Friday, May 02, 2008



Kuenea kwa ufisadi na

vyombo vya usalama

viko wapi?



Na Charles Kayoka

UNAPOFUATILIA habari za ufisadi na jinsi ulivyojikita miongoni mwa wale tuliowakabidhi dhamana ya kuiongoza nchi hii, au wale ambao tulidhani ndio watakaotusaidia kuiondoa nchi hii kutoka katika lindi la umasikini, magonjwa na ujinga, moja ya hitimisho unaloweza kulifanya ni kusema idara zetu za usalama zinafanya shughuli ya kulinda maslahi ya wale tuliowapigia kura na kuwa wakubwa kuliko sisi tuliowaweka madarakani.

La kwanza linalojionyesha ni kuwa tabia ya ufisadi haikuanza leo; imeota mizizi na ilifikia wakati likawa ni jambo la kawaida kwa wale waliojitangazia ukubwa na kutogusika kuendelea kufuja mali za umma na kuwanyonya walala hoi bila kujali kwani walijua kuwa hawawezi kushikwa wala kuadhibiwa.

Kuna wakati tuliamini kuwa kazi za idara ya usalama wa taifa- ikiwemo usalama wa taifa wenyewe, polisi, tume za kuzuia na kudhibiti rushwa na jeshi- ni kulinda maslahi ya taifa kwa kuwachunga maadui wa ndani na wa nje.

Tumekuwa makini sana katika suala ya madui wa nje lakini hili la maadui wa ndani linaonekana kushindikana. Pengine idara husika haijajua adui wa ndani ana sifa gani ili aweze kuingizwa katika orodha ya watu hatari.

Unapokuwa na afisa wa serikali ambaye amepewa madaraka ya umma ya kulinda rasilimali zetu kwa kuhakikisha kuwa anasaini mikataba ambayo haitafikia kuifilisi nchi; na kuwa mikataba hiyo haitazalisha kundi kuwa la watu wasio na kazi au kuwa na manung´uniko dhidi ya serikali yao, n.k. Lakini hafanyi hivyo na badala yake anaamua kuwa upande wa wawekezaji na kuanza kuwafundisha namna ya kukwepa kodi; anawasaidia wawekezaji kupata rasilimali zetu kwa chee; na matokeo yake ni kuikosesha serikali mapato na kuwafanya Watanzania kuendelea kuishi katika hali ya dhiki, kwa mawazo yangu hili ni suala la usalama na vyombo vya usalama vinapaswa kulifanyia kazi.

Pengine dhana ya usalama inatofautiana kati ya ile niliyonayo mimi na ya idara husika; na ile ya wakati wa Nyerere na hii ya sasa. Wakati ule tuliamini kuwa kazi za idara hizi, pamoja na majukumu mengine makubwa, ilikuwa ni kuhakikisha kuwa hakuna kiongozi anayejilimbikizia mali kwa njia isiyo halali.

Na ilifika mahali tuliamini kuwa ukishaingizwa katika utumishi wa umma, na hasa ule wa ngazi ya juu, wenzetu hawa walikuwa wamekufanyia utafiti wa kutosha kuhusu uadilifu wako na tabia yako kwa misingi ya uzalendo na uaminifu.

Tulidhani kuwa haikuiishia hapo, mtu uliendelea kuwekwa chini ya kurunzi la waheshimiwa hawa na kila unapokosea jambo fulani lingefanywa kukurekebisha, na pengine kuondolewa kabisa katika madaraka yako.

Kwa kadri tunavyoona mambo yanavyokwenda kwa sasa idara hizi hazifanyi kazi yake na tunadhani kwa wakati huu wameamua na wao kushirikiana na wakubwa wale wale waliopaswa kuwachunguza. Mambo yote haya, mimi naamini, yamekuwa yakifanyika huku wao wakijua fika nini kinafanywa na nani.

Tulidhani kuwa maana ya usalama wa taifa ni pamoja na kuzuia ufisadi ambao matokeo yake ni kuzalisha matajiri wachache na kuwaaacha wananchi wengi nje ya mfumo; maana ya usalama wa taifa ni kuhakikisha kuwa serikal inapata fedha zote halali na kuwa mikataba yote inakuwa ile ya kuifanya nchi kulinda rasilimali zake ili serikali iweze kuongeza pato la taifa na hivyo kuongeza unene wa bajeti; na kuwa usalama wa taifa ni pamoja na kuhakikisha kuwa idadi ya watu wasio na kazi wanapungua kabisa kwani ikiongezeka kuna uwezekano wa kuchafua hali ya hewa na hawa wazururaji wanaweza kutumika kuchafua amani ya nchi; kuwa usalama wa taifa unahakikisha kuwa bajeti iliyopangwa kwa ajili ya mipango na miradi mbalimbali ya maendeleo ya taifa inatumika ipasavyo na wale wanaoihujumu wanapata adhabu kali.

Inawezekanaje kuwa kiongozi aliyepewa dhamana ya kuiendesha nchi anaamua kuihujumu bajeti kwa kutumia fedha anavyotaka; au anaamua kujimilikisha mradi wa umma bila woga na huku idara husika ikimwangalia bila kumchukulia hatua.

Mimi nilidhani kazi nyingine ya usalama wa taifa ni pamoja na kulinda misingi ya maadili ya taifa na kuhakikisha kuwa viongozi walio walafi wanaondolewa madarakani ili wasije wakatuambukiza sisi tulio nje ya mifumo na hatimaye kudhani kuwa kula fedha za umma na kuhujumu miradi ya maendeleo ni sehemu ya bakshishi za ukubwa.

Yapi maadili ya taifa na nani wa kuyalinda kama taasisi hizi nyeti zilizopewa mamlaka makubwa zinanyamaza na kufumba macho na kuwalinda wakubwa, ndugu na jamaa zao.

Kama wakubwa na wadogo walio ndani ya serikali wanawaona wawekezaji ni muhimu kuliko maslahi ya taifa kimaendeleo; kama miradi ya uvunaji rasilimali hapa nchini inaweza kuwafanya raia wa nchi hii wasiwe na kazi- hasa wakulima ambao hawana ujuzi wa kujiajiri- kwa kukosa elimu na ujuzi zaidi ya kilimo na ufugaji wa mazoea; kama wananchi wanaposubiri fidia ya ardhi yao wanaachwa wateseke na hata wanapolalamika au kuandamana kudai haki wanashitakiwa kwa uvunjifu wa amani; lakini huyu aliyeamua asiwalipe maslahi yao au kuchelewesha, haonekani kuwa ni chanzo cha uvunjifu wa amani.

Sera na utendaji wa serikali unaposababisha mtu masikini akose ajira, ashindwe kujikimu, na kutopata haki sawa katika mfumo wa maslahi ya taifa, ni wazi hili ni suala la usalama wa taifa.

Kwa dalili hizi inaonyesha kuwa kuna ukungu ambao unaweza ksuababisha vurugu kubwa muda mfupi ujao kama hatua madhubuti hazitachukuliwa sasa wa kuikemea serikali ambayo inazembea.

Nina wasiwasi kama kweli waheshimiwa hawa wanaelewa wajibu wao. Na kama wanaelewa, basi wameamua kuiacha nchi hii igeuzwe kuwa mradi wa kujikimu wa wakubwa na wawekezaji kutoka nje.

Mustakabali wa nchi hii kwa kweli unakwenda kombo kwani ongezeko la umasikini; ongezeko la kukosekana kwa ajira; linaanza kuzua vitendo ambavyo vitauweka usalama wa taifa katika muhali.

Nadhani umefika wakati watafakari na kuona marekebisho gani wayafanye ya watendaji, utendaji na majukumu miongoni mwao. Huko tunakokwenda tutakuja kuwalaumu wao, sio serikali na chama tawala.

Baruapepe: mohamedmusta@gmail.com

Simu: 0755-833-933

No comments: