Saturday, May 03, 2008



HISTORIA ya

rushwa au ufisadi



na Mwassa Jingi


HISTORIA ya rushwa au ufisadi kama ambavyo neno ufisadi limeanza kutumika hapa Tanzania ni ndefu na viwango vyake hutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine. Aidha madhara yatokanayo na ufisadi nayo hutegemea viwango vya ufisadi katika jamii husika.

Jumla ya yote ni kwamba, ufisadi una madhara makubwa kwa kila jamii mahali popote duniani. kibaya zaidi ni kwamba ufisadi si ugonjwa ambao unaweza kupatiwa tiba ya kisayansi na wala si ugonjwa wa akili unaweza kutulizwa au kurekebishwa na wataalamu wa elimu ya saikolojia. Kwa hiyo madhara ya vitendo vya kifisadi ni makubwa ingawa tiba yake ni ngumu na hasa kwa jamii zinazopatikana katika ulimwengu wa tatu, maarufu kama nchi zinazoendelea.

Kama ambavyo historia ya ufisadi ni ndefu, ndivyo zilivyo na juhudi za kuukomesha au kuupunguza ili ubaki katika kiwango cha chini kisichoweza kuleta madhara makubwa kwa jamii husika. Katika Taifa letu changa la Tanzania, rushwa kama sehemu ya ufisadi imekuwapo tangu enzi za utawala wa kikoloni, ingawa imekuwa ikipanda na kushuka kwa viwango tofauti na kwa vipindi tofauti kutegemeana na ubora wa utawala katika majira husika. Kwa mfano, utawala wa Kiingereza uliodumu hapa nchini kwa takriban miaka 40 —kuanzia mwaka 1920 -1961, ulitambua kuwapo vitendo vya rushwa na hivyo kutunga sheria ya kuzuia rushwa mwaka 1958, wakati nchi yetu ikiitwa Tanganyika.

Miaka 10 baada ya uhuru, yaani mwaka 1971, Serikali changa ya Tanzania chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ilitambua dalili za kuongezeka kwa vitendo vya rushwa na hivyo kulazimika kutunga sheria mpya ya kuzuia rushwa au ufisadi. Sheria hiyo ya mwaka 1971 ndiyo iliyounda kikosi cha kuzuia rushwa kilichojulikana kwa jina maarufu la Anti- Corruption Squad. Sheria ya kuzuia rushwa ya mwaka 1971 iliendelea kuwa ndiyo sheria kuu ya kuzuia rushwa kwa kipindi cha miaka karibu 36, ikifanyiwa marekebisho ya hapa na pale, mpaka tulipopata sheria mpya ya kuzuia na kupambana na rushwa hapo mwaka jana (2007). Kabla ya sheria ya mwaka jana, taasisi ya kuzuia rushwa ilijulikana kwa jina la PCB- yaani Taasisi ya Kuzuia Rushwa chini ya sheria ya mwaka 1971.

Sheria mpya ya kuzuia na kupambana na rushwa ndiyo ambayo imeleta jina jipya la PCCB (Prevention and Combating of Corruption Bureau), likiwa ni kifupisho cha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Akiwasilisha bungeni muswada wa kuomba kutungwa kwa sheria hiyo mpya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora wa wakati huo, Philip Marmo alisema kuwa madhumuni na sababu ya kutungwa kwa sheria hiyo ni kutokana na sheria iliyopo ya mwaka 1971 kupitwa na wakati kulikotokana na mabadiliko makubwa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii; mabadiliko ambayo yalifanya sheria ya mwaka 1971 isiweze tena kudhibiti vitendo vya rushwa kikamilifu kwani makosa ya rushwa yameendelea kushamiri huku yakifanyika kwa ustadi na ufundi mkubwa.

Kutokana na madhumuni mazito ya kutaka kuwepo kwa sheria hiyo ya kuzuia na kupambana na rushwa, waheshimiwa wabunge kwa kauli moja waliupitisha muswada huo kuwa sheria. Rais naye kwa upande wake hakuchelewa kutia mkono wake ili kuruhusu muswada huo kuwa sheria na kuanza kutumika miezi mchache baadaye.

Tukirudi nyuma kidogo, tunaweza kujikumbusha jinsi hali ya rushwa ilivyokithiri katika jamii yetu kutokana na mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii kuanzia miaka ya 1980 na 1990, ambapo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 ulioshirikisha vyama vingi vya siasa rushwa ilionekana kukithiri.

Mgombea wa chama tawala, Benjamin Mkapa, ambaye baada ya uchaguzi alipata ushindi na kutinga Ikulu, alitoa kipaumbele cha kwanza kabisa kupambana na rushwa na dhamira hiyo ilithibitika pale alipounda Tume ya kuchunguza kero za rushwa nchini chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba. Taarifa ya Tume ya Jaji Warioba ya mwaka 1996, ilibainisha kuwapo kwa kiwango kikubwa cha rushwa katika nchi yetu karibu katika sekta zote kwenye utumishi wa umma.

Taarifa hiyo ya Tume ya Warioba ndiyo iliyompa Rais Mkapa jeuri ya kutaka kupambana na rushwa kwa nguvu zote. Serikali ya Mkapa ilijitahidi kupambana na rushwa si kwa kukamata wahalifu wa vitendo vya ufisadi kwa wingi na kufanikiwa kuwatia magerezani, bali zaidi sana ilitengeneza sera na sheria lukuki kama hatua ya kwanza ya kupambana na vitendo vya rushwa nchini. Pamoja na Mkapa kuapa kukomesha rushwa, hiyo rushwa haikupungua na badala yake ilizidi kupamba moto. Hali hii ndiyo inayoonekana sasa miaka miwili na nusu baada ya utawala wa Mkapa kukaa pembeni.

Kwa nini rushwa iliendelea kutesa pamoja na kuwa na ripoti ya Tume ya Jaji Warioba yenye kurasa zaidi ya 500, ikiwa imejaa maelezo na mapendekezo mengi kama hatua madhubuti ya kuisadia Serikali namna bora ya kupambana na vitendo vya kifisadi? Kikwazo kikubwa kilichokuwa kinatolewa na wadau wa kwanza wa kuzuia rushwa nchini na hasa PCB kilikuwa ni udhaifu mkubwa wa sheria ya kuzuia rushwa ya mwaka 1971. PCB ilidai kuwa sheria hiyo haikuwa na meno ya kutosha kuwawezesha kuzuia na kupambana na rushwa nchini kikamilifu.

Hoja ya PCB kutokuwa na meno ilinoga zaidi walipokejeliwa kuwa walikuwa si lolote katika jitihada zao za kuzuia na kupambana na rushwa kubwa kubwa na walichokuwa wanafanya ni kukamata dagaa tu. Shutuma hizi kwa PCB ya wakati huo zilitokana na matokeo dhaifu ya kazi yao ya kuzuia vitendo vya rushwa vyenye kufilisi nchi kupitia mikataba mikubwa hasa katika kipindi ambacho biashara kubwa ya serikali ya awamu ya tatu ilikuwa ni kuuza yaliyokuwa mashirika ya umma kwa bei ya kutupa na kuingiza idadi kubwa ya wawekezaji wakubwa katika sekta ya madini kwa mikataba tata.

Utetezi wa PCB siku zote ulikuwa ni kwamba wasingeweza kupambana na rushwa kubwa kubwa kwa kukamata ‘samaki wakubwa’ kutokana na udhaifu wa sheria iliyokuwapo. Nadhani sheria mpya ya mwaka 2007 inawezekana ni matokeo ya shinikizo la PCB na wadau wengine nje ya Serikali ili kupata meno ya kutosha kupambana na rushwa. Pamoja na udhaifu huo wa sheria ya mwaka 1971, bado sheria mpya ilichukua muongo mmoja kutungwa baada ya Serikali ya Awamu ya Tatu kuingia madarakani. Na kama si shinikizo kutoka nchi wafadhili kama Denmark na nyingine, inawezekana sheria mpya ya kuzuia na kupambana na rushwa isingekuwapo hadi leo hii.

Februari mwaka jana, Serikali ya Denmark ilitishia kuinyima Tanzania misaada kwa kukata asilimia 20 ya msaada wake kama isingeharakisha kupeleka bungeni muswada wa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa. Hatimaye sheria mpya waliyoitamani sana PCB kwa muda wa miaka zaidi ya 10 waliipata na kuitia kwapani. Ni karibu mwaka mmoja sasa tangu kukabidhiwa kwa PCB sheria hiyo mpya iliyobadilisha kanzu ya PCB kuwa PCCB.

Wananchi wengi walikuwa na imani kubwa na Serikali ya Mkapa na hasa baada ya Taarifa ya Tume ya Warioba, wakijua kuwa ndani ya kipindi cha miaka 10 cha utawala wa Mkapa rushwa ingebakia kuwa ni historia katika kizazi chetu. Kwa bahati mbaya Mkapa na PCB yake walimaliza miaka 10 wakiwa wamenasa dagaa na visamaki vichache fisadi, wengi wao wakiwa ni perege kama vile mahakimu wa mahakama za mwanzo na polisi wa vyeo vya chini kama vile makonstebo na makoplo.

Sijui hawa mahakimu na polisi waliotupwa gerezani kwa kupatikana na rushwa ya vijisenti kama Sh 10,000 wanajisikiaje wanaposikia sasa kuna jamaa wengine huku nje kila siku wanatangaza kujiuzulu kwa tuhuma za kudaiwa kulamba vijisenti vinavyofikia bilioni, tena vijisenti hivyo vikiwa vimewekezwa katika benki za nje.

Je, huu ndio utawala bora ambao ulikuwa ni kaulimbiu ya Mkapa ikichagizwa na maneno kama vile uwazi na ukweli? Baada ya ndugu zetu wa PCCB kukabidhiwa sheria mpya waliyoitamani muda mrefu, wengi tulitarajia kuwa sasa mwisho wa dunia ya mafisadi umekaribia; na kusema kweli tulitarajia kuanza kuona damu ya mafisadi ikimwagika kwa vile sasa PCCB haikuwa tena PCB iliyokuwa na meno manne tu, ambayo yasingeweza kuuma hata kipande cha nyama laini kama ile ya kuku wa kisasa anayekuzwa kwa dawa ndani ya majuma matatu.

Mkurugenzi wa PCCB, zamani PCB, mara nyingi tu kupitia vyombo vya Habari alisikika akilalama kuwa asingeweza kufanya maajabu kukabiliana na mafisadi kwa kutumia mdomo uliokuwa na meno manne tu; akimaanisha sheria ya zamani ya kuzuia rushwa ambayo iliainisha makosa manne tu, ambayo kwayo PCB ilipaswa kuwakamata na kuwatia hatiani wahalifu wa makosa ya kifisadi.

Kwa hoja hiyo, PCB ilishinda hoja siku zote. Sasa wanayo kwenye makabati yao sheria mpya yenye orodha ya makosa ya jina yapatayo 24, makosa ambayo kwa mujibu wa sheria hii mpya ni kama vile yalilenga kuzuia na kupambana na rushwa kwa kiwango cha juu kiasi kwamba hakuna jiwe litakalosalia juu ya jiwe katika kuzuia na kupambana na ufisadi.

Saa zimepita, siku zinapita, miezi inapita, miaka inapita, ndugu zetu wa PCCB bado wanasoma tu ile sheria bila kuitekeleza. Baada ya kuwa na sheria hiyo sasa PCCB wameikabidhi kwa shirika lisilo la kiserikali -NOLA ili waifundishe kwa makundi mbalimbali ya jamii, vikiwamo vyombo vya habari.

Hili ni jema, lakini ndio waishie hapo? Je, hicho ndicho kibarua ambacho miaka yote PCB na sasa PCCB walikuwa wanaisubiri ili wawafundishe wananchi pamoja na mafisadi namna ya kukataa vitendo vya rushwa? Na je, wale wasiofundishika kuacha vitendo vya rushwa mbona hawakamatwi? Ndiyo kusema baada ya sheria mpya kuwapo mafisadi tayari wameshajisalimisha na kwa hiyo hakuna tena fisadi wa kukamatwa na PCCB?

Kamati Teule ya Bunge ya hivi karibuni iliyopewa jukumu la kuchunguza vitendo vya ufisadi kwenye mkataba kati ya TANESCO na kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond iliibeza sana PCCB, kwamba si lolote katika kutetea maslahi ya umma. PCCB ambayo kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Dk. Harrison Mwakyembe ilichukua karibu miezi sita kuchunguza mkataba huo na hatimaye ikatoa taarifa kuwa mkataba wa TANESCO na Richmond haukuwa na harufu yoyote ya rushwa ukiachilia mbali kasoro ndogo ndogo za kufuata taratibu, ilionekana mbele ya jamii kama msaliti mkubwa wa Watanzania.

Kutokana na taarifa yao, Kamati ya Mwakyembe iliifananisha PCCB na taasisi ya kupamba rushwa. Kama kweli PCCB imeshindwa au itashindwa kufanya kazi baada ya kuwa na meno ya kutosha, basi hilo ni jambo la huzuni kwa Watanzania wote.

Kamati ya Dk. Mwakyembe ilitumia siku 45 tu na kuibuka na taarifa mbaya za kifisadi kuhusu mkataba wa TANESCO na Richmond. Je, haya meno 24 ya PCCB bado tu hayatoshi kuuma wakati tuliambiwa kuwa yangetosha kabisa kupambana aina zote za rushwa za zamani na zile mpya zinatokana na mazingira mapya ya sayansi na teknolojia? Serikali ya Awamu ya Tatu chini Mkapa ilifanya kazi kubwa ya kutandaza mtandao wa PCCB kuanzia ngazi ya mkoa mpaka wilaya karibu zote nchini, mtandao ambao tulitarajia ungenasa kila aina ya samaki na dagaa fisadi, lakini hali ilivyo inatia shaka.

Pamoja na mtandao huo mpana, bado mpaka sasa ukimuuliza mwananchi wa kawaida mtaani nini matunda ya kuwa na mtandao mkubwa wa PCCB, kwa hakika atakwambia hakuna chochote kilichokwishafanyika. Bila shaka PCCB sasa kazi yake ni kufunika mafisadi ili waendelee kutesa chini chini. Hata tuhuma hizi za ‘mafisadi’ wanaojiuzulu mfululizo siku hizi si matokeo ya mtandao wa PCCB.

Hata Dk. Wilbroad Slaa ambaye hana mtandao wowote wala mbwa wa kunusa ufisadi ameweza kuibua orodha ndefu ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na vitendo vya kifisadi, ambavyo sasa matokeo yake ni dhahiri, ingawa pale mwanzoni watu kama Dk. Slaa walipokuwa wanatoa ile ‘list of shame’ walionekana kama wendawazimu mbele ya jamii ya Kitanzania. Lakini baadhi ya waliotajwa wameshajiuzulu.

Ni kwa vipi watu kama Dk. Slaa, Zitto Kabwe na wengine waweze kuibua mikataba yenye harufu ya kifisadi, halafu PCCB wenye kila fani washindwe?

Nadhani hata Rais ameona PCCB yake haina kazi ndiyo maana amempa Mkurugenzi Mkuu wake kazi ya kukusanya pesa zilizochukuliwa na mafisadi kupitia mpango wa EPA kwa sababu PCCB pamoja na meno yote hayo hayawezi kuuma. PCCB si ajabu imeundwa ili kuongeza ajira angalau ichangie kufikisha idadi ya ajira milioni moja kama ilivyoagiza ilani ya chama tawala kwa wapiga kura wake hapo mwaka 2005.

Inakuwaje watu kama akina Chenge kuwa na vijisenti mabilioni nje ya nchi bila PCCB kujua? Je, PCCB hawaruhusiwi kukagua majalada ya wahemishiwa na kuona kama mali walizo nazo ni nyingi kiasi gani? Je, PCCB hawana ubavu kisheria kupitia mikataba yote, na kama hayo meno 24 hayawezi kuwapa nguvu ya kupitia vitu kama hivyo, je, kuna haja kweli ya kuwa na kitu kinachoitwa PCCB?

Ni afadhali tufute PCCB na kazi zake tuikabidhi taasisi kama SFO ya Uingereza kuliko kuwa na waajiriwa mamia walio kwenye orodha ya walipwaji kila mwezi wakati hawawezi hata kutusaidia kukamata hata fisadi moja lenye akaunti ya Sh milioni 200 tu, licha ile ya vijisenti bilioni moja vya Chenge. Huenda PCCB wanafanya kazi ambayo matokeo yake hayajawa dhahiri. Tunaomba PCCB wasikalie sheria mpya, bali watuambie sisi wananchi wanafanya nini na hiyo sheria mpya yenye meno 24?

mwassajingi@yahoo.com



No comments: