Sunday, May 04, 2008



Uwepo mkakati madhubuti

wa kukuza, kuendeleza

Kiswahili



Evance Ng’ingo
Jumapili, 4 Mei 2008


JANA ilikuwa ni siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani na kwa Tanzania iliadhimishwa sambamba na kumbukumbu ya Mzee Hamis Akida na Profesa Zacharia Mochiwa ambao walikuwa wataalamu wa lugha ya Kiswahili.

Kwa kuwa Wanahabari jana ilikuwa ni siku yao muhimu ya kuenzi shughuli zao napenda kuwakumbusha umuhimu wa wanataaluma hao katika kutunza na kukienzi Kiswahili nchini.

Kwa kuwa nchi yetu imejipanga vyema kuingia na Kiswahili katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa kama bidhaa ambako wataalamu wataajiriwa kufundisha lugha hiyo nje ya nchi, kuna umuhimu kwa wanahabari kukitunza na kukiendeleza Kiswahili.

Vipo baadhi ya vyombo vya habari nchini ambavyo hutumia maneno ya Kiswahili visivyo. Utakuta neno la Kiswahili linatumika mahala lisipotakiwa! Mfano mzuri ni neno fisadi ambalo limekuwa likitumiwa kwa wingi katika vyombo vya habari nchini likiwa linawatambulisha wabadhirifu wa fedha za umma.

Matumizi ya neno hili siyo sahihi hasa ikizingatiwa kuwa maana halisi ya neno hilo kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili ni mwanamume anayetembea ovyo na wake za watu. Nashawishika kuamini kuwa wanahabari wanaweza kuwa ni miongoni mwa makundi ya watu wanaoharibu Kiswahili labda kwa makusudi au kwa kutokufahamu.

Matumizi yasiyo sahihi ya maneno kama hayo ni mengi. Utakuta mara nyingine katika redio na runinga linatumika neno masaa badala ya saa, katika kuzungumzia wingi wa muda.

Ikumbukwe kwamba maneno mengi ambayo chanzo chake ni Kireno hayana wingi, likiwamo neno meza. Makosa kama hayo yanatokana na kutozingatia matumizi sahihi ya lugha bila kutambua kuwa kuna idadi kubwa ya wananchi wanaoweza kupotoka na kuyakariri maneno hayo yanayotumiwa visivyo, kama ambavyo imekuwa kwa neno fisadi!

Inabidi wanahabari kuhakikisha wanakuwa makini kwa maneno ya Kiswahili kuepuka kuyapotosha kwa sababu kwa kufanya hivyo wanakuwa wanarudisha nyuma maendeleo ya lugha hiyo.

Na kwa kuwa jana walikumbukwa Mzee Hamis Akida na Profesa Zacharia Mochiwa kwa mchango wao wa kuendeleza lugha hiyo basi ni bora serikali ikawakumbuka zaidi kwa vitendo.

Hatua hiyo itakuwa ni pamoja na kufanikisha makubaliano kati ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika kuhakikisha wanakamilisha mpango wa kupeleka wataalamu nje ya nchi kufundisha lugha hiyo.

Wapo wanaoenda kufundisha Kiswahili nje lakini baadhi yao hawana utaalamu wa lugha hiyo na huifundisha kutokana na mazoea tu hali inayoweza kuwapotosha wanaojifunza na kuweka mazingira ya ubabaishaji.

Kwa kuwa idadi kubwa ya walimu na wataalamu wa Kiswahili wanaweza kupata ajira nje ya Tanzania kwa kwenda kufundisha Kiswahili hapana budi serikali kuweka mikakati kabambe ya kuweza kuitumia lugha hiyo kama bidhaa itakayotoa ajira kwa kuwa tayari soko lipo.

Na kwa kuwa wanahabari na wataalamu wa Kiswahili kwa pamoja ndiyo msingi mkuu wa kukienzi na kukikuza Kiswahili ndani na nje ya nchi, inabidi kujipanga upya na kuwa na nia ya kweli ya kuiendeleza lugha hiyo.

No comments: