Saturday, May 03, 2008


Chenge achuriwa



na mwandishi wetu


UVUMI ulienea ndani na nje ya nchi jana, ukieleza kwamba aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, ‘amekufa’ kwa sumu.

Habari hizo zilizua taharuki miongoni mwa wananchi kadhaa ambao walihaha huku na kule kutaka kujua ukweli wa mambo.

Chumba cha habari cha MTANZANIA kilipokea simu zisizo idadi, huku wahariri na waandishi wa habari, wakifanya kazi ya kujibu simu na ujumbe mfupi wa maandishi (sms).

Ingawa uvumi huo ulipamba moto jana, lakini ulianza juzi usiku ambako sms yenye maneno: “Kifo cha Chenge kisiasa”, inadaiwa kuwa chanzo. Mtu aliyeandika ujumbe huo, hatujafanikiwa kumjua.

Baadaye kukawapo madai kwamba Chenge alikuwa amejiua kutokana na kukabiliwa na tuhuma za ufisadi zilizomfanya ajiuzulu uwaziri wiki mbili zilizopita.

Wavumishaji hao, baadaye walisambaza ujumbe ukidai kwamba mwanasheria huyo alichukua uamuzi huo kukwepa aibu anayoipata sasa, hasa anapopita mitaani na namna alivyoshupaliwa na vyombo vya habari.

Uvumi huo uligongana na mwingine uliodai kwamba Chenge hakujiua kwa sumu, badala yake ameuawa ikiwa ni mkakati ulioandaliwa kwa ajili ya kuwamaliza watuhumiwa wa ufisadi.

Ilidaiwa kwenye sms kwamba mpango umeandaliwa wa kuhakikisha kuwa watuhumiwa wa ufisadi, akiwamo Chenge, wanaondolewa ili kuwanusuru vigogo wengine mafisadi ambao hawajaguswa.

Uvumi huo ulikwenda mbali zaidi, kwa kueleza kwamba mwili wake ulikuwa umehifadhiwa katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo. Vyanzo vya habari ndani ya Lugalo vilikanusha taarifa hizo na kusema ni za uongo.

Tangu asubuhi, simu ya Chenge ilikuwa ikiita tu bila kupokewa. Hali iliendelea hivyo hadi mchana ambako ilitoa majibu kwamba imezimwa.

Hata hivyo, mmoja wa wafanyakazi wa Wizara ya Miundombinu, Ntemo, alipoulizwa kuhusu taarifa hizo, alisema ulikuwa uvumi ulioenezwa na baadhi ya watu wasiojulikana.

“Na mimi nilipata taarifa hizo, nikampigia simu na tukazungumza, yeye alichosema ni kwamba ‘wali hauliwi hapa’, mimi ni mzima,” alisema.

Maneno “wali hauliwi hapa”, bila shaka yalilenga kuonyesha kuwa yeye ni mzima, hivyo ‘shughuli’ ambayo kwa kawaida huambatana na chakula, hasa wali, isingekuwapo.

Kumeanza kujengeka tabia ya uvumi miongoni mwa wananchi. Miezi kadhaa iliyopita, kulisambazwa uongo kwamba Mohamed Mpakanjia, ambaye alikuwa mume wa marehemu Amina Chifupa, alikuwa amefariki dunia. Uvumi huo ulisambazwa siku chache baada ya kifo cha Amina, ambaye alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu.

Kabla ya tukio hilo, kulivumishwa kwamba Rais mstaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi, naye eti alikuwa ameaga dunia. Kauli kama hiyo imeshatolewa pia kwa Mzee Rashidi Kawawa (Simba ya Vita). Mara zote, uvumi huo umewavuruga baadhi ya wananchi, hasa wenye mapenzi kwa viongozi hao.





No comments: