Saturday, March 01, 2008

Na Richard Manyota

Skendo ya Kampuni hewa ya kuzalisha umeme ijulikanayo kwa jina la Richmond, imefikia patamu baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Pius Msekwa kuibuka na kumbeba aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa...

Habari zilizokusanywa na Risasi zimebaini kuwepo mwelekeo wa Lowassa kubebwa na Msekwa kufuatia kauli ya kigogo huyo wa CCM iliyotetea juhudi za watuhumiwa akiwemo waziri mkuu aliyejiuzulu, kujisafisha wakiwa nje ya bunge.

Msekwa alisikika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, akisema kuwa hakuna ubaya kwa ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza sakata la Richmond kukosolewa nje ya chombo hicho cha kutunga sheria nchini (bunge).

Matamshi hayo ya kiongozi huyo wa juu wa CCM yamezua mjadala na mshangao miongoni mwa wananchi ambao walisema yana lengo la kumtia nguvu Lowassa na wenzake wazidi kujikosha wakiwa nje ya bunge.

Wakati Msekwa akiwatetea watuhumiwa, Spika Samweli Sitta alipingana naye kwa kusema ni kinyume cha kanuni za bunge kwa mtu kuikosoa ripoti hiyo na kuwataka wenye hoja akiwemo Lowassa kuziwasilisha bungeni ili zijadiliwe upya na kamati husika.

“Kama Lowassa alikuwa na jambo la kusema angesema wakati huo, sio leo tena nje ya bunge,” alisema Sitta akipinga staili ya kujikosha inayotumiwa na waziri mkuu huyo aliyejiuzulu, kujitetea mbele ya umma kuwa kamati ilimnyima uhuru wa kujieleza kutokana na kutomhoji.

Sitta aliongeza kuwa ameiagiza kamati ya maadili ya bunge kuzisaka kwa udi na uvumba kanda na nyaraka zenye kauli ya viongozi wanaotumia majukwaa na vyombo vya habari kueleza dosari za ripoti hiyo ili ikijulikana kama wamekejeli na kutishia hadhi ya bunge waitwe na kubanwa.

Tangu kuzuka kwa sakata hilo lililowatia ‘kifungoni’ baadhi ya mawaziri, watendaji wa serikali wanaonyooshewa vidole na wapambe wao, wamekuwa katika mikakati ya kujaribu kupoza lawama zinazosemwa juu yao kuhusu ufisadi ‘walioutenda’ kwa taifa.

Hata hivyo, moto wa Richmond unaonekana kukua karibu kila siku kutokana na viongozi wa ngazi za juu wa chama na serikali kuibuka na kauli kinzani juu ya namna ‘mafisadi’ wanavyostahili kubanwa na nguvu za dola.

Baadhi ya viongozi wa serikali wamekuwa wakishinikiza ripoti ya tume ya kamati teule ya bunge iliyokuwa chini ya Dk. Harrison Mwakyembe itoshe kuwahukumu waliohusika huku wengine wakiingiza huruma, kutaka itazamwe namna ya ‘kuwapepea’ waliohusika.

Aidha, wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanaopitia matamshi ya viongozi ‘waliong’atwa’ na ripoti ya Mwakyembe na wale wa kambi ya fagio la serikali, wanabashiri kuwepo kwa mgawanyiko mkubwa ndani ya chama tawala na serikali yake.

Akihojiwa na Kituo cha Televisheni ya Taifa (TVT), katika kipindi maalumu kinachodaiwa kukatizwa kwa agizo la vigogo wa serikali, Lowassa alikaririwa akitoa kauli tata zilizoonesha msimamo wake wa kuonewa na kamati teule ya bunge.

Akieleza namna alivyobanwa na wabunge wa chama chake alisema: “Miongozo ya vyama vingi vya siasa duniani kote inataka kukosoana miongoni mwa wanachama wake kufanyike kwenye vikao si ndani ya bunge,” alimalizia bila kuweka wazi zaidi.

No comments: