Tuesday, October 07, 2008


Usalama wa Taifa na

ufisadi unaoendelea nchini



Na Stephano Mango 

KUNA maneno matatu, dola, nchi, Taifa ambayo kimsingi inawezekana ukayafananisha lakini katika maana ukapata moja. 

Taifa kama inavyojulikana maana yake na watu wengi kuwa ni jumuiya ya watu wanayoishi katika kipande cha ardhi chenye mipaka maalumu ambayo inatambulika rasmi na mataifa mengine. 

Kimsingi Taifa hufanya mambo yake ndani ya mipaka yake na hutumia vyombo kadhaa kuendesha shughuli zake na kulinda maslahi ya wanataifa dhidi ya maadui wa ndani au nje. 

Katika Taifa kuna mihimili mitatu ambayo ni Serikali, Bunge na mahakama na mara nyingi wadau wa habari tunaongeza mhimili mwingine wa nne, yaani vyombo vya habari. 

Serikali ndiyo mhimili wa kiutendaji na hivyo husimamia vyombo kadhaa katika utendaji huo, vyombo hivyo mara nyingi huitwa vyombo vya dola au vya usalama , hii ni pamoja na majeshi ya ulinzi na usalama yaliyo nchini mwetu. 

Tanzania tuna Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambalo kimsingi linahusika katika kulinda nchi yetu na mipaka yetu dhidi ya maadui wa nje na inapobidi kuingia vitani ili kulinda nchi na rasilimali zake. 

Tuna Jeshi la Polisi ambalo ndani yake kuna vikosi kama kikosi cha usalama barabarani, kikosi cha kutuliza ghasia, hawa kimsingi wapo kwa ajili ya usalama wa raia na mali zao. 

Tunalo Jeshi la Magereza ambalo limepewa jukumu la kuwahifadhi wahalifu na kuwafundisha maadili mema wanapotumikia vifungo vyao na kuwafanya warejee katika jamii wakiwa na tabia njema na stahiki katika jamii zetu. 

Kuna Idara ya Usalama wa Taifa (Tanzania Intelligence & Security Service = TISS), wengi tunafahamu majukumu ya chombo hiki kinadharia tu, maana shughuli zake hazionekani moja kwa moja hadharani kwani hufanya kazi kwa siri. 

Vyovyote ilivyo, Watanzania tunaamini usalama wa Taifa unamlenga kila mmoja wetu, unalenga uhifadhi wa rasilimali zetu kwa maslahi ya umma na kulinda haki ya kila mmoja wetu, awe raia huru au raia anayetumikia kifungo na ndio maana tunawalipa na wanatumia kodi zetu kwa kuwa wanatulinda na kuhakikisha rasilimali zetu hazikwapuliwi na manyang'au wachache. 

Usalama wa Taifa una kazi nyingi katika Taifa letu ikiwemo kuhakikisha na kulinda watu wake na rasilimali za Taifa letu kwa manufaa ya Watanzania wote bila kujali itikadi. 

Lakini cha kushangaza ni kuwa, wizi wa kalamu katika ofisi za umma unazidi kushamiri kila kukicha, ufisadi unazidi kustawi kupitia mikataba ya mibovu ambayo inasainiwa kati ya wezi wa ughaibuni na walio hapa nchini. 

Taifa linaendelea kuuzwa vipande vipande na umasikini unazidi kukithiri katika nyanja zote. Kuna kashfa nyingi hapa nchini, hebu rejea mikataba mibovu ya IPTL, Richmond, Alex Stewarts, Meremeta, Kiwira Coal Mines ,Aggreko. 

Mwananchi Goldmines , Songas Dowans , Kagoda Agriculture Ltd na wizi ambao unafanywa katika taasisi nyeti za Serikali ikiwemo BoT na kwingineko. 

Ingawa jambo la kushangaza usalama wa Taifa wapo na kwa namna moja au nyingine wameshindwa kuzuia ufisadi na ubadhilifu usitokee ama baada ya kutokea wameshindwa kuchukua hatua stahiki, ni jambo la kujiuliza ni usalama upi wa Taifa unaoshughulikia usalama wa nchi yetu . 
============= 
Ambapo wengi wanazidi kuwa na maumivu katika nafsi zao kutokana na umasikini na wachache wanaendelea kuneemeka? Usalama wa Taifa upo wapi katika lindi la wizi wa fedha za Taifa? Na masononeko ya wananchi katika kuchukua hatua kwa wale waliobainika kuiba na kufilisi nchi yetu? Kweli kuna usalama wa Taifa au uhasama wa Taifa. 
=========== 
Nani mwenye akili timamu atakaye elewa kazi za usalama wa Taifa katika lindi la ubadhilifu na kifisadi? Wapo wapi kuchukua hatua? Ilikuwaje mpaka mabilioni ya fedha yanayeyuka kienyeji hivi? Hawana aibu kukaa kimya baada ya wananchi kuwazomea mafisadi na kutaka hatua zichukuliwe? 

Hata hivyo tukiwa tunataka ukweli na uwazi katika kampuni ambazo zimefanya ubadhilifu, ufisadi wa fedha za umma, ikiwepo Kampuni ya Meremeta tumeshtushwa na kauli ya Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda aliyowahi kuitoa bungeni. 

Baada ya wananchi kuibana Serikali kupitia kwa wawakilishi wao yaani wabunge na kuitaka Serikali hiyo kuwataja wamiliki wa kampuni zote ambazo yametajwa kwa nyakati tofauti kufilisi nchi yetu. 

Waziri Mkuu, Bw. Pinda alilazimika kuwaambia wabunge kuwa hawezi kujibu hoja zozote juu ya Kampuni ya Meremeta na yupo wazi kusulubiwa na wabunge kuliko kuelezea kwa undani suala hilo kwani ni siri na pia linahusisha na Usalama wa Taifa kwa kuwa kampuni hiyo inamilikiwa na JWTZ. 

Ni ukweli ulio wazi kuwa, Waziri Pinda ametoa kauli yenye kitisho kwa wale wanaohoji suala la Kampuni ya Meremeta na kuificha kauli yake katika mbawa ya Usalama wa Taifa na kusema kuwa ni siri na inahusu Jeshi. 

Waziri Pinda ameshidwa kueleza kinagaubaga shughuli za Kampuni ya Meremeta bali kuipapasa kampuni hiyo kwa kusema inajishughulisha na uchimbaji wa dhahabu na inamilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. 

Kimsingi kauli ya Waziri Pinda inamaanisha kuwa usalama wa Taifa umebinafsishwa na upo mikononi mwa wageni kutokana na ushahidi wa kimazingira na kimaandishi ambao upo. 

Kimsingi Kampuni ya Meremeta inaaminika ilikuwa inafanya shughuli zake kwa maslahi ya wakubwa wachache, ingawa hadi sasa ni mwaka wa saba kilio kinaendelea katika vijiji sita katika kata ya Buhemba Wilaya ya Musoma ambapo kuna mgodi wa dhahabu uliokuwa unamilikiwa na kampuni hiyo. 


Zaidi ya nyumba 100 zilivunjwa ili kupisha mgodi huo ambao ulitangazwa kuwa ni wa Serikali, zahanati iliyokuwa ikitoa huduma kwa wakazi wa vijiji hivyo ilivunjwa, shule ya msingi iliyokuwa na wanafunzi wapatao 600 wa darasa la kwanza hadi la saba ilivunjwa. 

Hata hivyo kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) iliyoitwa Buhemba ilivunjwa na askari walihamishwa kwa kutumia usafiri wa mikokoteni ambayo ilikuwa inakokotwa na ng`ombe. 

Ingawa mgodi wa dhahabu wa Buhemba umewanyanyasa wananchi na kuvuruga miundombinu ya elimu, afya pamoja na mfumo wa maisha wa wakazi wake kwa ujumla, kwa kuwa wananchi walishambuliwa kwa kupigwa na kukamatwa ovyo na walinzi wa kampuni kwa madai ya kuingia kwenye eneo la mgodi. 

Hata hivyo fedha ambazo zimechotwa au kuchotewa kutoka BoT chini ya kivuli cha Kampuni ya Meremeta ni kiwango kikubwa na cha kutisha katika ustawi wa nchi yetu na usalama wetu. 

Ingawa Waziri Pinda anataka wananchi kupitia wabunge wao waamini kuwa Meremeta ni kampuni ya kuchimba dhahabu ambayo ilikuwa inamilikiwa na Jeshi la Ulinzi la wananchi. 

Jambo hilo linapingana na matamko mbalimbali ambayo yamewahi kutolewa na viongozi siku za nyuma, kwa mfano Msajili wa Hazina amewahi kusema Meremeta haimo katika orodha ya mashirika ya umma.

Hata hivyo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za fedha za Serikali amekiri kuwa kampuni hiyo haijawahi kukaguliwa na Serikali kwa miaka saba sasa tangu itajwe kuwepo. 

Hata siku moja Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa haijawahi kuonesha au kutangaza hesabu za fedha ambazo zimetokana na uchimbaji wa dhahabu kupitia Kampuni ya Meremeta, jambo ambalo linathibitisha kuwa mradi ule ulikuwa wa watu wachache.

No comments: