Saturday, March 01, 2008

Mapenzi ya simu




NAAM wapenzi wa kona yetu mantashau ya mabaha, kama kawaida yetu tumekutana tena kwenye kona yetu ili kujuzana machane yahusuyo mapenzi. Baada ya mada yetu ya wiki mbili zilizoshabihiana kwa namna moja au nyingine. Leo tumekuja na mada nyingine isemayo mapenzi ya simu.

Nimepata maswali mengi yahusuyo mapenzi ya simu, mapenzi ya simu yamefanya nini?

Tekinolojia ya mawasiliano kwa njia ya simu imeturahisishia mambo mengi, lakini kwa wengine, wamekuwa wakiitumia vibaya. Simu ndiyo imekuwa ikificha maovu mengi kwenye mapenzi. Kwa vile unayezungumza naye hamuonani. Basi utamdanganya kuwa unampenda na maneno yote mazuri utamwambia.

Kwa vile unamuamini mpenzio utakubaliana naye, na kuona katika watu wanaopendwa wewe ni mmoja wapo. Tatizo linakuja pale utakapokutana uso kwa macho, yote yalizungumzwa kwenye simu huyeyuka. Unajikuta unashangaa na kujiuliza yale maneno ya nakupenda kuliko maelezo yapo wapi? Ajabu hata muda wa kuongea unakosekana, ooh nipo bize ooh baba mkali. Lakini kwenye simu vyote hivyo havikuwepo.

Wengi wamejikuta wakikosa majibu kutokana na yanayojitokeza kwa wapenzi wao pale wanaposhindwa kuonyesha mapenzi kwa vitendo. Hii inatokana na watu kushindwa kuelewa matumizi ya simu. Simu ni chombo cha mawasilianona si chombo cha kumgeuza mwenzio katuni kwa kudanganywa "Nakupenda" kumbe unaye umpendaye kwa dhati.

Vilevile wanaokumbwa na matatizo haya ni wale wenye hamu ya kuelezwa naneno matamu kwa njia ya simu. Mpenzio anaweza kusema anakupenda kuliko kitu chochote kwenye dunia hii. Lakini kumbe muda huo yupo kifuani kwa mpenzi mwingine.

Mimi nafikiri ifike wakati watu wajue mapenzi si maneno matamu bali vitendo. Usikubali kubembelezwa kwa maneno matamu yasiyo na ukweli bali ni tambara la kukuziba usoni, kutumia simu kama kichaka cha kuficha maovu yake.

Lazima ajue kila lenye mwanzo lina mwisho wake, ya nini kutumia simu kuonyesha mapenzi ya uongo?Si wote wanaokubali kutapeliwa, wapo wasiokubali na kujikuta ukijivunjia heshima kwa watu wanaokufahamu. Kama umeoa au umeolewa kuwa mkweli kwa kutumia simu kuficha maovu yako haitasaidia kitu.

Wengi wamekuwa malimbukeni wa simu kugawa namba ovyo ili mradi apate wa kumpigia simu. Hapo hapo unakuwa muongo kwa wengine kutumia simu kumdanganya mtu kwa kusema anampenda ili aingiziwe vocha.

Ipo siku vocha hizo zitakutokea puani, kwa wanaume zaidi ya watano kila mtu kutaka penzi kwako. Kibaya wewe ni mke wa mtu na wote kwa njia ya simu uliwaambia unawapenda kama ubwabwa mandondo.

Sina haja ya kuwasema watu, la muhimu ni kukumbushana hakuna mapenzi kwa njia za simu zaidi ya kudanganyanya. Na mapenzi ya kweli si maneno matamu bali vitendo. Neno nakupenda liendane na matendo kuonyesha kweli unampenda mwenzio.

Vilevile mapenzi si lazima mlindane kama polisi na kibaka. Hata kama mwenzio hayupo karibu nawe jaribu kuwa mkweli na kuwa mwaminifu. Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo kwa upande wa pili wa mada hii yaani Penzi la mbali.

Kwa maoni ushauri au maswali nitwangie kwa Tel:0713 646500 au Email: ambedkt@yahoo.com

No comments: