Sunday, May 04, 2008


Binti akatwa masikio yote

katika kituko cha ndoa ya

kulazimishwa



Na Frederick Katulanda, Tarime

MSICHANA Robhi Thomas (15), amekatwa masikio yote na kujeruhiwa mabegani na vidole vya mkono wa kulia na baba mkwe.

Binti huyo ambaye anadai kuwa aliolewa kwa lazima baada ya baba yake kupokea mahali ya Sh350,000 alipata mkasa huo kufutia ugomvi uliotokea kati ya wazazi na baba mkwe aliyetambulika kwa jina la Mwita Thomas Mrimi.

Tukio hilo limetokea katika Kijiji cha Rusuti, Tarafa ya Tarime mjini Kata ya Inchage Aprili 18, mwaka huu usiku, wakati Robhi akiwa nyumbani kwa mume wake Thomas Mwita (18).

Kufuatia ugomvi wa wazazi wa Robhi na mkwewe nyumbani kwao, baba wa mume wake aliporudi alimwita mtoto wake Thomas na kumuagiza amfunge kamba mkewe , naye akafanya hivyo.

Akisimlia mkasa huo alisema baba mkwe alikwenda nyumbani kwa wazazi wake na kulalamika kuwa walikuwa wakimfundisha tabia mbaya, hatua ambayo ilizua ugomvi na kutokana na majibizano ya muda mrefu, mzee huyo aliokota kipande cha kuni na kumpiga nacho mama yake mdogo ambaye alikimbilia ndani na kutoka na panga na kupigwa nalo kwa kutumia ubapa wake.

“Baada ya kuanyiwa hivyo alikuja nyumbani, kamuita Thomas na kumwamuru anipeleke nikiwa nimefungwa kamba, naye akinamusha usiku na kunifunga kwa kamba mikononi na kunitoa nje.

"Baba mkwe alinieleza kuwa nyumbani kwenu wamenidhalilisha sana hivyo lazima na nikushikishe adabu, kisha akaanza kunikata sikio la kushoto taratibu kama anachinja nyama na la kulia na kunijeruhi sehemu nyingine,” alidai Robhi akiwa katika hosptali ya Mkoa wa mara ambako amelazwa kwa matibabu.

Robhi amejeruhiwa sikio lote la kushoto na kuondolewa sehemu kubwa ya ngozi mpaka eneo la shavu na sikio la kulia lililokatwa na kubaki likining’inia.

Pia Rhobi alitaktwa kwenye mabega yote mawili, shavu la kulia pamoja na vidole vyote vya mkono wa kushoto.

Alidai kuwa baada ya mkwewe kumkata, alitupa chini kipande chasikio hilo kutupwa ambacho kugombewa na mbwa.

Kamanda wa Polisi mkoani Mara, David Ole Saibullu alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa mtuhumiwa alikamatwa siku nne baada ya tukio hilo na kwamba polisi bado inamsaka mume wa Robhi ambaye alitoroka muda mfupi baada ya tukio hilo.

Kufuatia tukio hilo Shirika la Haki za Minadamu wilayani Tarime (Shehabita) na Shirika la Kutetea Haki za Wanawake la Kivulini Mwanza, walimtembelea binti huyo na kulaani vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa wanawake wilayani Tarime.

Mratibu wa Shehabita, Bonny Matto alilaani ukatili huo na kuiasa jamii ya wakazi wa eneo hilo kuepukana na mila potofu na kukemea vitendo hivyo kwa vile vimekuwa vikitokea kila mara na kusabisha vilema na vifo kwa wanawake wengi.

Naye Baranabas Solo ambaye ni Mwezeshaji wa Kivulini pia alilaani ukatili huo na kuitangaza wilaya ya Tarime kuwa ni eneo hatari kwa usalama na maisha ya wanawake kutokana na vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa.

“Huu ni ukatili wa kutisha dhidi ya wanawake, ukiangali binti amelazimishwa kuolewa na wazazi wake akiwa bado anahitaji kwenda shule, lakini sasa amekuwa kilema baada ya kukatwa katwa masikio na mabega, huu ni ukatili wa hali ya juu ambao unapaswa kulaniwa kwa nguvu na watu zote,” alieleza Solo.



No comments: