Mhadhiri Chuo
Kikuu Dar ataka
mdahalo wa

Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dk. Sengondo Mvungi, ameishauri Serikali ya Muungano kuitisha mdahalo utakaowezesha kumaliza utata kuhusiana na hoja ya kama Zanzibar ni nchi ama la.
Dk. Mvungi amesema kuwa bila kufanya hivyo, malalamiko kuhusiana na hoja hiyo yataendelea kushika kasi siku hadi siku.
Mhadhiri huyo wa sheria alikuwa akihojiwa na kituo kimoja cha redio hapa jijini.
Dk. Mvungi ambaye amewahi kugombea urais mwaka 2005 kupitia chama cha NCCR-Mageuzi, amesema mdahalo ndio njia pekee ya kumaliza suala hilo.
Hoja ya Zanzibar sio nchi ilianzia bungeni mjini Dodoma wakati Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda akijibu maswali ya wabunge kama utaratibu wake alivyojiwekea.
Swali hilo ambalo liliulizwa na mbunge mmoja wa CUF, lilijibiwa na Waziri Pinda kuwa Zanzibar sio nchi.
Tangu kutolewa kwa majibu hayo, hoja mbalimbali zimekuwa zikitolewa kuhusiana na suala hilo.
Mwanasheria mkuu wa Zanzibar, Bw. Pandu Hassan alikaririwa akisema Zanzibar ni nchi, kabla ya wajumbe wa Baraza la wawakilishi kuchachamaa zaidi.
Hata pale, spika wa baraza la wawakilishi alipopiga `stop` suala hilo kuendelea kujadiliwa, wajumbe wa baraza waliendelea kuchomekea suala hilo kabla baadaye kutakiwa liachwe kwa wanasheria wa pande zote mbili ili wakae na kuyatolea ufafanuzi muafaka.
- SOURCE: Alasiri
No comments:
Post a Comment