Thursday, March 06, 2008

Ukabila na Richmond:

Tusisubiri maji yazidi unga



Evarist Chahali, Uskochi

KATI ya mambo yaliyonivutia katika hotuba ya mwisho wa mwezi uliopita ya Rais Jakaya Kikwete ni pale alipowakumbusha Watanzania kutokutoa fursa kwa watu wanaotaka kupandikiza mbegu za ukabila katika jamii.

Aliyaongea hayo muda mfupi baada ya kushiriki jitihada (zinazostahili pongezi nyingi) za kuleta suluhu nchini Kenya. Ni kweli kabisa kwamba vurugu zilizokuwa zikiendelea Kenya zingeweza kuwa na madhara makubwa zaidi iwapo “virusi” vya ukabila vingeungana nguvu na vile vya udini.

Kama mwanasiasa mwenye uelewa mkubwa, Rais Kikwete hakutaja majina wala kutoa mifano hai kuhusu nani hasa walikuwa walengwa wa onyo hilo, lakini haihitaji taaluma ya uchambuzi wa hotuba kujua kuwa kiongozi huyo naye alishtushwa na kauli za mtu aliyempatia dhamana ya kuvutia wawekezaji, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji, Emmanuel ole Naiko, ambaye hivi karibuni alikaririwa akidai kuwa kutajwa kwake katika ripoti ya “Tume ya Mwakyembe” ni mithili ya mpango wa mauaji ya halaiki dhidi ya watu wenye asili ya Monduli.

Kuna nyakati huwa najiuliza inakuwaje watu wenye mawazo hatari kama hayo ya ole Naiko wanaweza kufikia hatua ya kukabidhiwa ofisi nzito kitaifa kama TIC. Mamlaka husika zinapaswa kumhoji kwa undani mtu huyu (mwenye heshima kubwa ndani na nje ya nchi) kutokana na matamshi hayo ambayo yanaweza kabisa kuathiri hata utendaji wa ofisi yake kwani hakuna mwekezaji aliye tayari kuja kuwekeza kwenye nchi inayoelekea kwenye ethnic cleansing.

Pengine kauli mufilisi kama hiyo ya ole Naiko zinatolewa hadharani bila uoga si kwa kigezo cha uhuru wa kutoa maoni bali kutokana na ukweli kwamba watoa kauli wanajua hawatachukuliwa hatua zozote za maana.

Japo nisingependa kulilaumu Bunge moja kwa moja,lakini nashawishika kuhoji kile kinachoweza kutafsiriwa kama “double standards” katika kulinda heshima na hadhi yake. Kauli zilizotolewa na baadhi ya watajwa wa ripoti ya “Tume ya Mwakyembe” ni sawa kabisa na kukidhalilisha chombo hicho muhimu kwa Taifa.

Naomba nifafanue:Kwa kudai tume hiyo ilikuwa na ajenda za siri ni sawa na kujaribu kutuaminisha kwamba uteuzi wa wajumbe hao uliofanywa na Bunge nao ulizingatia ajenda hizo za siri.Sasa kama Zitto Kabwe alisimamishwa ubunge kwa madai ya kulidhalilisha Bunge na hakupatiwa hata nafasi ya kujitetea iweje leo Edward Lowassa aliyepewa fursa ya kujitetea na akakimbilia kujiuzulu, asichukuliwe hatua kwa kauli zake za uchonganishi?

Kuna matatizo makubwa katika utekelezaji wa sheria baadhi ya tulizojiwekea wenyewe.Hivi kama watu wote waliotajwa kuhusika na mkataba wa kilevi wa Richmond wangekuwa wameshachukuliwa hatua zinazostahili, unadhani tungeendelea kusikia hizo ngonjera za kujisafisha majina? Na tutarajie nini iwapo mtu aliyelazimika kujiuzulu kutokana na kashfa anapoishia kupongezwa “kwa ushujaa” na kupokelewa kifalme bila kusahau fursa iliyotolewa na chombo cha walipa kodi,TVT, kusikiliza “rekodi iliyopaswa kuwekwa sawa” huko Bungeni Dodoma!?

Johnson Mwanyika, Edward Hosea na wengineo kadhaa waliotajwa kwenye ripoti ya Tume hiyo bado wako ofisini kana kwamba hawajaboronga lolote. Wakati tukiendelea kupiga kelele kuwa wawajibishwe, ni muhimu kujiuliza kwamba jeuri waliyonayo wanaipata wapi. Ni vema pia kuangalia iwapo jeuri hiyo haihamasishi watu walio safi kuamini kwamba “ufisadi unalipa” kwani ingekuwa kinyume na hivyo basi angalau muda huu tungekwisha kuona hatua fulani zimechukuliwa.

Mwisho wa makala hii nitatoa pendekezo kuhusu nini kifanyike pindi kunapotokea “kusuasua” kwenye kuchukuliwa hatua za haraka. Lakini kwa sasa ningependa kuwakumbusha wazalendo kama Mzee John Malecela na Kingunge Ngombale Mwiru kuwa hekima na busara zao zinahitajika zaidi wakati huu pengine zaidi ya vipindi vya kampeni za uchaguzi.

Wakongwe hawa wa siasa wako kimya kabisa kana kwamba hakuna linaloendelea kwenye anga za siasa za nchi.Ukimya wao unaacha maswali mengi kuliko majibu.

Wakati naandaa makala hii,kulikuwa na habari kwamba mapokezi ya Dk. Harrison Mwakyembe huko Kyela yalikuwa yakikumbana na vipingamizi mbalimbali kwa sababu zisizojulikana.Niseme hivi,huyu alipaswa kupokelewa kama shujaa wa Mkoa wa Mbeya na wananchi wote bila kujali tofauti zao za kiitikadi kwani uongozi wake kwenye tume ya Bunge ya kuchunguza sakata la Richmond umeupa sifa Mkoa wa Mbeya na kila Mtanzania mwenye uchungu wa dhati kwa nchi yake.

Vikwazo dhidi ya mapokezi yake ni mwendelezo tu wa siasa za chuki zinazoachiwa kushamiri mkoani humo.Na hilo linaturejesha tena kwenye tatizo la msingi la “kusuasua” katika kuchukua hatua za haraka kutatua matatizo yaliyo wazi.Kama Lowassa alipokelewa kishujaa huko Monduli kwa “ujasiri wake” kwanini iwe dhambi kwa Mwakyembe kupokelewa kishujaa kwa uzalendo wake?Ina maana kujiuzulu kutokana na kashfa ni suala lenye maslahi zaidi kwa wananchi kuliko kuongoza tume iliyofichua namna pesa za walipa kodi zinavyotafunwa kirahisi?

Msemo “kufanya kosa si kosa bali kurudia kosa” unaweza kuwa sahihi lakini vipi kama kosa hilo linaathiri maisha ya mamilioni ya Watanzania ambao pengine hawana uhakika wa kuwa hai kushuhudia kosa la mwanzo likirudiwa mara ya pili!? Nadhani ilipaswa kuwa hivi: kosa moja tulilofanikiwa kulifahamu liwe ni kichocheo cha kuitisha uchunguzi wa kina kuhakikisha kwamba hakuna makosa mengine lukuki yaliyofanyika kwa siri.

Kulalamika bila kutoa ushauri kuhusu nini kifanyike sasa si jambo bora sana kwani lawama pekee hazijengi.Wakati tunasubiri hatua za mamlaka husika dhidi ya wote waliotia Taifa hasara,ni muhimu kwa kila Mtanzania kutumia nafasi yake kuinusuru nchi. Hivi kweli hatuna wanasheria wenye uchungu na nchi wanaoweza “kununua kesi” dhidi ya mafisadi?Kutoa maoni ya kitaalamu kwenye vyombo vya habari ni kitu kizuri lakini kuchukua hatua za kisheria kwa niaba ya wananchi ni ujasiri uliotukuka. Makundi ya kijamii nayo yasiishie kukemea tu bali wafungue kesi dhidi ya mafisadi kwa niaba ya wananchi.

Kwa CCM,ushauri wangu kwao unaambatana na tahadhari.Chama hicho kikongwe kimeshajichanganya vya kutosha pale kilipong’ang’ania kudai kwamba chenyewe ndicho mwanzilishi wa hoja dhidi ya ufisadi.La muhimu si kuanzisha hoja bali kuchukua hatua stahili. Tahadhari yangu kwa CCM ni kuwa hizo tetesi tunazosikia kwamba kuna kundi jipya la “Agenda 21” zisichukuliwe kuwa ni hadithi za kuvuta muda.

Kuna watu wanaitaka Ikulu kwa udi na uvumba hata kama harakati zao hizo zitamaanisha kusambaratika kwa CCM au kuvunja utaratibu wa namna ya kumpata mgombea wa chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.Nyenzo za kuwadhibiti zipo lakini kama ilivyo ada, watu hawajali hadi maji yatapozidi unga usiku wa manane wakati maduka yameshafungwa.You have been warned!

Barua-pepe: epgc2@yahoo.co.uk
Blogu: http://chahali.blogspot.com

Kutoka Raia Mwema wiki hii



No comments: