
Basi
Na Mwandishi Wetu, Polisi
WATU watatu wamekufa katika matukio tofauti akiwamo mwanafunzi kutumbukia katika kisima cha shule na mwingine kugongwa na basi la Hood.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum Dar es Salaam, Jamal Rwambow amesema kuwa ajali ya basi la Hood imetokea jana saa 2 asubuhi, Ubungo Maji.
Amesema gari lililomgonga lilikuwa na namba za usajili T 469 AAZ aina ya Scania bus mali ya Hood lililokuwa likiendeshwa na Abdul Ally (44), aliyekuwa akitokea Ubungo kwenda Morogoro.
Amesema gari hilo liliacha njia na kumgonga John Elias (31), ambaye alikuwa akivuka barabara na alifia njiani wakati akikimbizwa Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu.
Pia, mwanafunzi wa darasa la tano kutoka shule ya Msingi Yombo Vituka Tumaini Prosper (13), amekufa baada ya kutumbukia ndani ya kisima kilichopo shuleni hapo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala Kanda Maalum Dar es Salaam, Faustine Shilogile amesema kuwa tukio hilo limetokea jana saa 7 mchana, Yombo Vituka.
Amesema mtoto huyo alikuwa akicheza na wenzake na kwa bahati mbaya alitumbukia ndani ya kisima hicho kilichochimbwa wakati wakijenga nyumba za walimu na alikufa baada ya kunywa maji mengi.
Naye, mkazi wa Bonde la Msimbazi Issa Mshami (35), amekutwa amekufa chumbani kwake huku akiwa amelala kitandani na hana jeraha lolote.
Kamanda Shilogile amesema kuwa tukio hilo limetokea jana saa 4 asubuhi, Bonde la Msimbazi.
Chanzo cha kifo cha mtu huyo bado hakijafahamika na polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi wa tukio hilo.
Maiti wamehifadhiwa chumba cha maiti Hospitali ya Mwananyamala na Amana na polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi wa matukio hayo.
No comments:
Post a Comment