Saturday, March 01, 2008

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI

YA MUUNGANO WA TANZANIA,

MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO

KIKWETE, KWA WANANCHI,

DAR ES SALAAM,
TAREHE 29 FEBRUARI, 2008



Ndugu Wananchi;

Mwezi tunaoumalizia ulikuwa wa aina yake kwa nchi yetu na kwa nchi jirani na rafiki ya Kenya. Ulikuwa mwezi wa matukio makubwa ya kukumbukwa kwa miaka mingi ijayo. Matukio ambayo yatapata nafasi yake katika historia ya nchi yetu. Jambo la kwanza ni lile linalohusu kikao cha Bunge kilichopita, ambapo utekelezaji wa maamuzi yake yanasimamiwa na Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda. Jambo la pili ni lile la kupokea ugeni mkubwa wa Rais wa Marekani, Mheshimiwa George W. Bush alipotembelea nchi yetu kuanzia tarehe 16 mpaka 19 Februari, 2008. Jambo la tatu ni kutiwa saini kwa mkataba wa kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini Kenya kulikofanywa jana.

Napenda kuitumia nafasi hii kuwashukuruni Watanzania wenzangu hasa wa mikoa ya Dar es Salaam na Arusha kwa jinsi tulivyompokea vizuri sana mgeni wetu Rais George Bush na mkewe Mama Laura Bush pamoja na ujumbe wao. Hii ni mara ya kwanza kwa nchi yetu kumpokea Rais wa Marekani kwa ziara ya kitaifa. Ugeni wa Rais wa Marekani katika nchi yoyote duniani huwa na ugumu wake na uzito wa aina yake hata kama ni wa saa chache. Kwetu sisi amekuwepo kwa siku nne na kutembelea maeneo mawili: Dar es Salaam na Arusha. Ugumu na uzito wake haukuwa mdogo hata kidogo.

Lakini, pamoja na yote hayo mambo yalikwenda vizuri. Wageni wetu wameondoka nchini wakiwa wamefurahia sana mapokezi tuliyowapa. Ninyi wenyewe na dunia nzima ni mashahidi wa furaha aliyoionyesha kwa kipindi chote cha siku nne alichokaa hapa nchini. Kila mahali alikotembelea kiongozi huyo wa taifa kubwa duniani alionyesha wazi furaha yake kwa jinsi tulivyompokea. Alikuwa mwingi wa tabasamu na uchangamfu usio kifani. Alisalimia watu bila kubagua, na hata baadhi yetu alitukumbatia kwa furaha. Naamini wengi wetu hatukutegemea yote tuliyoyaona kwa jinsi dhana tuliyokuwanayo juu ya Rais George Bush kabla ya kumuona kwa karibu ilikuwa tofauti.

Hakika wageni wetu wameondoka nchini akiwa na kumbukumbu nzuri sana ya nchi yetu na watu wake. Nawashukuru sana viongozi wa Serikali Kuu na wa Mikoa ya Dar es Salaam na Arusha kwa uongozi wao mzuri kabla na wakati wa ziara hii. Hali kadhalika nawashukuru viongozi na wafanyakazi wa Hospitali ya Amana, Hospitali ya Meru na Kiwanda cha Vyandarua cha A to Z bila ya kuwasahau walimu na wanafunzi wa shule ya wasichana ya Emulsoi. Pia nawashukuru Mama Salma Kikwete na viongozi wenzake wa WAMA na viongozi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa maandalizi mazuri ya shughuli za Mama Laura Bush wakati wa uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kusaidia Watoto Yatima na utoaji wa gari la kubeba wagonjwa.

Ndugu Wananchi;

Napenda pia kutoa pongezi za kipekee kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri waliyoifanya kabla na wakati wa ziara ya Rais Bush hapa nchini. Vyombo hivi vilifanya kazi mchana na usiku katika kuhakikisha kuwa mgeni wetu huyo anakuwa salama muda wote wa ziara yake. Kazi hiyo haikuwa ndogo lakini waliitekeleza vizuri na hivyo kumwezesha mgeni wetu na ujumbe wake kukaa na kuondoka salama salimini. Kwa niaba yenu nyote navipongeza sana kwa kazi nzuri.

Kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania nawashukuru kwa gwaride lililofana. Mgeni wetu alisifu sana jinsi mistari ilivyooka na ukakamavu waliouonyesha wanajeshi wetu. Alitambua na kusifu weledi (professionalism) wa Jeshi letu.

Ndugu Wananchi;

Napenda pia kuvipongeza vyombo vya habari vya hapa nchini na vya nje kwa kazi nzuri waliyoifanya. Kupitia kwao wananchi wetu wote na watu wengi duniani kote waliweza kufuatilia kwa karibu ziara nzima ya Rais Bush. Naamini vile vile kuwa kazi yao haikuwa rahisi lakini waliifanya kwa ufanisi wa hali ya juu. Hawa wote wanastahili pongezi zetu za dhati kwa mchango wao muhimu uliofanikisha ziara hii.

Ndugu Wananchi;

Ziara ya Rais Bush barani Afrika imezua mjadala wa aina yake miongoni mwa watu wengi nchini, barani Afrika na hata duniani. Kumekuwepo na dhana kuwa Rais huyo alikuwa anatafuta nchi ya kuweka makao makuu ya Kamandi ya Afrika ya Jeshi la Marekani. Napenda kuwahakikishia wananchi wenzangu kuwa suala hilo halikujitokeza katika mazungumzo yetu. Lakini, pia haijapata kutokea wakati wowote katika mahusiano yetu na Marekani kuwepo kwa maombi ya namna hiyo kufikishwa kwa Serikali yetu. Nawaomba muondoe hofu kabisa kwani sikuiona hata dalili ya kupata maombi ya namna hiyo hivi karibuni na wala sioni dalili ya kuwepo maombi hayo siku za usoni.

Ndugu Wananchi;

Nilichojifunza mimi kuhusu madhumuni ya ziara ya Rais Bush katika Bara la Afrika pamoja na Tanzania ni nia yake ya kutaka kusisitiza agenda ya Serikali ya Marekani kuhusu misaada kwa Afrika. Kubwa zaidi ni lile la misaada katika mapambano dhidi ya maradhi ya UKIMWI na Malaria pamoja na juhudi za kupunguza umaskini barani Afrika. Rais Bush alikuja kuwathibitishia wananchi wa Marekani kuwa sera yao ya misaada Afrika ni sahihi na kwamba mafanikio yaliyotarajiwa yanapatikana. Kwa ajili hiyo, aliamua kukaa hapa kwetu kwa siku nyingi kwa sababu, katika misaada yao ya kupambana na malaria na UKIMWI barani Afrika, hapa Tanzania kumekuwepo na mafanikio ya kutolewa mfano.

Hivyo alikuja Tanzania kuona utekelezaji na programu zao ili awaonyeshe na kuwathibitishia viongozi na wananchi wenzake wa Marekani kwamba sera yao ya misaada kwa upande wa malaria na UKIMWI imepata mafanikio. Aidha, alitaka kuwathibitishia kuwa pesa zao zinatumika vizuri na kuutumia ukweli huo kuwashawishi wakubali kuendelea kuisaidia Tanzania na Afrika katika mapambano hayo.

Ndugu Wananchi,

Rais Bush analipa umuhimu mkubwa sana suala la Marekani kuendelea kuisaidia Afrika katika mapambano yetu dhidi ya umaskini, maradhi na ujinga. Kwa vile yeye sasa anamaliza kipindi chake cha mwisho cha uongozi, angependa kuona programu hizo zinaendelea kutekelezwa hata baada ya yeye kuacha madaraka. Ameona njia bora ni hii ya kufanya ziara ili yeye mwenyewe aone mafanikio yaliyopatikana na kupitia ziara yake wananchi wenzake waone ili wapate moyo wa imani wa kuendeleza programu alizozianzisha. Pia alikuja kutambua mahitaji zaidi ili Serikali yake isaidie. Matokeo ya hayo ni ule uamuzi wa msaada wa vyandarua milioni 5 ambao haukuwepo katika mpango wao wa awali.

Ndugu zangu, Watanzania wenzangu;

Ni jambo la kutia faraja kwamba Rais George Bush na Serikali ya Marekani kwa jumla wameridhika na utekelezaji wa programu za UKIMWI na Malaria tunaoufanya hapa nchini. Hatuna budi kujipongeza kwa sifa hiyo. Hata hivyo, lazima tuazimie kuwa tutajitahidi kufanya vizuri zaidi. Kamwe tusirudi nyuma. Daima tusonge mbele. Kwa ajili hiyo, tuwafichue wale wenzetu wanaofanya vitendo viovu kinyume na misingi ya uadilifu.

Imani huzaa imani. Kuridhika kuwa fedha zao zinatumika vizuri ndiko kulikomfanya Rais Bush na Serikali yake kukubali kuipatia nchi yetu misaada zaidi. Kama tujuavyo, wakati alipokuwepo nchini tulitiliana saini mkataba wa kuipatia Tanzania dola za Kimarekani 698 milioni za kuendeleza ujenzi wa miundombinu nchini chini ya Mpango wa Changamoto za Milenia. Pia alitupa ahadi ya kutupatia vyandarua milioni 5 zaidi kwa ajili ya watoto.

Ndugu Wananchi;

Msaada uliotolewa chini ya Mpango wa Changamoto za Milenia utasaidia ujenzi wa barabara za Tunduma - Sumbawanga, Tanga - Hororo na Namtumbo – Songea – Mbinga kwa upande wa Tanzania Bara. Kwa upande wa Zanzibar barabara kadhaa zitatengenezwa. Vile vile utatumika kukijenga kiwanja cha ndege cha Mafia ili ndege kubwa ziweze kutua usiku na mchana. Kwa upande wa umeme msaada utatumika kujenga kituo cha kuzalishia umeme katika Mto Malagarasi. Umeme huo utatumika Kigoma na Kasulu hivyo kuondoa tatizo la muda mrefu la umeme usiotosheleza mahitaji mjini Kigoma na tatizo la miji ya Kasulu na Uvinza kukosa umeme.

Kadhalika, usambazaji wa umeme utaimarishwa katika mikoa ya Tanga, Morogoro, Dodoma, Mwanza, Iringa na Mbeya. Kupitia msaada huo pia ujenzi wa mradi wa kupitisha umeme wa chini ya bahari kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar utatekelezwa. Mradi huo utaongeza umeme kwa kisiwa cha Unguja hivyo kuimarisha upatikanaji wa umeme. Kwa miji ya Dar es Salaam na Morogoro huduma ya upatikanaji maji itaboreshwa hivyo kupunguza ukali wa tatizo la upungufu wa maji katika miji hiyo.

Ndugu zangu;

Rais Bush alipokuwa Arusha alitangaza uamuzi mpya wa kutoa vyandarua milioni 5 kwa watoto. Vyandarua hivyo vitatolewa bure tofauti na ilivyo sasa ambapo hulipiwa ingawaje kwa bei ndogo kwa sababu ya kuwepo ruzuku. Msaada huu unajibu hoja yetu kwamba ili tufanikiwe kumaliza tatizo la malaria nchini moja ya hatua za kuchukua ni kutafuta njia ya kuwawezesha Watanzania wengi kupata vyandarua vilivyotiwa dawa inayoua mbu bure. Nimefurahi kwamba kilio chetu kimepata sikio sikivu la Rais George Bush wa Marekani. Tayari tumepata hivyo vyandarua milioni 5, tunaendelea kutafuta vyandarua vingine zaidi ya milioni 15 ambavyo vikipatikana hoja yetu itakuwa imepatiwa ufumbuzi. Nina matumaini makubwa kuwa Mwenyezi Mungu atatusaidia tutafanikiwa. Dalili ni nzuri.

Ndugu Wananchi;

Napenda kwa niaba yenu, nimshukuru tena Rais George Bush kwa moyo wake na upendo wake kwa watu wa Bara letu la Afrika na kwa misaada ya Serikali yake kwa Tanzania. Ukiacha misaada mipya tuliyopata wakati wa ziara yake, Serikali ya Marekani ni moja ya mataifa wafadhili yanayotupatia misaada mikubwa ya maendeleo katika nyanja mbalimbali hapa nchini.

Wakati tunamshukuru Rais Bush kwa misaada hii mikubwa hatuna budi kutambua wajibu wetu wa kuhakikisha kuwa misaada hiyo inatumika vizuri na kwa malengo yaliyokusudiwa. Huu ni wajibu wetu wa msingi kwetu wenyewe na ni wajibu wetu wa msingi kwa wale wanaotusaidia. Hatuna budi kuutimiza.

Ndugu Wananchi;

Jambo la pili, ninalopenda kulizungumzia siku ya leo ni makubaliano yaliyotiwa saini jana mjini Nairobi, Kenya baina ya Mheshimiwa Rais Mwai Kibaki wa nchi hiyo na Mheshimiwa Raila Odinga, Kiongozi wa Chama cha ODM cha nchi hiyo. Makubaliano ya ushirikiano wa vyama vya ODM na PNU katika uongozi wa taifa la Kenya. Kama sote tujuavyo nchi jirani na rafiki ya Kenya iliingia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa, ghasia na matatizo ya kiusalama kufuatia uchaguzi mkuu wa Desemba 27, 2007.

Kufuatia machafuko na ghasia zilizotokea, mali nyingi zimeharibiwa, zaidi ya watu 1,000 walipoteza maisha na wengine zaidi ya 300,000 wamekuwa wakimbizi ndani ya nchi yao. Wapo pia baadhi ambao wamekuwa wakimbizi katika nchi jirani. Ghasia hizo zilizokuja kuwa kati ya watu wa makabila mbalimbali ya nchi hiyo zaidi ya kuwa kati ya wafuasi wa vyama vya siasa, zimeathiri sana upendo, mshikamano na umoja wa watu wa Kenya. Kadhalika zimekuwa na athari kwa uchumi wa Kenya na uchumi wa nchi zetu jirani na Kenya.

Juhudi za kutafuta suluhisho la mgogoro huo zilianza mara baada ya kuzuka kwake. Juhudi hizo zimekuwa zinapata mafanikio ya kutia moyo, lakini jana, yale yaliyokuwa yakisubiriwa kwa muda mrefu yalitimia. Agenda ya kusimamisha machafuko na mapigano baina ya wana-Kenya na juhudi za kushughulikia tatizo la huduma kwa wakimbizi wa ndani zilishakamilika na utekelezaji wake unaendelea. Jana agenda ya namna ya kutatua mgogoro ikakamilika baada ya Rais Mwai Kibaki na Mheshimiwa Raila Odinga kukubaliana na kuthibitisha makubaliano yao kwa saini zao. Kilichobaki ni utekelezaji wake.

Ndugu Wananchi;

Hatua ya jana ni mwanzo wa mchakato wa kuitoa Kenya kwenye mgogoro wa kisiasa na kuihakikishia misingi imara ya amani na utulivu. Naomba Watanzania wenzangu tuwatakie heri na kuwaombea ndugu zetu wa Kenya watekeleze kwa ukamilifu makubaliano ya jana na yale ya nyuma ili waiondoe nchi yao kwenye matatizo yaliyokuwepo. Ni kazi ngumu lakini sasa inawezekana kufanyika.

Makubaliano ya jana ni jambo la faraja kubwa kwa wananchi wa Kenya na kwa Watanzania pia. Kwa Wakenya inaashiria mwanzo wa mwisho wa hali ngumu, hali ya wasiwasi na hali ya hatari waliyokuwa nayo kwa takriban miezi miwili sasa. Watu sasa wanapata uhakika wa usalama wa maisha yao, mali zao na shughuli zao. Wananchi wa Kenya wanapata fursa ya kujenga upya pale palipo haribika.

Kwa Watanzania ni jambo la faraja kwetu kwamba matatizo yaliyokuwa yanamkabili jirani mwema na rafiki yamepatiwa ufumbuzi. Jambo lingine la faraja ni kwamba katika kupatikana kwa suluhu ya Kenya na sisi Watanzania tumetoa mchango wetu. Mchango mkubwa ni ule alioutoa Rais Mstaafu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa tangu mwanzo wa mchakato huo na bado anaendelea. Na, huku mwishoni ni ule mchango nilioutoa mimi. Ni bahati iliyoje kwa nchi yetu kupata nafasi ya kumsaidia jirani wakati wake wa shida.

Watanzania Wenzangu;

Wakati tukiwapongeza Wakenya kwa mafanikio yaliyopatikana na kuwapa pole kwa magumu yaliyowakuta yatupasa kujiuliza mafunzo gani tunayopata. Mafunzo hayo ni muhimu ili tujiepushe na kasoro zilizowafikisha hapo. Kwa maoni yangu, fundisho kubwa sana tuliloliona ni kuwa kuendeleza ukabila ni jambo hatari sana kwa taifa. Bahati nzuri, katika nchi yetu tatizo la ukabila halipo, lakini linaweza kuwepo tusipokuwa waangalifu kwa vile makabila yapo. Nawasihi, ndugu zangu, tusiwape nafasi wale wote wanaofanya vitendo vinavyoweza kuturudisha kwenye ukabila.

Lakini, kwa nchi yetu lililo hatari la kujiepusha nalo si la ukabila tu, lipo la udini na yapo masuala ya ubaguzi mwingineo. Kenya hawakuwa na tatizo la udini lakini la ukabila lilitosha kuivuruga nchi. Je, kama lingeongezeka na tatizo la udini ingekuwaje? Tufanye kila tuwezavyo tuhakikishe kuwa tunapiga vita kwa uwezo wetu wote vitendo, fikra au hata mwelekeo tu unaoweza kutugawa kwa misingi ya makabila yetu, dini zetu, rangi za ngozi zetu, maeneo tutokako na mengineyo. Wale wenzetu wanaotaka kutupeleka kubaya tusiwape nafasi. Tusivumilie kauli zao za uchochezi au matendo yao ya kibaguzi. Misingi iliyowekwa na waasisi wa taifa letu hususan hayati Mwalimu Julius Nyerere na hayati Abeid Amani Karume daima tuienzi. Tukiipuuza ole wetu.

Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa Kunisikiliza.


No comments: