Sunday, April 27, 2008


Kikwete acharuka


* Alimpa Chenge chaguo; kujiuzulu au kufukuzwa
* Hamad, Kilango, Sozigwa, Simba, Marmo, wanena
* Aagiza akaunti za vigogo zote nje zichunguzwe


na waandishi wetu


ALAMA za nyakati, ishara na matukio yanayoendelea katika siasa za Tanzania yanadhihirisha wazi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, emechukia na sasa ameamua kucharukia wote wenye kukinzana na maadili, sheria na kanuni za utawala bora.

Vita dhidi ya rushwa, aliyoianzisha siku 10 tu, baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Desemba 30, mwaka 2005, ni wazi sasa imeshika kasi.

Rais Kikwete alikemea vitendo vya rushwa, kuchota mali za umma, kuvuna na kulimbikiza utajiri usio na maelezo, na akaonya: “Tuwe waadilifu… tusilaumiane mbele ya safari," haya ni maneno ya Kikwete Desemba 30, mwaka 2005.

Kila kinachotokea sasa katika siasa za Tanzania hakuna kinachotokea kwa bahati mbaya. Kikwete tangu siku ya kwanza alipopewa fursa ya kuhutubia wananchi kupitia wawakilishi wake bungeni, alisema:

“Jambo hili linakera sana watu kuona mtu ambaye hana chochote, lakini miezi michache tu baada ya kuwa Mbunge au Waziri, Katibu Mkuu au Mkurugenzi, au mkuu wa idara, ana majumba ya fahari, madaladala, teksi bubu nyingi, anaishi maisha ya kifahari yasiyoelezeka,” alisema Kikwete katika hotuba hiyo kali iliyosifiwa kila kona ya duniani.

Pia alibainisha wazi kuwa asingemkingia kifua yeyote katika vita dhidi ya rushwa na upotoshaji wa maadili aliposema: “Maombi yangu kwa Tume ya Maadili ya Viongozi ni kuwa wasione haya kutuuliza jinsi tulivyopata mali tunazosema tunazo. Tusingoje mpaka mtu aje kulalamika. Nitawasaidia kujenga uwezo wa kufanya hivyo. Tuwe waadilifu, tusilaumiane mbele ya safari.”

Joto la kuwajibisha mawaziri na vigogo waliojirimbikiza mali isivyo halali ndani na nje ya nchi, litaendelea kuwachoma wengi. Baada ya Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, kujiuzulu taarifa zilizolifikia gazeti hili la Rai zinasema kuwa Rais Kikwete ameamuru ufanywe uchunguzi wa akaunti za Watanzania wote ndani na nje ya nchi kujua wanamiliki fedha kiasi gani na wamezipataje.

“Hii ni hatari. Uchunguzi huu ni mpana. Rais ameagiza akaunti zote zichunguzwe huko Marekani, Uingereza, Uswisi na mataifa yote ya Ulaya kuhakikisha tunajua fedha za nchi zinavujia wapi. Nia ya Rais ni kuhakiksiha kila mtu anapata halali yake… anataka fedha hizi ziwe hapa nchini ziendeleze uchumi wa taifa hili. Hana mpango wa kuwanyang’anya wenye fedha zao kihalali, ila zisizofahamika zimepatikanaje, itabidi wahusika wazitolee maelezo,” kilisema chanzo chetu.

Uamuzi huu ni mwendelezo wa msisitizo ambao amekuwa akiutoa mara kwa mara Rais Kikwete juu ya dhana ya kutenganisha siasa na biasara. Februari, mwaka huu, akiwa visisani Zanzibar, alisema bayana kuwa siasa si mahala pa kuchumia fedha, bali ni fani ya utumishi wa umma, hivyo akatoa wito wa kutenganisha siasa na biashara.

Matukio matatu ya hivi karibuni; kwa kuanzia na lile la Januari 9, mwaka 2008, Rais Kikwete alipoanza kukunjua kwa ufasaha makucha yake kwa kumfukuza kazi aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Dk. Daud Balali, yanaashiria mwelekeo mpya.

Hatua ya kumfukuza kazi Balali na kumteua Prof. Benno Ndulu, siku moja baadaye, aliichukua siku chache baada ya kuwa ameamuru aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, afikishwe mahakamani kwa tuhuma za udokozi wa Euro milioni tatu, karibu sh bilioni 4.5.

Mambo hayakuishia hapo. Rais aliruhusu uchunguzi wa Kampuni ya Kufua Umeme kutoka Marekani ya Richmond, ambayo matokeo yake yalisababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kuwajibika kwa makosa ya watendaji waliokuwa chini yake, akaamua kujiuzulu na hatimaye Baraza la Mawaziri likavunjwa.

Kikwete mara tu alipounda upya Baraza la Mawaziri, miezi miwili iliyopita alitamka bayana kuwa yeyote atakayekiuka maadili ya utumishi wa umma, asingesita kumwondoa serikalini na kwamba huo haukuwa mwisho wa kuvunja Baraza iwapo mambo yasingekwenda kama atakavyo.

Kabla vumbi halijatulia, zikaibuka habari za Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, kutuhumiwa kumilikia wastani wa dola milioni 1, karibu Sh. bilioni 1.2, kwenye akaunti ya kimataifa iliyopo Kisiwa cha Jersey nchini Uingereza.

Chenge mwanzoni alisema hawezi kujiuzulu na akakiita kiasi hicho cha fedha kilichopo kisiwani Jersey kuwa ni vijisenti. Inawezekana alikuwa anapima upepo. Kidole alichotumbukiza kwenye maji, amekuta ni ya moto muno na hayaogeki. Akajiuzulu.

Habari za uhakika Rai ilizozipata kutoka Ikulu, zinaeleza kuwa Rais Kikwete amemlazimisha Chenge kujiuzulu. Bila kujali iwapo fedha hizo kwenye akaunti zinatokana na rushwa ya ununuzi wa rada iliyofanyika mwaka 2002 au vinginevyo, inasemekana hoja iliyotumiwa na Rais kumtaka Chenge ajiuzulu, ni kwamba upepo hauruhusu Chenge kuendelea kutumikia katika wadhifa aliokuwanao.

Afisa aliye karibu na Rais Kikwete, aliliambia Rai wiki hii kama ifuatavyo: “Haya yanayotokea, hayatokei kwa bahati mbaya. Rais amedhamiria kufuta rushwa katika siasa za Tanzania. Ni mwendelezo wa nia yake thabiti ya kutenganisha siasa na biashara.

“Katika mabadiliko yoyote, hakuwezi kukosekana matatizo. Rais anajua wapo watu wenye kutaka kutumia fursa hii kisiasa na wapo watu watakumbwa (necessary casualties by accident)… Rais amelazimisha audited report ya serikali itangazwe hadharani, tunaoma vita dhidi ya rushwa yakiwamo haya ya EPA…

“Rais anataka nchi iwe na mfumo wa Utawala Bora. Operesheni kubwa kama hii, haijawahi kufanyika tangu uhuru. Mambo haya hayatokei kwa bahati mbaya,” alisema Afisa huyo Mwandamizi.

Uchunguzi wa Rai umebaini kuwa Rais Kikwete aliamua kutoa kibali cha kumchunguza Chenge, bila kusita akitekeleza kauli yake kuwa yeye ndiye Rais na urais wake hauna ubia na mtu yeyote kama ilivyodhaniwa na baadhi ya wakosoaji wake wakati anaingia madarakani.

Chanzo chetu kingine kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKUKRU), ambayo inashirikiana na Ofisi ya Uchunguzi wa Ubadhirifu (SFO) ya Uingereza, alisema fedha za Chenge hazihusiani na rushwa ya ununuzi wa rada, lakini alikataa kuingia kwa undani zimetoka wapi.

Mchumi anayeendesha shughuli zake katika jijini London, Dk. Steve Wilcock, ambaye amezungumza na Rai amedai kuwa ingawa yeye ni Mwingereza amekuwa akifuatilia mwenendo wa siasa za Afrika, na amemmwagia sifa Rais Kikwete.

“Nimefuatilia kwa miaka mingi siasa za Afrika, sijapata kuona nchi yoyote ya Kiafrika na hata nyingi zilizoendelea kwamba fedha zinaporwa na zinarejeshwa. Fedha zilizoporwa kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kurejeshwa na waliohusika ni maajabu. Kitendo cha watu kurejesha wastani wa sh bilioni 60 za EPA, kinanifanya niamini kuwa Kikwete ana nguvu za ziada, na inawezekana anaogopwa kweli,” alisema Dk. Wilcock.

Afisa anayefanya kazi Wizira ya Sheria na Mambo ya Katiba, alisema Rais Kikwete sasa emeipiga nchi pasi. Alisema hali inavyoendelea yeye ameshuhudia mazungumzo sasa yanabadilika kwa watumishi wa umma kutoka kusifia rushwa na kuanza kuigopa. “Watumishi wa umma sasa wanaogopa rushwa. Tunarejea enzi za Mwalimu (Julius) Nyerere si muda mrefu,” alisema.

Afisa Mwingine kutoka Ikulu, alisema anavyofahamu hali ilivyo, kufikia mwisho wa mwaka huu nchi itakuwa na mifumo ya utendaji itakayorahisisha utawala bora na kurejesha nidhamu ya utumishi iliyokwishapotea.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni Hamad Rashid Mohamed amesema kama serikali ina nia ya dhati ya kuondokana na ufisadi wa kutisha kwa viongozi wake, orodha ya mali wanazomiliki iwe wazi kwa kuonwa na kila mtu.

“Bado kuna maeneo mengine yanayotakiwa kuangaliwa kwa umakini na zaidi ni fomu ya kujaza mali za viongozi. Wakati umefika sasa fomu hizo kuwa wazi na siyo siri tena mbele ya wananchi. Kwani kinachojazwa ndani ya fomu hizo si kile kinachomilikiwa na kiongozi aliyepo serikalini,” alisema Hamad na kuongeza:

“Kama tunataka kuondokana na ufisadi wa kutisha inabidi fomu hizo zipitiwe kwa manufaa ya wanaongozwa. Kama kiongozi hataki kuweka fomu yake hadharani basi, hakuna kuingia ndani ya uongozi,” alisema.

Hamad alitonesha vidonda vya Watanzania pale alipokumbushia jeuri na kiburi cha viongozi wa serikali kinachoendelea kukua siku hadi siku:

“Wakati wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa wananchi walidhalilishwa kwa kuambiwa ni bora wale majani ili ndege ya Rais iweze kununuliwa. Leo katika utawala wa Rais Kikwete wananchi wanaambiwa mabilio ya shilingi ni sawa na vijisenti. Haya ni maneno ya kejeli na dharau kwa Watanzania wanaoishi katika dimbwi la umasikini,” alisema Hamad.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki CCM, Anne Kilango Malecela alisema angemshangaa Chenge kama angeendelea kung’ang’ania madarakani bila kujiuzulu.

“Unajua hili suala linafanyiwa uchunguzi kwa karibu na vyombo vya nje ya nchi. Sasa kama angeendelea kuwa madarakani bila kusoma alama za nyakati, hakika vyombo vinavyofuatilia suala hili vingeishangaa Serikali ya CCM kwa kuona kiongozi anayetuhumiwa kwa kashfa kama yake anaendelea kubakia madarakani,” alisema Killango na kuongeza:

“Siku zote nimekuwa nikijiuliza. Tanzania si nchi masikini, lakini Watanzania ndiyo masikini. Mpaka hapo ukiangalia kwa makini kama ambavyo nimekuwa nikisema siku zote na nitaendelea kusema kwamba rasilimali zetu zimekuwa zikihamishiwa nje ya nchi.

“Haiwezekani na utajiri tulionao leo tuendelee kuwategemea wafadhili kwa kiwango kikubwa katika bajeti yetu ya serikali. Angalia Kenya wameweza kujizatiti na kutegemea wafadhili kwa kiwango kidogo. Hapa lazima kuwe na kitu,” alisema Killango.

Alisema kwamba karibu ya mambo yote yanayoendelea kufumka na hata viongozi kufunuliwa uozo wao mengi yanatokana na uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tatu. Alisema katika hali ya kawaida huwezi kumlaumu Rais Kikwete.

“Katika hili ninaamini kama Chenge asingejiuzulu, basi Rais Kikwete angemuondoa madarakani kwani tayari na yeye jambo hili lilikuwa limemkera. Kwa hiyo Chenge amesoma alama za nyakati,” alisema Killango.

Lakini kwa upande wake aliyewahi kuwa Kkiongozi Mwandamizi katika Kamati ya Maadili ya CCM, Paul Sozigwa, alitoa kauli yenye kumpoza Chenge kidogo aliposema:

“Unajua bwana kama kila mtu anakunyoshe vidole wewe peke yako akidai ni mchafu na unanuka utakuwa ni wa aajabu kama hutajitoa ili uweze kujisafisha. Hii ni kazi ya umma ukiendelea kung’ang’ania mwisho wake ndiyo inakuwa balaa hata kama ningekuwa mimi nimetuhumiwa ningeachia ngazi mapema.

“Alichokifanya Chenge, ni sahihi kabisa. Na kama Chenge ni mkosaji kama ilivyo kwa watu wengine basi apelekwe kwenye vyombo vya sheria badala ya kuendelea kumsakama mpaka mtu anakonda,” alisema Sozigwa.

Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Philip Marmo, amesema Sheria ya Kupambana na Rushwa iliyoanza kufanyiwa kazi mwaka jana imeanza kuonyesha mafanikio mazuri.

Akizungumza na Rai, Marmo alisema kutungwa kwa sheria hiyo kumeweza kuhalalisha vyombo mbalimbali vya kimataifa vinavyojishughulisha na uchunguzi wa rushwa kuwa na nguvu inayovuka mipaka ya nchi husika.

"Umeona mashirika ya nje yanayojishulisha na uchunguzi wa rushwa yanafanya uchunguzi hata ndani ya nchi. Suala ni kuangalia mazingira ya uchunguzi yawe mazuri vipi," alisema Marmo.

Hata hivyo, Rai ilipowasiliana na Chenge kwa njia ya simu wiki hii, alisema:

“Bwana, mimi siku hizi bila kukumbana uso kwa uso na nyinyi (waandishi wa habari) sizungumzi kabisa. Ukiweza nifuate nipo Dodoma bungeni (akakata simu),” alisema Chenge.


Hii imetoka kwenye gazeti la Rai, tarehe 24 Aprili 2008



No comments: