*Waziri Nishati anaswa ofisini kwao usiku
*Katibu Mkuu akiri alionya, akapuuzwa
Na Hassan Abbas
*Katibu Mkuu akiri alionya, akapuuzwa
Na Hassan Abbas
HUKU wakionekana kuwa na ujasiri wa aina yake na uthubutu ambao chanzo chake kinapaswa kufanyiwa uchunguzi zaidi, baadhi ya vigogo waandamizi serikalini sasa imezidi kuthibitika jinsi 'walivyoamua kufa,' kuhakikisha kampuni ya Richmond ya Kariakoo, Dar es Salaam, ikijinasibu kutoka Houston, Marekani, na kupata kila ilichokitaka katika zabuni ya umeme wa dharura, Majira Jumapili limebaini.
Kwa mujibu wa taarifa za mashahidi kadhaa walionukuliwa kwenye ripoti rasmi za Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dkt. Harrison Mwakyembe, nyendo za vigogo wengi serikalini wakati wa mchakato wa kuipa Richmond tenda, zilijaa mashaka.
Nyendo hizo zilistaajabisha na zilioonekana kulenga, kwa gharama yoyote, kufikia jambo moja adhimu; iwe isiwe, Richmond inapata ilichokitaka.
Saa tano usiku ofisi za Richmond
Akihojiwa na Kamati hiyo, gazeti hili limebaini, mmoja wa mashahidi muhimu walioifahamu Richmond, wakili Tahir Muccadam ambaye ni mmiliki wa jengo ambalo Richmond waliwahi kupanga na kuweka ofisi zao kabla ya kuvurumushwa kwa kushindwa kulipa pango, amemtaja Waziri Mwandamizi kuwa alikuwa akionekana mara nyingi kwenye ofisi za kampuni hiyo nyakati za usiku.
Waziri huyo ambaye wakili huyo alimtaja kuwa ni wa Nishati na Madini na alipoulizwa ni Msabaha (Dkt. Ibrahim), alifafanua kuwa ni yule aliyewahi kuingia matatizoni na aliyekuwa Marekani. Bw. Nazir Karamagi ndiye aliyechukua nafasi ya Dkt. Msabaha kwenye Wizara hiyo.
Bw. Muccadam akaiambia Kamati kuwa Waziri huyo alikuwa akifika kwenye ofisi hizo zilizokuwa Muccadam House, Upanga, Dar es Salaam akitumia gari binafsi na kwamba walinzi wa ofisi mbalimbali zilozoko kwenye jengo hilo walikuwa wakimuona na kumbaini.
Sehemu ya mahojiano kati ya wakili Muccadam na wajumbe wa kamati hiyo ilikuwa hivi:-
Lucas Selelii: Lakini kuna habari nyingine tumezipata kwamba kwa influence ya kwako ya uanasheria na influence ya Mzee uliwapa contact kupita milango, mikubwa mikubwa ambayo siyo rahisi kuingia kwao, ndiyo ulisaidia kuwafungulia milango kwa maana ya wakubwa.
Tahir Muccadam: Mheshimiwa Mwenyekiti sijaelewa kwa vipi, make it more clear (fafanua).
Lucas Selelii: Kwa sababu ulimpokea Naeem (Gire, ambaye ndiye Mkurugenzi wa Richmond upande wa Tanzania) na umekuwa naye siku zote (akiwa mpangaji) na unamfahamu(walicheza na kusoma pamoja).
Kwa kutumia ile hadhi uliyonayo ya uanasheria na ya mzee marehemu (Mzee Muccadam aliyekuwa wakili maarufu wa CCM na viongozi kadhaa), uliwasaidia kuwatambulisha katika maeneo makubwa makubwa ya watu wakubwa. Unakumbuka kitu cha namna hiyo?
Tahir Muccadam: Mheshimiwa Mwenyekiti, Naeem alikuwa ananiambia wanatafuta ofisi na kuna jenereta wanataka kuleta, sijui nasikia kuna watu mbalimbali watawapa commission sijui tenda kitu kama hivi.
Na wakadeal sijui na Mkurugenzi wa TANESCO lakini picha hasa ninavyoona mimi kutokana na maoni yangu mpaka kupata ile contract, nahisi probability, Im not so sure, lakini nahisi labda Waziri wa Nishati na Madini anaweza akawa ame-involve sana.
Lucas Selelii: Bw. Msabaha au huyu wa sasa (wakati huo Nazir Karamagi)?
Tahir Muccadam: Yule ambaye alikuwa katika zile problem, sijui alikwenda Marekani. Unajua Naeem alikuwa mtu wa kujisifu (proud). Nimepata tenda na hivi na nini, Waziri anakuja kunitembelea. Halafu kuna ushahidi Waziri alikuwa anakuja saa nne usiku, saa tano usiku pale kwetu, usiku mara nyingi.
Lucas Selelii: Pale kwako au kwa Neem?
Tahir Muccadam: Ofisini pale
Lucas Selelii: Upanga?
Tahir Muccadam: Upanga, na walinzi wapo ambao tulishuhudia, tulimwona watu wote. He has to come many times (alikuwa akija mara nyingi). Wanapigiana simu wenyewewe, wanakutana.
Lucas Selelii: Lakini wewe ni mwanasheria, hivi ni kitu cha kawaida kweli Waziri kwenda kwenye...!
Tahir Muccadam: Na mimi I a m also surprised, maana yake nashangaa na system mtu Waziri una ofisi yako mwenyewe... unakwenda katika ofisi kama ile ya Richmond, I am very surprised.
Waziri ataka kumwaga fedha
Mbali na ushahidi huo mzito wa wakili Muccadam, sakata la vigogo kuonekana kuwa tayari 'kufa na Richmond,' linaonekana kuwa na mtandao mpana unaorejea hadi enzi za utawala wa Awamu ya Tatu, ambapo ndipo kampuni hiyo ilipoingia rasmi nchini mwaka 2004 na kupewa katika mazingira tata, mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Aliyeanika zaidi ukweli juu ya Richmond kubebwa ni mmoja wa maofisa wa kampuni ya AFRICOMMERCE ambayo ndiyo iliyobuni na kupewa kazi ya awali ya mradi huo kabla ya kupokwa na kupewa Richmond, Bw. Eliapenda Chuwa wakati akihojiwa na Kamati ya Mwakyembe.
"Tulikwenda kumlalamikia (baada ya kupokwa mradi huo) Mheshimiwa Daniel Yona (wakati huo akiwa Waziri wa Nishati na Madini) ofisini kwake...Yeye akasema tutawapeni hela. Sasa utupe hela tumekwambia tunahitaji hela?
Akinukuliwa tena katika ukurasa wa 951 wa taarifa rasmi za Kamati hiyo, Bw. Chuwa aliiambia Kamati hiyo: "Waziri Danieli Yona tulipomwuliza kwa nini unafanya vitu vya namna hii akasema ninyi nendeni tutawapa hela, sasa hatujui kwamba zinatoka wapi."
Katika hatua nyingine yenye utata juu ya uadilifu wa watendaji serikalini na katika kile kinachoweza kusisitizwa tena kuwa mkakati mpana usioshikika wala kukamatika wa vigogo kuhakikisha Richmond inakipata kila inachokitaka.
Mkurugenzi Mkuu wa AFRICOMMERCE, Bw. Elisante Muro naye akitoa ushahidi wake kwenye Kamati ya Mwakyembe ananukuliwa akisema Bw. Yona alidiriki hata kuwapatia Richmond nyaraka zao za siri ili ziwasaidie.
Akinukuliwa katika ukurasa wa 952 wa taarifa za Kamati hiyo, Bw. Muro anakieleza kitendo hicho cha kutia shaka cha utendaji wa kigogo huyo akisema: "Kampuni moja inaitwa ENERGEM ya Canada tulikutana nao, wakatuandikia kwamba wana uwezo na wangependa kuuendeleza huu mradi wakishirikiana na AFRICOMMERCE.
"Out of our goodwill (kwa nia njema) tukamwonyesha Waziri Daniel Yona kwamba yupo mtu ambaye huu mradi utatekelezwa na kampuni iliyobobea. Akachukua ile barua akawapelekea Richmond, wakaenda kwa wale wawekezaji wetu Energem wakawaambia ule mradi ni wetu (wa wao Richmond) kwa hiyo kama mnataka pitieni kwetu."
Rutabanzibwa apuuzwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, ambaye aliwahi kuwa kwenye Wizara ya Nishati na Madini wakati Richmond waliposhindwa kutekeleza mradi wa bomba la mafuta na anayeijua vyema kuwa ni kampuni ya kisanii, Bw. Patrick Rutabanzibwa naye ametoa kauli mbele ya Kamati ya Mwakyembe inayozidi kuthibitisha kuwa kuna watu waliamua kufa na Richmond.
Akinukuliwa kwenye Kamati hiyo, Rutabanzibwa, alisema:
"...Nakumbuka nilipopata habari kwamba Richmond Development Company ndio wamepewa ule mradi mara moja nilimpigia simu Kamishna wa Nishati, Ndugu Bashir Mrindoko nikamwuliza nikisema nimesikia Richmond ni wale wale tuliokuwa nao au vipi?
"Akanieleza kwamba ni wale wale, nikasema sasa imekuwaje, lazima kuna matatizo huko kwenu."
Bw. Rutabanzibwa akaendelea kueleza juu ya suala hilo akisisitiza:
"Ninakumbuka taarifa ilipokuja (kwenye Kamati ya Makatibu Wakuu wa Wizara za Serikali), kwamba Richmond Development Company ndio wamepewa huo mkataba... Niliungwa mkono na wenzangu wengi kwamba tutafute kila njia kuachana nao,.." .
"...Na ushauri niliotoa kwenye kikao cha MCT (Makatibu Wakuu) ni kwamba hawa tunawajua hawana uwezo technically (kiufundi) au financially (kifedha)."Maoni hayo ya Rutabanzibwa yakapuuzwa, Richmond wakapewa mkataba na kukipata walichokuwa wakikitaka.
Mkurugenzi TANESCO naye anena
Akizidi kuongeza nguvu katika dhana kuwa kuna watu walikuwa tayari kufa ili Richmond ipate ilichokuwa ikikitaka, mmoja wa waliokuwa Wakurugenzi wa TANESCO wakati wa kusainiwa kwa mkataba huo, Bw. Yohanes Hans, raia wa Afrika Kusini alisema kuwa madai kwamba Richmond ilipewa tenda hiyo kwa sababu ya kuwa na bei ya chini kuliko kampuni zote ni uongo.
Aliiambia Kamati kuwa kampuni ya Songas ilikuwa imeshakubali kuikodisha TANESCO mitambo ya umeme, kwa bei ya chini zaidi ya Richmond na ambayo TANESCO wangeiendesha wenyewe (bila kulazimika kulipa capacity charges kama sasa ambapo Richmond inalipwa sh. milioni 152 kwa siku; izalishe umeme, isizalishe).
Lakini, kwa mujibu wa taarifa ya Bw. Hans, wakati Songas pia walikubali kuuza umeme wao TANESCO kwa senti 3.84 kwa yuniti (tofauti na Richmond wanaouza kwa senti 4.99 kwa yuniti), kama kawaida, vigogo wa Serikali 'waliamua kufa na Richmond,' ili kuhakikisha, kama ilivyopangwa, kampuni hiyo inakipata ilichokitaka na Songas wakaachwa.
Mtoto wa Sokoine asaidia
Katika kuonesha kuwa wapo Watanzania ambao kwa upande mwingine wamepania kuhakikisha kuwa ubinafsi na uzembe Serikalini unakomeshwa, wakati vigogo kadhaa wakiumbuliwa kwa kuonekana walishiriki kuhakikisha Richmond inakipata kila ilichokitaka, wapo maofisa Serikalini ambao pia walihakikisha kampuni hiyo inajulikana ukweli wake halisi.
Mmoja wa waliosaidia hilo ni mtoto wa aliyekuwa Waziri Mkuu na mbunge wa zamani wa jimbo la Monduli. hayati Edward Moringe Sokoine, Bw. Joseph Sokoine ambaye ni Ofisa Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani anayeshughulikia masuala ya Siasa, Biashara na Utalii.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati, wakati baadhi ya wajumbe walipokwenda nchini Marekani kujua ukweli kuhusu Richmond, Bw. Sokoine alikuwa mmoja wa maofisa waliotoa msaada mkubwa na kuwaongoza wanakamati hao.
Kamati hiyo ilipokuwa nchini Marekani ndiko ilikofanikiwa kubaini kuwa Richmond haikuwa imesajiliwa na wala haikuwa na ofisi na wala haitambuliki miongoni mwa makampuni ya nishati yaliyoko Houston, Texas.
Hata hivyo, hivi karibuni Bw. Yona alikaririwa na vyombo mbalimbali vya habari akikana kuhusika katika sakata hilo la Richmond.
No comments:
Post a Comment