Nape Ruksa Kukata
Rufaa kama
Hukuridhika na
Uamuzi- Rais Kikwete
Rais Kikwete, Mwenyekiti wa CCM mjini Dodoma jana,
kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM.
MWENYEKITI wa CCM, Jakaya Kikwete (Pichani) amempa ruksa mwanasiasa kinda wa chama hicho, Nape Moses Nnauye kukata rufaa iwapo anaona hakuridhika na uamuzi wa kumvua uanachama wa Umoja wa Vijana wa chama hicho, UVCCM, akitofautiana na katibu wake, Yusuf Makamba, ambaye alisema kijana huyo hawezi kukata rufaa katika chombo chochote.
Rais Kikwete Kikwete, akitoa taarifa fupi kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM(NEC) jana, pia alisema chama hicho tawala kitaendelea kumtambua Nape kama mjumbe wake, mwanachama na kutambua nyadhifa zake zote ndani ya CCM, tofauti na mapendekezo ya Baraza Kuu la UVCCM lililotaka mtoto huyo wa mwanasiasa aliyekuwa na ushawishi mkubwa ndani ya chama hicho,marehemu Moses Nnauye, avuliwe nyadhifa zake zote.
Baraza hilo, ambalo lilimjumuisha Makamba, ambaye ni mtendaji mkuu wa CCM na mwanasiasa mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombare Mwiru, ambaye ni kaimu kamanda wa vijana Tanzania Bara, lilimvua Nape uanachama na kupendekeza avuliwe nyadhifa nyingine zote ndani ya CCM kwa madai kuwa alisema uongo alipotoa tuhuma nzito kuwa mkataba wa uwekezaji wa jengo la makao makuu ya UV-CCM unanuka rushwa.
Lakini jana, kwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka ndani ya kikao cha NEC kilichofanyika mjini Dodoma, Rais Kikwete, ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliuambia mkutano huo kuwa Halmashauri Kuu inamtambua Nape kama mjumbe halali, mwanachama wa CCM na pia inatambua nyadhifa zake zote ndani ya chama na kwamba kijana huyo machachari anayo haki ya kukata rufaa kupinga maamuzi ya Baraza Kuu la UV-CCM. Habari na Ramadhan Semtawa
No comments:
Post a Comment