Saturday, May 03, 2008



Jamhuri ya

mapwagu na mapwaguzi



Rais Kikwete ana kazi kubwa na ngumu mbele yake. Wananchi wameonyesha wazi kwamba wanataka mabadiliko. Wamechoka kuambiwa kwamba maisha ni magumu, huku wakiona wezi wakineemeka

na manyerere jackton


BUNGE lililokuwa likililiwa na wananchi, kupitia vyombo vya habari, walau sasa limeanza kuonekana.

Heshima ya Bunge na wabunge, vilipotea kwa kasi ya kusikitisha. Shukrani kwa Mwenyezi Mungu, kwa kusikia kilio cha wananchi, hata akaweza kuwafanya wabunge sasa wawe wawakilishi wa kweli wa maslahi ya wananchi.

Mara kadhaa nimeandika makala nyingi kuwashutumu wabunge. Ilifikia hatua nikalifananisha Bunge na mhuri Fulani mkubwa wenye herufi zaidi ya 200; ambao hauna kazi yoyote ya maana.

Kazi zilizofanywa na Bunge tangu mwanzoni mwa mwaka huu, hata kama si za kuridhisha sana, lakini zinatia moyo. Zinatia moyo kwamba kumbe wabunge wakiamua, wanaweza kabisa kutetea na kulinda masilahi ya nchi yetu.

Kumbe wabunge wakiamua, wanaweza kusimama upande wa makabwela. Wakawatetea. Wanaweza kabisa kuibana Serikali na vyombo vyake, na kuhakikisha kuwa vinawajibika kwa wapiga kura wan chi hii.

Mwamko wa wabunge kwa mwaka huu, unazidi kunisaidia kwenye hoja yangu ya kila mara, ya kwamba nchi yetu inavurugwa na viongozi. Viongozi wamepewa dhamana ili wawatetee wananchi. Wamepewa dhamana ili waulinde utajiri wa nchi yetu kwa masilahi yetu sote.

Lakini wao wanapokuwa wa kwanza kuwa mapwagu na mapwaguzi, tusitarajie muujiza. Inapotokea kiongozi akahifadhi nje ya nchi, mabilioni ya fedha, lazima wananchi wahoji. Lazima wapewe majibu kwa sababu katika nchi kama yetu, kiongozi (si mfanyabiashara) kuwa na mabilioni benki, si jambo la kawaida.

Wakati fulani Rais Jakaya Kikwete, akiwa Uingereza, alikutana na maswali ya Watanzania waishio huko ambao kwa kawaida, huwa hawana simile kwenye maswali. Akaulizwa kuhusu ukwasi wa Mzee Benjamin Mkapa, na tuhuma zinazomkabili.

Katika majibu yake, Rais Kikwete, alitaka Watanzania wamwache ‘mzee wa watu’ apumzike baada ya kazi kubwa ya kuliongoza taifa. Tena akasema asingekuwa tayari kuanzisha uchunguzi dhidi yake.

Nashukuru kwamba mimi nilikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kabisa, siku moja baada ya kauli hiyo, kuandika makala ya kupingana na Rais Kikwete. Tulimpinga Rais Kikwete kwa hoja kwamba kama tutaendeleza utamaduni wa kuwaacha viongozi wastaafu, wanaotajwa tajwa kwenye ufisadi, basi tutakuwa tunajiandalia taifa la waporaji.

Hoja ya kuamini hivyo ni kwamba wanaweza kuja viongozi (si lazima wawe marais), wakaongoza kibabe, wakawa hawaambiliki, wakakwapua ukwasi wa nchi, wakamaliza muda wao wa utawala wakiwa matajiri wa kutupwa na mwishowe wasihojiwe.

Hawa wataiba kwa juhudi kubwa wakitambua wazi kuwa hakuna mrithi wao atakayethubutu kuwahoji. Nchi haiwezi kujengwa kwa staili hiyo.

Tena mara kadhaa tumehoji uyoga wa majumba ya kifahari yanayoonekana maeneo mbalimbali ya nchi. Namshukuru Mungu kwamba nimejaliwa kupata ki-jumba cha kuishi. Kijumba changu ni kidogo mno, lakini nikiri kwamba kazi ya ujenzi ni ngumu mno, na hadi sasa baada ya nusu mwongo, sijakamilisha ujenzi.

Najiuliza, kama nimeweza kutokwa jasho kiasi hiki, kwa kujenga vyumba vitatu, hawa wanaojenga mahekalu Mikocheni, Oysterbay, Masaki, Msasani, Mbezi na kwingineko nchini, ukwasi huu wameutoa wapi? Je, ni kweli mshahara tu wa kiongozi unaweza kumwezesha kuwa na maghorofa kila mahali?

Je, nani, katika maisha haya ya Kiafrika, ya (extended family), anaweza kuwa na jeuri ya kuhifadhi ‘viji-senti’, tena nje ya nchi? Hili linaweza kuwa jambo la kawaida, lisilo na maswali kama kwenye fedha hizo ni mfanyabiashara, lakini kwa kiongozi, tena wa umma, lazima tuhoji. Haiwezekani jamani tukaachia hivi hivi tu.

Rais Kikwete ana kazi kubwa na ngumu mbele yake. Wananchi wameonyesha wazi kwamba wanataka mabadiliko. Wamechoka kuambiwa kwamba maisha ni magumu, huku wakiona wezi wakineemeka. Hawataki kudanganywa tena, wala kusikia porojo za ugumu wa maisha kutoka kwa wanasiasa.

Wabunge wameanza kutekeleza wajibu wao wa msingi, wa kutetea na kulinda masilahi ya wananchi na nchi kwa jumla. Hawataki mzaha tena. Katika hili, kila mwenye macho na masikio, hahitaji kufafanuliwa. Linaonekana na kusikika kwa kila mmoja wetu.

Tuanze kuhojiana mmoja baada ya mwingine. Hawa wenye majumba na rasimali za kutisha, tuawaulize wenzetu wamezipataje? Tuwaulize bila woga wala uonevu.

Hivi karibuni nilikuwa wilayani Handeni. Wale wanaodhani kwamba eti mikoa ya kusini au magharibi ndiyo “iliyosahaulika’, wanajidanganya. Kutoka Handeni hadi Dar es Salaam ni umbali wa kilometa 240 hivi. Lakini ni vigumu mno kuamini kuwa maisha ya wananchi katika wilaya hiyo, ni maisha yaliyo karibu na waridi, yaani Dar es Salaam.

Handeni imejaa nyumba za tope zilizoezekwa kwa majani. Chache zilizoezekwa kwa mabati, mabati hayo yamezeeka. Tena inaonekana kuwa mabati hayo yaliezekwa wakati ule wa uhamasishaji ujenzi wa nyumba bora vijijini na mijini. Wakati ambao kina Mzee Rashid Kawawa walipita kila kijiji nchini, kuhamasisha kilimo na maendeleo miongoni mwa wananchi.

Handeni, wananchi wanalima, lakini hawaoni manufaa yoyote. Hawapewi elimu ya kuhifadhi vyakula ili ikiwezekana, wawe na hifadhi pamoja na ziada kwa ajili ya kuuza. Sasa njaa inabisha hodi, si Handeni tu, bali sehemu mbalimbali nchini. Adha zilizoikumba nchi mwaka 2006, sote tunajua. Viongozi kadhaa wako mstari wa mbele kupiga marufuku biashara ya mahindi mabichi. Sawa, uamuzi huu unalenga kuwasaidia wasife njaa. Lakini tunapaswa tutambue kuwa wakulima hawa hawana njia nyingine ya kujipatia mahitaji muhimu.

Wanahitaji sabuni. Wanahitaji kwenda hospitali kulipia ‘ushauri’ wa daktari, kabla ya kuandikiwa vyeti ili wakanunue dawa katika maduka yaliyojaa dawa za zilizoibwa serikalini. Kuwazuia, maana yake ni kuwataka watafute mbadala. Mbadala wa karibu ni kuvamia misitu wachome mkaa na kukata kuni. Vinginevyo, wavamie hifadhi za wanyama ili wapate vitoweo. Umasikini unazidi kuwaumiza siku hadi siku.

Barabara ni mbaya kiasi kwamba baadhi ya vijana, sasa hawafanyi kazi yoyote ya uzalishaji, zaidi ya kwenda maeneo ambayo wanajua magari yatakwama. Wanafanya kazi ya kuyakwamua ili wapate fedha za kuendeshea maisha. Kwa wanasiasa wetu, hiyo ni burudani kwao! Wanasema hiyo ni ajira!

Handeni na wilaya nyingine nchini, tunashuhudia ajuza wakilima. Ajuza mwenye umri wa miaka 75 au 80, atalima shamba la ukubwa gani ili aweze kupata mahitaji muhimu ya kibinadamu? Hawa, Serikali imewaandalia nini ili waweze kumaliza kwa raha, ngwe yao ya kuishi hapa duniani?

Viongozi wetu wanapopita wakiwa ndani ya magari, wakawaona wazee hawa wakiwa na majembe mikononi au mabegani; wanapopita na kuwaona watoto wasioenda shule kwa ajili ya kilimo; wanapoona watu wakikimbizana kuokota chupa tupu za maji au makopo ya bia na juisi; viongozi wanaoshuhudia haya, machozi yao huwa yako wapi? Huruma huwa wameitupa wapi? Wangapi husimama hata wakaweza kuzungumza kidogo na wananchi hawa?

Viongozi wetu wameshindwa kubadilisha maisha ya wananchi, badala yake wanachofanya ni kuota na kupanga mikakati ya ushindi wa kishindo mwaka 2010. Tumekuwa nchi ya uchaguzi tu! Nchi ambayo viongozi hupigana kufa au kupona ili washike madaraka, lakini ndani ya miaka mitano, wanachofanya ni kuhubiri mbinu nyingine za kupata ushindi katika uchaguzi ujao.

Umasikini wa Watanzania uko katika makundi mengi. Kuna kundi la masikini ambao ni masikini kwa sababu hawana namna ya kujikwamua. Hawa ni masikini wa mali. Lakini kuna masikini wa hali. Hawa wana mali na utajiri mwingi uliowazunguka, lakini ni masikini.

Hawa ndiyo wenye ng’ombe 200, lakini wanalala katika nyumba za tope zilizoezekwa kwa nyasi au udongo. Hawa ndiyo wenye watoto wanaokwenda shule wakiwa hawana viatu, na kama wanavyo, basi ni ‘makatambuga’. Hawa ni katika kundi la wafugaji wa kuku wanaoshuhudia watoto wao wakiugua kwashakoo, ilhali wao wakipeleka mayai yote sokoni na misheni!

Kundi la kwanza ni gumu kulibadili. Lakini hatuoni kama kuna juhudi za kweli za kubadili hili kundi la pili ambalo lina utajiri, lakini limegeuka na kuwa watumwa wa utajiri.

Hapa ndipo tulipotarajia kuwaona na kuwasikia viongozi wetu wakihubiri mabadiliko. Hapa ndipo wanasiasa walipopaswa kusimama majukwaani na kuwataka wananchi wabadilike. Yale makundi ya wanaharakati, mashirika yasiyo ya Serikali na kadhalika, ndipo yanapotakiwa yakeshe yakiendesha semina za kuwabadili wananchi ili wauchukie umasikini.

Lakini wapi. Hakuna kitu. Wanasiasa wanapozuru maeneo hayo, wanachofanya ni kutoa tambo za kukua kwa uchumi. Wanatamba TRA kuvuka malengo ya kukusanya kodi kwa mwezi! Kwa mwananchi wa kawaida, mwananchi wa Kideleko, Tanga au Kasesya kule Rukwa, takwimu hizo zinamsaidia nini? Sana sana kinachoonekana, ni wananchi wenye uelewa, kuanza kuwachukia viongozi.

Viongozi, badala ya kwenda kubadili maisha ya wananchi, wanamaliza muda wote majukwaani, wakisifiana na kupeana pongezi zisizo na msingi wowote. Wanakaukiwa mate midomoni wakiomba mwaka 2010 wachaguliwe eti kwa sababu hakuna chama kingine chenye kuweza kuwaletea wananchi neema.

Dhana hii ya kupuuza kuhimiza maendeleo, na kuanza kuomba kura za uchaguzi ujao, ni hirizi ya umasikini.

Nchi yenye viongozi ambao kazi yao si kupima yale waliyoahidi, bali kuomba wachaguliwe ili watoe tena ahadi, haiwezi kuendelea.Wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu na makundi mengine ya ulaji, wanachofanya si kuwafikia wananchi moja kwa moja vijijini au mijini.

Wanashinda na kukesha katika hoteli kubwa za Dar es Salaam, Bagamoyo, Mwanza, Arusha na Morogoro, wakiendesha semina zisizokuwa na manufaa yoyote kwa masikini. Wangapi wamekwenda vijijini, wakaendesha semina, warsha au makongamano kwa wakulima na wafugaji? Wangapi wamekwenda kuwafundisha makabwela wa nchi hii, wajue haki na wajibu wao?

Walichobaki wakifanya ni kutafuta fedha kwa udi na uvumba, waandae viji-semina uchwara katika hoteli kubwa kubwa mijini, wakimaliza wagawane fedha. Wazungu wanaotoa fedha hizo si wajinga.

Wanajua sana mchezo huu unaoendelea, lakini wanachekelea. Wanachekelea kwa sababu si wazungu wote wanaofurahi kuona Mwafrika akiondokana na umasikini. Hawana huruma hiyo. Nao wanapoona tuna makundi ya wezi kupitia semina hizi, huburudika, maana hujua uzuzu utaendelea kudumu miongoni mwetu.

Matajiri, kama ndugu yetu Andrew Chenge, wawe na huruma. Sh bilioni moja kwenye akaunti yake ni viji-senti ambavyo akiamua kuviwekeza hapa nchini vitabadili maisha ya watu. Fikiria, zile Sh bilioni moja za Rais Kikwete, kwa kila mkoa, zimekuwa na matokeo gani?

Kama Sh bilioni moja zimetolewa kwa mkoa, je, ingekuwaje Chenge akaamua hiyo Sh bilioni moja akaitoa kama mkopo kwa wananchi wa jimbo lake tu? Hivi Sh bilioni moja ziingie Bariadi Mashariki, watu wakopeshwe, ziwekwe kwenye mzunguko wa uzalishaji, haziwezi kubadili maisha ya wananchi walau kwa kiasi kidogo?

Nihitimishe kwa kusema kwamba matatizo ya nchi yetu yatamalizwa au kupunguzwa na viongozi waliodhamiria kwa dhati kuwatumikia wananchi.

Kama nilivyoamini, na ninavyoendelea kuamini, viongozi wamewaangusha wananchi. Yanahitajika mabadiliko makubwa na ya haraka.

Nguvu ya wananchi ndiyo mwamuzi. Wananchi wamemkubali Rais Kikwete. Kwa sababu hiyo, hana shaka ya kuwa mwoga. Amiri Jeshi anayekwenda vitani, akijua wananchi, wapiganaji na makamanda wake wanamuunga mkono, hawezi kuwa na shaka ya ushindi.

Kwa hakika, huu ni wakati sasa wa Rais wetu kuonyesha kuwa yale mamilioni ya kura, hakuyapata kwa bahati mbaya.

Wabunge wameonyesha mfano wa namna nchi inavyoweza kurejeshwa kwenye mstari. Tusiwaangushe. Wananchi lazima tuwe mstari wa mbele kuwaunga mkono, na kusema sasa kuonewa basi; kunyimwa maendeleo, sasa basi. Ukaidi wa viongozi, sasa basi. Wananchi wakiamua, hakuna litakaloshindikana. Kwa pamoja, Tanzania tutaibadili.

manyerere@hotmail.com
0713 335469




No comments: