Wednesday, December 31, 2008

JK ashtushwa na

mauaji ya mamia

ya Wapalestina


Rais Jakaya Kikwete


Na Ramadhan Semtawa

SIKU chache baada ya Israel kufanya mauaji ya kinyama dhidi ya Wapalestina zaidi ya 370 kwa kutumia ndege zake za kivita katika Ukanda wa Gaza, Rais Jakaya Kikwete, ametuma salamu za rambi rambi kwa Rais wa taifa hilo, Mahmoud Abbas, akieleza kushtushwa na mauaji hayo.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete, imekuja wakati tayari hali katika eneo la Ukanda wa Gaza ambako ni ngome ya Chama cha Hamas, ikiwa tete kufuatia mauaji hayo huku dunia ikitaka kusitishwa kwa machafuko.

Rais Kikwete katika salamu zake hizo kwa niaba ya serikali na Watanzania, zilizotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alisema licha ya kushtushwa, lakini hali ilivyo sasa inaweza kuathiri mpango wa kutafuta amani Mashariki ya Kati maarufu kama Road Map.

Katika kuonyesha msisitizo, rais alifafanua kwamba, alisoma kwa mshtuko na huzuni taarifa za mashambulizi mfululizo ya ndege za Israel katika Ukanda wa Gaza ambayo yaliua zaidi ya raia wa Palestina 375, huku yakiacha wengine majeruhi ambao ni pamoja na wanafunzi.

Rais alisema, mwendelezo huo wa hali ya mambo ilivyo kwa sasa, utaathiri mpango huo wa kuleta amani katika mgogoro wa Palestina na Israel na kuongeza kwamba, ameungana na Jumuiya ya Kimataifa ikiwemo ya wapenda amani kupinga mauaji hayo.

"Kwa niaba ya serikali, watu wa Tanzania na kwa niaba yangu, ningependa kutuma salamu kwako na watu wa Palestina na familia za wapendwa wetu, kueleza majonzi na simanzi kwa hasara iliyotokea," ilisema taarifa hiyo ikimnukuu Rais Kikwete.

Akionyesha msisitizo, Rais alisema Tanzania iko pamoja na watu wa Palestina katika kuugulia maumivu hayo.

Juzi Israel ilifanya mauaji ya kinyama dhidi ya raia wasiokuwa wapiganaji wa Hamas, kutokana na kile ilichokieleza kwamba ni kujibu mapigo kufuatia chama hicho ambacho kina ngome katika Ukanda wa Gaza, kufyatua roketi kuelekea Israel; ni hatua ambayo inaweza kuathiri mpango wa amani wa Road Map.

Kutoka Mwananchi


No comments: