. Kawawa ni mfano mwingine. Amepata kuwa Waziri Mkuu na nyadhifa nyingine nyingi. Naye aliziona nyumba za Serikali, lakini leo anaishi kule kijijini kwake Kiluvya kwenye nyumba aliyojenga kwa jasho lake. Kuna mifano mingine mingi ya viongozi wa namna hiyo. Bila shaka, kuendekeza ubinafsi kunachangia katika mamuzi yasiyo na maslahi kwa taifa kama vile Richmond, IPTL na miradi mingineyo.

Kama vikao vya CCM kule Butiama havitafaulu kuja na azimio au taratibu zitakazoweza kukisafisha chama hicho na kuondokana na mafisadi wachache ndani ya chama hicho, basi, hata Mwalimu akiwa kaburini kwake Butiama , bado ataendelea kutusikitikia Watanzania wake aliotupenda kwa dhati.

Ikumbukwe siku zote, kuwa jambo zuri na la halali, daima litabaki kuwa ni zuri na la halali hata kama hakuna mwenye kuitenda halali hiyo. Na jambo baya na haramu, daima litabaki kuwa ni jambo baya na la haramu hata kama ni wengi wenye kuifanya haramu hiyo. Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

0754 678 252
mjengwamaggid@gmail.com
http://mjengwa.blogspot.com


Kutoka gazeti la Raia Mwema wiki hii


No comments: